Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) yaombwa kufikisha uelewa wa magonjwa ya moyo mashuleni

 

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Winnie Masakuya akitoa uelewa wa jinsi ya kutunza moyo ili uwe na afya njema kwa  walimu wakuu wa shule za Sekondari nchini waliofika katika banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kupima viashiria vya magojwa ya moyo wakati wa mkutano wa walimu hao unaomalizika hivi karibuni jijini Dodoma.


Walimu wakuu wa shule za Sekondari nchini wameiomba Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuhakikisha uelewa wa magonjwa ya moyo unatolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na siyo kwa watu wazima peke yao.

Wamesema uelewa wa magonjwa hayo ukiwafikia wanafunzi utawasaidia kuitunza mioyo yao na hivyo kuweza kuishi maisha marefu zaidi tofauti na inavyofanyika kwa sasa ambapo uelewa unatolewa kwa watu wazima wengi wao wakiwa na umri wa kuanzia miaka 35 na kuendelea.

Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na baadhi ya walimu waliohudhuria mkutano wa 15 wa walimu wakuu wa shule za sekondari nchini uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete uliopo jijini Dodoma.

Walimu hao walisema ili kuwa na Taifa lenye afya njema ni vyema uelewa ukatolewa kwa makundi yote kwenye jamii wakiwemo vijana walioko shule za msingi na sekondari kwani wao ni wepesi wa kuelewa na kuyafanyia kazi maelekezo wanayopewa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kabugaro iliyopo mkoani Kagera, Lucas Kajuna alisema wataalamu wa afya wanajitahidi kuelimisha wananchi lakini bado uelewa wa magonjwa hayo ni mdogo nchini.

“Hasa kwa wengi waishio vijijini ambao hawawezi kupata taarifa hizo kupitia vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, redio na Televisheni,”alisema.

Mwalimu Kajuna aliongeza “Hivi sasa maisha yetu Watanzania wengi yamebadilika tuna magari hata wale ambao hawana wanatumia usafiri wa umma, bodaboda au bajaji, wengi hatufanyi  mazoezi hata ya kutembea, tunakula vizuri ila siyo vyakula vyenye afya.

“Je, kutokana na hali hii watanzania wangapi wanapata uelewa (awareness) wa magonjwa ya moyo ili waweze kuepukana nayo?”, alihoji Mwalimu Kajuna.

 Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mnolela iliyopo mkoani Lindi, Adelfina Mbonde, alisema hii ni mara ya pili kushiriki katika mkutano huo na ameshuhudia tofauti kubwa.

“Mkutano wa sasa umekuwa na mada nzuri ikiwemo ya jinsi ya kuepukana na magonjwa ya moyo iliyotolewa na Profesa Janabi (Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI) pamoja na kufanyiwa uchunguzi wa afya,”alisema.

Mwalimu huyo alisema kwa hatua hiyo imewasaidia kupata uelewa jinsi ya kujikinga na magonjwa hayo kwani mtu anapougua matibabu yake ni gharama kubwa.

“Ninaiomba Serikali itoe uelewa wa magonjwa haya kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi, binafsi nitakaporudi Lindi, nimekusudia kila mwaka kuhakikisha walimu na wanafunzi wa shule ninayoisimamia wanafikishiwa elimu hii kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, ili wapate uelewa,”alisisitiza.

Aliongeza “Katika shule yetu wamekuwa wakija wataalamu wanaotoa elimu kuhusu namna ya kuepuka magonjwa ya kuambukiza na hata malaria lakini kwa upande wa magonjwa yasiyoambukiza hawajawahi kutufikia,”.

Mkutano huo umeandaliwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Global Education Link, ambapo JKCI imeshiriki kutoa uelewa (awareness) kuhusu magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kufanya uchunguzi wa viashiria vya  magonjwa ya moyo kwa walimu 700.


Daktari bingwa wa magojwa ya moyo kwa watoto na mkuu wa kitengo cha mafunzo na utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  Naiz Majani akimwelekeza mwalimu mkuu wa shule ya sekondari umuhimu wa kula chakula bora kwa afya ya moyo wakati wa mkutano wa walimu hao uliomalizika hivi karibuni jijini Dodoma ambapo JKCI ilishiriki kwa kufanya upimaji wa viashiria vya magonjwa ya moyo  pamoja na kutoa uelewa (awareness) wa magojwa hayo kwa walimu 700.


Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Winnie Masakuya akimwelekeza mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Kyamulaile iliyopo mkoani Kagera Gerac  Henerico madhara ya mafuta katika mishipa ya damu ya moyo wakati wa mkutano wa walimu hao uliofanyika jijini Dodoma ambapo JKCI ilishiriki kwa kufanya upimaji wa viashiria vya magonjwa ya moyo  pamoja na kutoa uelewa (awareness) wa magojwa hayo kwa walimu 700.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Wamara akimweleza mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Kabugaro iliyopo mkoani Kagera Lucas Kajuna madhara ya uzito mkubwa katika afya ya moyo wakati wa mkutano wa walimu hao unaofanyika jijini Dodoma. JKCI ilishiriki  katika  mkutano huo kwa kufanya upimaji wa viashiria vya magonjwa ya moyo  pamoja na kutoa uelewa (awareness) wa magonjwa hayo kwa walimu 700.

Mwandishi wa kujitegemea wa habari za afya Veronica Mrema akimpima urefu mwalimu mkuu wa shule ya sekondari aliyehudhuria mkutano wa walimu wakuu wa shule za sekondari nchini uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete uliopo jijini Dodoma. JKCI imeshiriki katika mkutano huo kwa kufanya upimaji wa viashiria vya magonjwa ya moyo pamoja na kutoa uelewa (awareness) wa magojwa hayo  kwa walimu 700.

 

 

 

 


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari