Watoto wenye umri chini ya miaka mitano kuathirika na tatizo la misuli ya moyo (Dilated Cardiomyopathy - DCM)
Hayo yamebainishwa
katika utafiti uliofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Januari 2021 hadi Desemba 2025 uliangalia
taarifa za watoto waliolazwa JKCI wakiwa na ugonjwa huo kwa lengo la kuchambua
sifa za ugonjwa pamoja na matokeo ya matibabu yake.
Kwa mujibu wa utafiti
huo, jumla ya watoto 3,330 waliolazwa JKCI katika kipindi hicho watoto 45 sawa
na asilimia 1.4, waligundulika kuwa na tatizo la DCM, Hata hivyo watoto 10
waliondolewa katika utafiti kutokana na kutokamilika kwa taarifa zao za
kitabibu hivyo utafiti kujumuisha watoto 35.
Akizungumzia utafiti
huo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto aliyefanya utafiti huo Zawadi
Kalezi alisema matokeo yameonesha kuwa kati ya watoto 35 waliofanyiwa uchunguzi,
24 sawa na asilimia 68.6 walikuwa chini ya umri wa miaka mitano, huku wavulana
wakiwa wengi kwa asilimia 51.4.
Dkt. Zawadi alisema utafiti
ulibaini kuwa hali ya kuvimba kwa misuli ya moyo (myocarditis) ilikuwa sababu
iliyobainika mara nyingi zaidi ikihusisha watoto 15 sawa na asilimia 42.9 huku
sababu nyingine kuwa hitilafu za mpangilio wa mapigo ya moyo (arrhythmias)
iliyohusisha watoto watano sawa na asilimia 14.3 na watoto wengine 14 sawa na
asilimia 40 chanzo cha ugonjwa huo hakikuweza kubainika.
“Utafiti umeonesha kuwa
kiwango cha wastani cha uwezo wa moyo kusukuma damu (LVEF) kilikuwa asilimia 30
ikionesha udhaifu mkubwa wa kazi ya moyo kwa watoto hao”, alisema Dkt. Zawadi
Dkt. Zawadi alisema
utafiti umeonesha kuwa matibabu yalisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza dalili
za kushindwa kufanya kazi kwa moyo ambapo watoto 32 sawa na asilimia 91.4
walionesha kuimarika na kutokuwa tena na dalili za kushindwa kufanya kazi kwa
moyo wakati wa kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Dkt. Zawadi alisema
baada ya watoto hao kuruhusiwa kutoka hospitalini, wataalamu waliendelea
kuwafuatilia kwa kipindi cha miezi 18 ambapo watoto saba sawa na asilimia 25
walirejea katika hali ya kawaida ya utendaji wa moyo. Watoto 11 sawa na
asilimia 39.3, walionesha kuimarika kwa utendaji wa moyo, wakati watoto 10 sawa
na asilimia 35.7, hawakuonesha mabadiliko katika kiwango cha utendaji kazi wa
moyo.
“Utafiti umeonesha kuwa
ugonjwa huo unaweza kuwa na madhara makubwa kwani watoto watano sawa na
asilimia 14.3 walipata matatizo wakati wanalazwa ambapo wawili walipata
kiharusi na watatu walipata tatizo la ghafla la figo, aidha watoto watano walirudi
hospitalini kutokana na moyo kushindwa tena kufanya kazi vizuri”, alisema Dkt. Zawadi
Watafiti wameeleza kuwa
idadi kubwa ya watoto ambao chanzo cha DCM hakikubainika inaonesha umuhimu wa
kuimarisha uwezo wa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa watoto hususan vipimo vya
vinasaba (genetic testing) na MRI ya moyo, ambavyo vinaweza kusaidia kubaini
chanzo cha ugonjwa kwa watoto ambao sababu zake hazijulikani.
Utafiti huo
uliochapishwa mwezi Agosti 2026 katika jarida la Frontiers in Cardiovascular
Medicine unatoa picha ya hali ya ugonjwa wa DCM kwa watoto wanaopatiwa huduma
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) nchini na unaonesha umuhimu wa
utambuzi wa mapema, matibabu na ufuatiliaji wa karibu wa watoto wenye matatizo
ya moyo.
%20(1).jpeg)
Comments
Post a Comment