WACHEZAJI 30 WA TIMU YA TAIFA CHINI YA MIAKA 20 NGORONGORO HEROES WAFANYIWA UCHUNGUZI WA MOYO
Baadhi ya wachezaji
wa timu ya taifa chini ya miaka 20
Ngorongoro Heroes wakiwa katika foleni ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo
leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Wachezaji 30 wa timu hiyo
walifanyiwa vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, umeme wa moyo
unavyofanya kazi na damu ikiwa ni mojawapo ya kutekeleza sheria ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kila mchezaji anayeshiriki mashindano hayo
kupima.
Fundi sanifu wa moyo
(Cardiovascular technologist) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Paschal
Kondi akimpima mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography –
ECG) mchezaji wa
timu ya taifa chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes Kimwe Kisare wakati timu hiyo
ilivyofika JKCI kwa ajili ya kuwafanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo kabla ya
kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika
nchini Mauritania mwezi Februari mwaka huu.
Wachezaji 30 wa timu ya Taifa chini ya
miaka 20 Ngorongoro Heroes wamefanyiwa uchuguzi wa kina wa magonjwa ya moyo
kama Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) linavyoelekeza kabla ya kuanza
kwa mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ni lazima wachezaji wanaoshiriki
mashindano hayo wapimwe afya zao.
Vipimo walivyofanyiwa wachezaji hao ni
vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph), mfumo wa umeme wa moyo
unavyofanya kazi (Electrocardiography –ECG), na vipimo mbalimbali vya damu
kuangalia afya ya mwili kwa ujumla. Upimaji huu umefanywa na madaktari bingwa
wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI).
Vipimo vya damu vilivyofanywa kwa
wachezaji hao ni pamoja na kuangalia kama kuna maambukizi yoyote kwenye damu,
kipimo cha kuangalia viwango vya mafuta katika mwili, kuchunguza madini ya
chumvi mwilini na kipimo cha kuangalia kiwango cha sukari mwilini.
Matokeo ya vipimo hivyo yatasaidia
kufahamu afya za wachezaji na utimamu wao wa kimwili kabla ya kwenda kushiriki
katika mashindano ya AFCON yanayotarajia kuanza tarehe 14/02/2021 huko nchini
Mauritania.
Tunatoa wito kwa vilabu vya mpira hapa
nchini kuwaleta wachezaji wao kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya
moyo hii itawasaidia wachezaji hao kufahamu kama wanamatatizo au la na
kuepukana na vifo vya ghafla vinavyoweza kuwapata wakiwa uwanjani. Kwa upande
wa wananchi kabla ya kujiunga na vilabu vya mazoezi ni muhimu wakapima afya zao
yakiwemo magonjwa ya moyo..
Comments
Post a Comment