Walimu nchini wapewa mbinu zitakazowawezesha kufaidi matunda ya uchumi wa kati katika miaka ijayo
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akitoa mada
kuhusu magonjwa ya moyo na jinsi ya kuyaepuka kwa walimu waliohudhuria mkutano
wa walimu wakuu wa shule za sekondari nchini uliofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Jakaya Kikwete uliopo jijini Dodoma. JKCI imeshiriki katika mkutano
huo kwa kufanya upimaji wa viashiria vya magonjwa ya moyo pamoja na kutoa uelewa (awareness) wa magojwa hayo.
Walimu
nchini wamepewa mbinu zitakazowawezesha kufaidi matunda ya uchumi wa kati
katika miaka ijayo, miongoni mwa mambo muhimu waliyohimizwa kuyazingatia ni
kutunza afya zao.
Wamehimizwa
pia kuepuka uzito uliokithiri na kufanya mara kwa mara uchunguzi wa afya ili
kujua hali zao na kutibiwa mapema ikiwa watagundulika tayari wameanza
kushambuliwa na magonjwa mbalimbali hususan yasiyoambukiza ambayo hivi sasa ni
janga la dunia.
Rai hiyo
imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI),
Profesa. Mohamed Janabi, alipowasilisha mada wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu
wa 15 wa Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA).
Mkutano huo
unaofanyika jijini hapa kwa muda wa siku tatu tangu jana (Desemba 20)
ukitarajiwa kuhitimika Desemba 22, mwaka
huu umepewa kauli mbiu isemayo ‘Elimu Bora na Umuhimu Wake katika Maendeleo ya
Uchumi wa Kati’
“JKCI
tumealikwa katika mkutano huu kuwasilisha mada kuhusu magonjwa yasiyoambukiza
na kutoa huduma ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo, hatukusita kuja.
“Tangu
tulipoanza leo (jana) asubuhi hadi sasa (saa tano) ambapo mimi pia nimewaona
walimu kadhaa, tumeona walimu 40, asilimia 37 ya walimu hawa tumewakuta wana
uzito mkubwa (obesity) na asilimia 37.5 wana shinikizo kubwa la damu na
hawakuwa wanajua hali zao kwamba ni wagonjwa.
“Kwa hali
hii, tunapenda kutoa tahadhari kubwa kwa walimu wetu kwamba wanapaswa kuchukua
hatua, nchi yetu ipo uchumi wa kati, kufaidi matunda yake lazima tutunze,
watunze afya zao,” alisisitiza.
Aliongeza
“‘Presha’ ni ugonjwa ambao hauna dalili na wengi hapa tumewakuta wanaugua
tayari lakini walikuwa hawajui kwa sababu hawakuwa na dalili zozote.
“Wengine
huwa wanasema kuumwa kichwa ni dalili ya ‘presha’, sikubaliani nao sana kwa
sababu, kwa mfano nikiwa sina hela kichwa, wengine wakiwa na njaa kichwa
kinauma.
“Hatari yake
ni kwamba kitu chochote kikitokea, kikampa msongo wa mawazo mtu mwenye ‘presha’
na hajui hali yake, zile ‘stress’ zitaongezeka na itaweza kupasua mishipa yote
ya damu,” alisema.
Prof. Janabi
aliwahimiza kwamba kinga ni muhimu kuliko tiba katika kukabiliana na magonjwa
hayo kwani gharama zake za matibabu ni kubwa.
“Matibabu
dhidi ya magonjwa haya ni ghali na ndiyo maana nimesisitiza kwamba wakate bima
ya afya kama ambavyo Serikali inaelekeza na inavyoelekea huko,” alisema.
Aliongeza
“Imani yetu, walimu hawa ni wakuu wa shule, watakaporudi kule kwenye shule zao,
watakwenda kuwaeleza walimu wao na walimu watawaeleza wanafunzi wao na
wanafunzi watakwenda kueleza nyumbani kwao, elimu sahihi itaifikia jamii.
Aliongeza
“Wazingatie wanatembea ‘steps’ (hatua) 10,000 kwa siku, wachunguze afya zao
mara kwa mara, wazingatie ulaji unaofaa, ili kuepuka magonjwa haya.
“Lakini kwa
wale ambao ni wagonjwa ni muhimu wazingatie matumizi ya dawa kama
walivyoelekezwa na madaktari wao, shinikizo la damu ni tatizo lililopewa jina
‘silent killer’ (unaua taratibu).
“Dalili zake
huchelewa kujitokeza kwa walio wengi, na ndiyo maana kitaalamu tunazungumzia
moja ya tatu, kwa maana kwamba ukiwa na wagonjwa 90, yaani 30 kati yao huwa
hawajijui, kundi jingine la watu 30 hawatumii dawa ipasavyo na kundi jingine la
watu 30 wanatumia dawa.
“Tunaelimisha
kwamba dhumuni letu, ni kuongeza hii idadi ya wagonjwa wa shinikizo la damu
wanaotumia dawa kwa usahihi katika kukabiliana na tatizo hili,” alisema Prof.
Janabi.
Comments
Post a Comment