Wagonjwa 22 wamefanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo bila ya kuusimamisha moyo katika kambi maalum ya matibabu ya siku kumi
Wagonjwa
22 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo
wakati moyo ukiwa unafanya kazi katika kambi maalum ya matibabu ya siku kumi
iliyofanywa na madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na Daktari
bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Sinha kutoka hospitali ya
Max iliyopo New Delh nchini India.
Upasuaji
huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 330 ambapo kama wagonjwa hao
wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu hayo gharama za matibabu
zingefikia kiasi cha shilingi milioni 900.
Akizungumza
na waandishi wa habari hivi karibuni kuhusu kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa
JKCI Prof. Mohamed Janabi amesema JKCI imekua ikifanya kambi mbalimbali za
matibabu na wataalam kutoka nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na
kupata mbinu mpya za kitabibu.
“JKCI
tumekua tukifanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo takribani
miaka mitano lakini tofauti kubwa ni kwamba sisi tulikua tunasimamisha moyo
kabisa ndio tunafanya upasuaji na baada ya hapo tunaustua moyo lakini kupitia
ujuzi tulioupata kutoka kwa Daktari kutoka Hospitali ya MAX Subhash Sinha
tumeweza kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo bila kuusimamisha moyo” alisema
Prof. Janabi
“unapofanya
upasuaji wa moyo wa kupandikiza mishipa ya damu wakati moyo unapiga humsaidia
mgonjwa kukaa muda mfupi zaidi hospitali, hatari za upasuaji zinakua chache
zaidi, upasuaji unatumia muda mfupi tofauti na ule wa kuusimamisha moyo lakini
pia mgonjwa hutumia siku 10 hadi 14 kurejea katika hali yake ya kawaida na
kuendelea na shughuli zake” alisema Prof. Janabi
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Upasuji wa Moyo na Mishipa ya Damu wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete Angella Muhozya amesema Kuwa kwa kipindi cha miaka mitano JKCI
imefanya upandikizaji wa mishipa ya damu kwenye moyo kwa wagonjwa zaidi ya 100.
“Utaalamu
huu tulioupata kutoka kwa Dkt. Sinha wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo
bila ya kuusimamisha moyo utatusaidia kuwafanyia upasuaji wagonjwa wengi zaidi
kwa kipindi kifupi tofauti na awali tulipokua tukisimamisha moyo kwani
ilitulazimu kuchukua muda mwingi kufanya upasuji huo” alisema Dkt. Angella
“Baada ya kambi hii sisi kama JKCI tutaendelea
kufanya upasuaji huu kwa wagonjwa wetu bila kusimamisha moyo lengo letu likiwa
ni kuifanya JKCI kuwa kituo cha ubora katika kutoa huduma za matibabu ya afya
ya moyo” alisema Dkt. Angella
Naye
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Sinha kutoka
hospitali ya Max iliyopo New Delh nchini India amewapongeza wataalam wa afya wa
JKCI kwa huduma bora za kitatibu wanazozitoa kwa wagonjwa wao huku akiwataka
wataalam hao kuendelea kujifunza kila wanapopata nafasi ya kujifunza mbinu mpya
za kitabibu.
“Madaktari
wa JKCI wana utayari wa kujifunza na kubadilishana uzoefu nasi, hii nimeiona
nilivyokuwa nafanya nao upasuaji kwa kipindi cha siku hizi 10, naamini JKCI
inaelekea kuwa tegemeo barani Afrika kutokana na huduma bora na nzuri
wanazozitoa” alisema Dkt. Sinha
Comments
Post a Comment