Wagonjwa 11 wafanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa bila kuusimamisha moyo kwenye kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Daktari
bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Sinha kutoka hospitali ya
Max iliyopo New Delhi nchini India akishirikiana na wataalamu wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupandikiza
mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery - CABG) kwa wagonjwa bila ya kuusimamisha moyo katika
kambi maalum ya siku 10 inayofanyika katika Taasisi hiyo.
Baadhi
ya wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wakifuatilia mafunzo ya upasuaji wa mshipa mkubwa wa damu wa kifuani (Thoracic and Abdominal
Aortic Aneurysm Dissection) yaliyokuwa yanatolewa leo na Daktari bingwa
wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Kumar Sinha kutoka Hospitali ya
Max iliyopo New Delhi nchini India. Mafunzo hayo yanaenda sambamba na kambi maalum ya upasuaji wa
moyo ya siku 10 inayofanyika katika Taasisi hiyo.
Na: JKCI
Wagonjwa 11 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa bila kuusimamisha moyo katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Sinha wa Hospitali ya MAX iliyopo New Delhi nchini India.
Kambi hii ya siku 10 ambayo inaenda sambamba na utoaji wa mafunzo na kubadilishana ujuzi kwa wataalamu wa upasuaji wa Taasisi yetu ilianza tarehe 10 na itamalizika tarehe 19 mwezi huu ambapo baadhi ya upasuaji unaofanyika ni ule ambao haufanyiki hapa nchini.
Upasuaji wa moyo unaofanyika katika kambi hii ni wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery - CABG) kwa wagonjwa ambao uwezo wa moyo wao kufanya kazi umepungua kwa kiwango cha chini cha asilimia 35.
Upasuaji wa aina hii unafanyika katika Taasisi yetu, tofauti iliyopo ni kuwa wataalamu wetu walikuwa wanausimamisha moyo wakati wanafanya upasuaji lakini katika kambi hii upasuaji unafanyika huku moyo ukiendelea kufanya kazi kama kawaida. Wagonjwa saba wameshafanyiwa upasuaji huu hadi sasa. Kufanyika kwa upasuaji wa aina hii kutawasaidia wagonjwa kupona haraka na kukaa hospitali kwa siku chache.
Aidha upasuaji mwingine unaofanyika katika kambi hii ni kwa watu wenye matatizo ya mshipa mkubwa wa damu wa kifuani (Thoracic and Abdominal Aortic Aneurysm Dissection). Hadi sasa wagonjwa wanne wameshafanyiwa upasuaji wa aina hii.
Tunaamini kambi hii itawasaidia wataalamu wetu kupata ujuzi wa kutosha ambao utawasaidia kufanya upasuaji wa aina hii siku za karibuni.
Changamoto kubwa tunayokutana nayo ni upatikanaji wa damu kwani wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wanahitaji kuongezewa damu nyingi kati ya chupa sita hadi saba. Tunawaomba wananchi muendelee kujitolea kuchangia damu kwa ajili ya wagonjwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kuokoa maisha yao.
Hadi kumalizika kwa kambi hii tarehe 19/04/2021 tunatarajia wagonjwa 20 watakuwa wamefanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo na wagonjwa nane watakuwa wamefanyiwa upasuaji wa mshipa mkubwa wa damu wa kifuani. Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wanaendelea vizuri na wengine wamesharuhusiwa kutoka katika chumba cha uangalizi maalum na kurudi wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu ikiwemo mazoezi.
Comments
Post a Comment