Prof Janabi: Sigara husababisha vifo tatribani milioni nane kwa mwaka duniani

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumzia madhara ya matumizi ya tumbaku na athari zake kwa wagonjwa wa moyo na wagonjwa wa UVIKO -19 wakati wa mkutano wa kutoa tathmini ya jinsi makampuni ya tumbaku yanavyoingilia sera za afya na sera za kudhibiti tumbaku ulioandaliwa na chama cha kudhibiti Tumbaku Tanzania na kufanyika katika Ukumbi wa mikutano JKCI jana jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa kutoa tathimini ya jinsi makampuni ya tumbaku yanavyoingilia sera za afya na sera za kudhibiti tumbaku ulioandaliwa na Chama cha kudhibiti Tumbaku Tanzania uliofanyika jana katika Ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) uliopo jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF) Lutgard Kagaruki akitoa matokeo mbalimbali ya tafiti walizofanya kuhusu makampuni ya tumbaku yanavyoathiri afya na kusababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza wakati wa mkutano wa kutoa tathimini ya jinsi makampuni ya tumbaku yanavyoingilia sera za afya na sera za kudhibiti tumbaku ulioandaliwa na TTCF na kufanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jana jijini Dar es Salaam.

***********************************************************************

Madhara ya moshi wa sigara yanaelezwa husababisha takribani vifo milioni nane Duniani kwa mwaka yakiwahusisha wavutaji wa sigara na watu wengine wanaovuta moshi wake.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati wa mkutano wa kutoa tathimini ya jinsi makampuni ya tumbaku yanavyoingilia sera za afya na sera za kudhibiti tumbaku ulioandaliwa na Chama cha kudhibiti Tumbaku Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam.

Prof. Janabi alisema moshi wa sigara unaathiri viungo mbalimbali vya mwili ikiwemo moyo, ubongo, mapafu na maini hivyo basi ni muhimu elimu sahihi ikatolewa kwa wananchi kuhusu madhara ya matumizi ya tumbaku na kuweza kuepukana nayo.

 “Kampeni ya kuzuia matumizi ya tumbaku kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza inahitajika, kwa tafiti zetu asilimia 25 ya magonjwa ya moyo na asilimia 80 ya saratani za mapafu husababishwa na matumizi ya tumbaku”, alisema Prof. Janabi.

Aidha Prof. Janabi aliwasihi watanzania kuacha kutumia tumbaku kwani ikitokea mtumiaji wa tumbaku akapata ugonjwa wa UVIKO-19 na tayari mapafu yake yalishaanza kuaribika kutokana na matumizi ya tumbaku hujiweka katika hatari kubwa zaidi ya kuathiri moyo.

“Matumizi ya tumbaku huathiri moyo ikiwemo valvu za moyo, kuna wagonjwa wengi ambao tumewafanyia upasuaji mkubwa wa kubadilisha valvu za moyo. Wagonjwa hawa wakieleza historia ya maisha yao wanasema walitumia tumbaku kwa muda mrefu, hata pale walipoambiwa  waache kutumia walibisha na matokeo yake mioyo yao ikaharibika”, alisema Prof. Janabi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF) Lutgard Kagaruki alisema madhumuni ya mkutano huo ni kufanya muendelezo wa tafiti za toka mwaka 2019 hadi sasa ili kutoa taarifa ya uchunguzi ambao umekuwa ukifanyika dunia nzima kuangalia jinsi makampuni ya tumbaku yanavyoingilia sera za afya na sera za kudhibiti tumbaku.

Lutgard alisema TTCF inatoa matokeo ya utafiti wa jinsi makampuni ya tumbaku yanavyoingilia sera za afya ili kuweza kuishauri serikali namna gani wanaweza kudhibiti tumbaku na hivyo kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo tumbaku ndio kisababishi kikubwa.

“Mmesikia tumbaku inavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo, saratani, kisukari, magonjwa sugu ya kifua, mapafu lakini pia uharibifu wa mazingira na umasikini katika familia zetu”,.

“Kwa bahati mbaya sana Tanzania tupo karibu na mwisho katika kudhibiti matumizi ya tumbaku, duniani kati ya nchi 80 Tanzania ni nchi ya 67 katika kudhibiti matumizi ya Tumbaku lakini kwa Afrika kati ya nchi 14 zilizofanyiwa utafiti Tanzania imekua nchi ya 13 katika kudhibiti matumizi ya tumbaku”, alisema Lutgard.

Lutgard aliiomba  serikali kupitisha sheria madhubuti inayoendana na mkataba wa kidunia wa shirika la afya duniani wa kudhibiti matumizi ya tumbaku ili kuokoa kizazi cha sasa na kijacho.

“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanazidi kuongezeka, kama serikali itaongeza kodi ya tumbaku na pombe, matumizi ya vilevi hivyo yatapungua, mapato ya serikali yataongezeka na tutaweza kuokoa kizazi cha sasa na kijacho lakini pia kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza”, alisema Lutgard. 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024