Warembo wa Miss Tanzania kutengeneza maktaba ya watoto Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)

Miss Tanzania (2000) Jacqueline  Mengi akimsikiliza Winifrida Kusekwa ambaye mtoto wake Collean Yakwala amelazwa  katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya matibabu  wakati mamiss  Tanzania wa miaka mbalimbali  walipotembelea Taasisi hiyo leo kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia watoto wanaotibiwa katika Hospitali hiyo. 

Na Anna Nkinda

Warembo waliowahi kushinda taji la Miss Tanzania miaka mbalimbali, wakiongozwa na Miss Tanzania wa mwaka 2000, Jaqueline Ntuyabaliwe wameahidi kutengeneza maktaba na kuweka vitabu kwa ajili ya watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). 

Akizungumza mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, Jaqueline amesema mwaka huu anatimiza miaka 20 tangu aliposhinda taji hilo kwa kushirikiana na wenzake ameona vema kutengeneza maktaba hiyo ili kuisadia jamii.

 “Nimefika hapa ili kuwasilisha wazo letu la mradi ambao tutautoa kama msaada kwa hospitali yetu, nasema yetu kwa sababu sisi sote ni Watanzania inatuhudumia,” amesema Jackqueline ambaye pia ni Mjasiriamali.

Ameongeza “Hivyo, tulikaa tukakubaliana mwaka huu tutatoa msaada kwa wazazi na watoto, tuliona sehemu nzuri ni kuja hapa, tulifikiria kuna matatizo mbalimbali, kwa utashi wetu tuliona vizuri tutengeneze maktaba na kutoa vitabu viweze kuwasaidia watoto wanaokuwa wamelazwa kwa muda mrefu.

“Tunajua kuna wanaougua moyo, saratani na magonjwa mengine wanakaa kwa muda mrefu, mazingira ya ugonjwa huwa ni magumu hata kwa watu wazima.

“Na ndiyo maana tulifikiria nini tunaweza kufanya kuwasaidia hawa watoto wakiwa hapa hospitali maisha yao yaweze kuwa marahisi kidogo, tutengeneze mazingira ambayo yanaweza kuwapa furaha,” amesema.

Jackqueline ameongeza “Mimi nina taasisi ya Dk. Ntuyabaliwe, niliianzisha kwa ajili ya kumbukumbu ya baba yangu ambaye pia aliwahi kuwa daktari wa kina mama Muhimbili.

“Alipenda kusoma vitabu na nilipokuwa nakua nilikuwa nasoma vitabu karibu kila siku, kwa hiyo kupitia taasisi hii kazi yetu ni kutengenza maktaba na kugawa vitabu hapa Tanzania, tumeshafanya kwa shule nyingi hapa Dar es Salaam , Morogoro na Dodoma.

“Kwa hiyo nikasema kwa kushirikiana na wenzangu tunaweza kutengeneza kitu kikubwa zaidi kikawa kinaleta kumbukumbu ya muda mrefu, tukakubaliana kuleta hiyo maktaba,” amebainisha.

Amesema wamefurahi mno kwani wamepokewa vizuri na uongozi wa JKCI juu ya wazo lao hilo wanalokusudia kulifanya kwani limeonekana lina manufaa kwa watoto wa Tanzania.

“Tutashirikiana vizuri na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ili maktaba hii iwanufaishe watoto wote wanaokaa hapa hospitalini wakitibiwa, wanaolazwa kwa magonjwa ya muda mrefu itawasaidia,” amesema.

Amesema pia wanakusudia kutoa misaada mingine kwa watoto wanaozaliwa kabla ya kutimia umri (njiti) pamoja na wodi ya wazazi.

“Novemba 14, mwaka huu tutafanya ‘fund raising’ (harambee) kwa ajili ya kukusanya fedha kufanikisha wazo hili, tuna imani Watanzania watatuunga mkono.

“Beauty legacy tunapenda kurudisha fadhira kwa jamii yetu, sisi wengine ni kina mama tayari hata wenzetu ambao bado hawajawa wakina mama wanafahamu kuna changamoto, tutatumia majina yetu kukusanya fedha ili tuweze kusaidia watanzania wote.

Pamoja na hili, Jaqueline amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali na wadau wake katika ujenzi wa taasisi hiyo.

“Jinsi ‘facility’ ya taasisi ya moyo ilivyo ni ‘very modern’ (ya kisasa), ukiingia humu huwezi kujua kama ni Tanzania utadhani upo Ulaya, napongeza wote walioshiriki kuhakikisha haya mabadiliko yametokea.

“Kwa mtanzania yoyote hata kama hajawahi kufika hapa anaweza kujivunia juu ya hili, ni taasisi inayofanya vizuri, sehemu ambayo unaweza kupata huduma ukiwa mgonjwa unatoka ukiwa umepona.

“Watu kuugua ni kitu ambacho binafsi nimezoea kukiona lakini kuona hii ‘facility’ ni kitu kipya kwangu nimefurahi kuwepo hapa leo,” amesema.

Naye, Prof. Mohamed Janabi amesema Jaqueline aliwasilisha ombi hilo wiki mbili zilizopita na hawakusita kumwambia waje kwenye taasisi yetu.

“Kwa sababu sisi tuna watoto wengine wanakaa muda mrefu, wapo wanaokuja wakiwa na shida nyingine kama nimonia, hatuwezi kuwafanyia upasuaji mpaka tutibu shida nyingine kwanza na wengine baada ya kufanya upasuaji wanakaa wodini muda mrefu.

“Kuwa na maktaba ndogo itakayowasaidia kusoma vitabu, kuandika na mengineyo ni sehemu ya tiba, nchi za wenzetu wana kitu kinaitwa rehabiritation post-operative (yaani baada ya kupasualiwa), sasa kama mtoto alikuwa shule, ataendelea kusoma hapa.

“Vitawasaidia katika kipindi wanachopitia kupata unafuu kabla ya kurudi nyumbani, tumelipokea wazo lao ni zuri na ndiyo maana tumewapeleka kila mahala.

“Ujio wao tunautumia fursa ya kujitangaza pia natumaini watakuwa mabalozi wazuri kuanzia sasa na kuendeleza, kwa sababu library’ ni kitu watakiona kila mara na watakuja na mawazo ya kuiboresha, inaweza kuja kuwa na video games na vitu vinginevyo.

“Itatusaidia kupunguza stress ya watoto na wazazi wanapokuwa wakijitayarisha kwa matibabu ya moyo, tunawashukuru mno kwa kuja, imani yangu hiki kitu kitafanyika mapema mwaka huu,” amesema.

Mkuu wa kitengo cha  Uuguzi  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Flora Kasembe akiwaonesha mamimiss Tanzania wa miaka mbalimbali namna ambavyo mashine ya kusaidia kupumua (ventilator) inavyotumika kwa wagonjwa waliolazwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) walipotembelea Taasisi hiyo leo kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia watoto wanaotibiwa katika Hospitali hiyo.

Daktari bingwa wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Palvina Kazaura akiwaeleza mamimiss Tanzania  wa miaka mbalimbali jinsi mashine ya kipimo cha kuangalia moyo unavyofanya kazi (Echocardiography ) inavyotumika  kwa watoto wanaotibiwa katika Hospitali hiyo. Mamiss hao walitembelea JKCI kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kuangalia  ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia watoto wanaotibiwa mahali hapo.

Mamiss Tanzania wa miaka mbalimbali wakitoka katika jengo la kliniki ya watoto wakati wa ziara yao ya kutembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kuangalia  ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia watoto wanaotibiwa katika Hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kuwatengenezea maktaba. 
Daktari bingwa wa wagonjwa waliopo katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Amanda Anyoti akiwaeleza  mamimiss Tanzania wa miaka mbalimbali huduma za matibabu wanazozitoa kwa wagonjwa waliotoka kufanyiwa upasuaji wa moyo. Mamiss hao walitembelea JKCI kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kuangalia  ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia watoto wanaotibiwa mahali hapo.

Mkuu wa kitengo cha  Uuguzi  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Flora Kasembe akiwaonesha mamimiss Tanzania wa miaka mbalimbali kitanda cha wagonjwa wa moyo kilichopo katika chumba cha watu maarufu (VIP) ambacho ni kimoja wapo ya vitanda vinavyotumiwa na wagonjwa wa Taasisi hiyo walipotembelea JKCI leo kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia watoto wanaotibiwa katika Hospitali hiyo. 

Mkuu wa kitengo cha  Uuguzi  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Flora Kasembe akiwaonesha mamimiss Tanzania wa miaka mbalimbali kitanda cha wagonjwa wa moyo kilichopo katika chumba cha watu maarufu (VIP) ambacho ni kimoja wapo ya vitanda vinavyotumiwa na wagonjwa wa Taasisi hiyo walipotembelea JKCI leo kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia watoto wanaotibiwa katika Hospitali hiyo. 

Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi hiyo na mamiss Tanzania wa miaka mbalimbali mara baada ya kumaliza ziara yao ya kutembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kuangalia  ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia watoto wanaotibiwa mahali hapo. Kushoto ni mama wa mtoto.

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari