TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI MAFANIKIO YA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWA MIAKA 60 YA UHURU WA TANZANIA BARA.
Ndugu
Wanahabari, Disemba 2021 nchi yetu inaadhimisha miaka 60 ya Uhuru
tangu tarehe 09 Desemba, 1961 tulipoanza kujitawala hivyo, maadhimisho haya ni
tofauti na miaka mingine kutokana na haja ya kutafakari kwa pamoja
tulikotoka, tulipo na tunakoelekea. Maadhimisho haya yanaongozwa na Kaulimbiu isemayo “MIAKA 60 YA UHURU; TANZANIA IMARA, KAZI
IENDELEE”.
Tangu mwaka 1961, Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikitekeleza Sera,
Miongozo na Sheria mbalimbali kulingana na maboresho ya muundo wa wizara kwa
wakati husika. Kufikia mwaka 2016 Wizara mbili ziliunganishwa ambazo ni Afya
na Ustawi wa Jamii pamoja na Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,
hivyo kutengeneza Idara Kuu ya Afya inayoshughulikia masuala yote ya Afya na
Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii inayoshughulikia Masuala yote ya Maendeleo ya
Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto na Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali.
Ndugu Wanahabari, huduma za tiba ya magonjwa pamoja na maendeleo
ya jamii zimekuwepo kwa karne nyingi huku huduma za tiba ya asili zikiitangulia
tiba ya kisasa. Aidha, baada ya karne ya 10 huduma ya tiba za kigeni iliingizwa
na wafanyabiashara wa Kiarabu, Kireno, Kifaransa, n.k. Hata hivyo, Tiba asili
na tiba mbadala pamoja na tiba ya kisasa zimeendelea kutolewa hadi sasa karne
ya ishirini na moja. Aidha, maendeleo
makubwa katika huduma za afya na maendeleo ya jamii yamejitokeza zaidi baada ya
uhuru na katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru ukilinganisha na kipindi cha
takribani miaka 71 ya ukoloni (Utawala wa Wajerumani, 1889 -1916 na Utawala wa
Waingereza, 1916 – 1960).
Napenda kuanza kuangazia huduma za afya kabla
ya Uhuru; kabla ya uhuru makabila
yote 126 yalitumia tiba asili katika kutibu na kujikinga na magonjwa na kwa
mara ya kwanza huduma za tiba za kigeni (Western Medicine) ziliingizwa nchini
mwaka 1887 na kuanza kutolewa mwaka 1889-1916 na wamisionari kipindi cha
utawala wa wajerumani. Vilevile, huduma za kinga hususan Chanjo ya Ugonjwa wa Ndui ilianza kutolewa kwa mara ya kwanza mwaka
1891. Hata hivyo, bado tiba asili
iliendelea kuwepo hata wakati wa Utawala wa Mkoloni (Ujerumani na Uingereza)
huku baadhi ya huduma za tiba asili zikipigwa marufuku na nyingine kuruhusiwa
baada ya kukidhi masharti ya Mkoloni. Aidha,
zile zilizopigwa marufuku ni zile zilizohusishwa na imani za kishirikina au
uchawi. Kutokana na changamoto hizo, mwaka 1928 Sheria ya kwanza ilitungwa
ya kuruhusu uhusishwaji wa tiba asili katika kutoa matibabu na kuwakinga
wananchi.
Ndugu Wanahabari, huduma za afya za kisasa zilizokuwa zinatolewa
wakati huo zilikuwa ni pamoja na Malaria, Chanjo ya Ndui, huduma za afya dhidi
ya Tauni, Malale, Ukoma na Magonjwa ya akili. Hata hivyo, huduma hizo zilikuwa
zikitolewa zaidi kwa Watumishi wa Serikali ya Kijerumani, Wafanyabiashara na
Askari wa Kiafrika huku Vituo vya kutolea huduma hizo za tiba vikijengwa zaidi
katika miji na makazi ya wajerumani na hospitali ya kwanza ikijengwa
Mamboya, Mpwapwa.
Kwa
kifupi, upatikanaji wa huduma za afya za kigeni au kisasa enzi hizo haukuwa na
usawa kwa wote (equity) na huduma zilikuwa chache na mbali na wananchi walio
wengi.
Ndugu Wanahabari, sura hii ya huduma za afya iliendelea hivyo
hata baada ya vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1914 ambapo, nchi ya Tanganyika
ilitawaliwa na Mwingereza kuanzia mwaka 1916-1960. Ni katika kipindi hicho
ambapo, huduma za tiba zilizidi kuendelezwa kwa kiasi kikubwa huko huko maeneo
ya mijini ikilinganishwa na maeneo ya vijijini huku zikitoa kipaumbele kwenye
tiba zaidi kuliko kinga licha ya uwepo wa idara ya tiba na usafi kwa ajili ya afya ya jamii. Kwa upande Mwingine,
watumishi wa afya waliongezeka kwa idadi na aina ya kada zikiwemo madaktari wa kigeni, matibabu (medical
assistants), watoaji dawa (dispensers), wasaidizi maabara (African Laboratory
assistants), wahudumu wa tiba (medical auxiliaries), wafunga vidonda (tribal
dressers), wakaguzi wa usafi (urban sanitary inspectors), wauguzi, n.k
Aidha, juhudi
zingine katika uboreshaji wa huduma za afya zililenga katika upatikanaji wa
maji, huduma za utupaji taka, kuangamiza mazalia ya mbu huku vituo vingi vya
kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na hospitali vikijengwa.
Ndugu Wanahabari, Vita Kuu ya Pili ya Dunia iliyoanza mwaka 1939 ilirudisha
nyuma maendeleo ya huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya zilizokuwa
zinasimamiwa na Wizara ya Afya na Kazi
huku huduma hizo zikitolewa zaidi kwa wageni waliokuja nchini, hususan
watumishi wa utawala wa kikoloni, wafanyabiashara na askari. Kwa hali hii ilikuwa vigumu kwa wananchi walio
vijijini kupata huduma hizo. Aidha,
katika kipindi hicho, kulikuwepo na uchache wa raslimali za kuwezesha
upatikanaji wa huduma za afya hasa watumishi, dawa, vifaa tiba na vituo vya
huduma.
Ndugu Wanahabari, zifuatazo ni baadhi ya takwimu za hali ya
upatikanaji wa raslimali kwa ajili ya huduma za afya kabla ya uhuru;
1.
Idadi ya
hospitali na zahanati kwa pamoja ilikuwa 1,343 zikiwa na jumla ya vitanda
18,832.
2.
Aidha,
hadi kufikia mwaka 1960 kulikuwa na hospitali kubwa 12 tu zikiwa na jumla ya
vitanda 3,046. Kati ya hospitali hizo, Saba (7) zilikuwa zinamilikiwa na
Serikali, Nne (4) Mashirika ya Kidini na Hospitali moja (1) binafsi. Hospitali hizo zilikuwa katika maeneo ya Dar es
Salaam (Jimbo Mashariki), Tanga (Jimbo la Tanga), Moshi (Jimbo la Kaskazini),
Peramiho (Jimbo la Kusini), Mwanza (Jimbo la Ziwa), Tabora (Jimbo la
Magharibi), Morogoro (Jimbo Mashariki), Bumbuli (Jimbo la Tanga), Ifakara
(Jimbo la Mashariki), Dodoma (Jimbo la Kati), Ndanda (Jimbo la Kusini) na Sumve
(Jimbo la Ziwa).
3. Uwiano wa wagonjwa kwa vitanda ulikuwa ni kitanda
1 kwa kila watu 1,000 (1:1000). Ikumbukwe, hadi kufikia mwaka 1956 kulikuwa na
uwiano wa vitanda 0.6 kwa kila watu 1,000 chini ya lengo la kitanda 1 kwa kila
watu 1,000.
4. Uwiano wa vituo vya afya kwa idadi ya watu
ulikuwa kituo cha afya 1 kwa watu 40,000 au 50,000.
5. Aina ya watumishi kwenye vituo hivyo ulikuwa:
a. Mganga Msaidizi mmoja (1),
b. Mkaguzi wa Afya mmoja (1),
c. Wakunga kijijini wawili (2),
d. Wauguzi wawili (2),
e. Mhudumu wa Afya mmoja (1), na
f. Watumishi wa kawaida wawili (2).
6. Watumishi waliofuzu shahada ya udaktari
walikuwa 400 tu huku watanzania wazawa wakiwa chini ya 20.
7. Jumla ya madaktari waliosajiliwa na wenye
leseni na kufanya kazi hadi mwaka 1961 walikuwa 403 tu (182 walikuwa katika vituo binafsi; 140 wakiwa
serikalini; na 81 waliajiriwa na Mashirika ya Afya ya Kujitolea). Aidha, jitihada za
kuongeza watumishi zilifanyika katika kipindi cha miaka 5 ya mwisho katika
kipindi cha ukoloni wa Waingereza.
Ndugu Wanahabari, kwa mara ya kwanza mwaka 1960 zilianzishwa
huduma za kinga kwa njia ya chanjo kwa watoto. Katika kipindi hiki Mashirika ya
Kujitolea yalitoa mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za mama na mtoto huku
mama 1 kati 6 ndiye aliweza kupata huduma za uzazi kutoka kwa mtumishi wa afya
aliyepata mafunzo.
Hadi kufikia Desemba 1961 hali ya utumiaji wa
huduma za Mama na Mtoto ilikuwa kama ifuatavyo;- Jumla ya Kiliniki zilifikia 412 ambazo
zilikuwa chini ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Kujitolea na
ziliweza kutoa huduma za Kiliniki kwa jumla ya wajawazito 177,214.
1. Serikali Kuu ilikuwa ikimiliki Kiliniki 71
ambapo mahudhurio ya kwanza kwa mama wajawazito yalikuwa 48,667,
2. Serikali za Mitaa ilikuwa ikimiliki Kiliniki
204 ambapo mahudhurio ya kwanza ya Mama Wajawazito walikuwa 68,601; na
3. Mashirika ya kujitolea yalikuwa yakimiliki
Kiliniki 137 ambapo akinamama wajawazito 59,946 walihudumiwa.
Ndugu Wanahabari, kipindi hicho (Disemba, 1961)
pia kulikuwa na Kliniki za watoto zipatazo 454 ambapo;
1.
Serikali
Kuu ilimiliki 69 na watoto 29,715 walihudhuria hudhurio la kwanza;
2.
Serikali
za Mitaa ilimiliki Kiliniki 195 na watoto 52,635 walihudhuria hudhurio la
kwanza; na
3.
Mashirika
ya Kujitolea yalimiliki Kiliniki 190 ambapo watoto 54,154 walihudhuria udhurio
la kwanza.
Kwa ujumla wake Kliniki hizi za watoto
ziliweza kutoa huduma za Kiliniki 136,504 tu.
Ndugu Wanahabari, endeshaji wa huduma za Afya Serikali
Kuu ulikuwa katika ngazi tatu ambazo ni
Wizara, Mkoa na Wilaya. Huduma za afya ziliendeshwa chini ya Wizara ya Afya na
Kazi na Kiongozi Mkuu alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali akiwa na wasaidizi wa
aina tatu: Madaktari Waandamizi (Principal Medical Officers) 3; Muuguzi Mkuu
(Principal Matron), na Mkaguzi Mkuu wa Afya (Chief Health Inspector). Huduma
maalumu zilizosimamiwa zilikuwa: Mafunzo (Medical training); Huduma za maabara
na dawa (pathology and pharmaceutical services); Huduma za afya ya akili
(psychiatric services); na Vitengo maalumu: Malaria, Elimu ya Afya na Lishe.
Ndugu Wanahabari, sasa naomba nijielekeze
kwenye hali ya Huduma za Afya baada ya Uhuru wa Desemba 9, 1961; tunapotimiza
miaka 60 tangu kupatikana kwa Uhuru tunashuhudia mabadiliko na mafanikio makubwa
ya maendeleo kwenye huduma za afya ukilinganisha na kabla ya uhuru.
Maendeleo
au mafanikio haya yametokana na msingi mzuri na thabiti uliowekwa na Rais wa
kwanza na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo
alielekeza nguvu za Taifa katika kukabiliana na adui watatu wakubwa, yaani
Ujinga, Umaskini na Maradhi huku viongozi wengine wa taifa hili awamu zote
wakiendelea kupambana kutimiza ndoto hizo. Vilevile, mafanikio
hayo yametokana kazi kubwa ya Serikali za Chama cha Mapinduzi na Ilani zake
nzuri awamu zote sita za uongozi
zilizowezesha kupata Marais mahiri na wenye uthubutu, kuwa na utashi wa kisiasa
kwenye maendeleo nyakati zote, kuunda Serikali zenye uongozi bora na kupata Sera
nzuri za Afya.
Pia,
mafanikio haya yametokana na uboreshwaji wa ushirikiano na mashirika ya dini na
binafsi, wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja wananchi wa taifa hili kwa ujumla
wake.
Kwa
ujumla wake, mazingira haya yamewezesha utekelezaji wa masuala ambayo huko
nyuma yalikuwa yanaoneka kama ndoto.
Ndugu Wanahabari, mafanikio ya miaka 60
baada ya uhuru ni mengi na ni vigumu kuyaeleza
kinagaubaga na kumaliza hivyo nitafupisha kwenye maeneo muhimu kama ifuatavyo;
miaka 60 baada ya uhuru;-
1. Idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya ngazi
zote imeongezeka hadi kufikia vituo 8,537
ikilinganishwa
na vituo 1,343 Mwaka 1960. Ongezeko
hili ni sawa na asilimia 84.26. Aidha, kati ya vituo hivyo, Serikali inamiliki
asilimia 64, Mashirika ya dini asilimia 9 na vituo binafsi asilimia 27.
2. Mtandao wa vituo vya
huduma za afya umepanuka na kusogea karibu zaidi na wananchi ambapo; zahanati ni 7,242; vituo vya afya
926; na Hospitali za Wilaya ni 178, Hospitali zingine ni 151. Aidha, hospitali
za kibingwa ngazi ya mikoa ni (28), ngazi ya Kanda Sita (6), hospitali za
ubingwa maalumu ni Tano (5) na hospitali ya taifa ni moja (MNH).
3. Vituo vyote hivi vina
jumla ya vitanda 90,488 ikiwa ni sawa na ongezeko la vitanda 71,656 sawa na
asilimia 79.18. Kwa sasa uwiano wa vituo kwa idadi ya watu ni kituo kimoja kwa
watu 6,751.5 (1: 6,751.5) tofauti na 1:40000-50000 kabla ya uhuru. Hivyo, Tanzania imefikia malengo ya umoja
wa mataifa katika upatikanaji wa huduma za afya kwa kuzingatia idadi ya watu na
jiografia.
4. Aidha, uwiano wa vitanda kwa idadi ya watu ni
kitanda kimoja kwa watu 637 (1:637) ukilinganisha na 1:1000 kabla ya uhuru. Hadi mwaka 2020 uwiano wa wagonjwa kwa vitanda umekuwa kitanda kimoja kwa watu 19
(1:19).
5. Idadi ya watumishi na wigo wa kada za wataalamu
kwenye vituo vya huduma umepanuka kiasi kwamba hivi sasa vituo vya afya
vinafanya hadi huduma za upasuaji mkubwa ambao awali ulikuwa haufanyiki.
6. Idadi ya wataalamu wa baadhi ya kada mbalimbali
za msingi kwenye afya waliosajiliwa imeongezeka hadi kufikia zaidi takribani 71,365
na usajili unaendelea kila siku. Hawa ni baadhi tu ya kada zinazojumuisha
madaktari bingwa, wa kawaida, wauguzi, wataalamu wa maabara, mionzi, wafamasia
na mionzi. Kabla ya uhuru wote hawa kwa ujumla walikuwa 435 tu. Hii ni hatua
kubwa sana.
7. Hadi kufikia Juni, 2021 huduma za chanjo
zimepanuka na kuimarika na kufanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi
zinazotekeleza kwa ufanisi eneo hili hususan chanjo za watoto chini ya mwaka
mmoja (1) huku utekelezaji ukiwa umefikia asilimia 101. Aidha, kila kituo cha
huduma za afya kina huduma ya chanjo kwa ajili ya Kinga ya ugonjwa wa Polio (OPV3), PENTA-3 kwa ajili ya kuzuia magonjwa
ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda (tetanus), homa ya ini na homa ya uti wa
mgongo na chanjo ya Surua/ rubella.
8. Idadi ya Kliniki za afya ya uzazi imeongezeka
na sera ni kuwa katika kila kituo cha huduma za afya kuwe na huduma za afya ya
uzazi na mtoto.
9. Mifumo ya uongozi na uendeshaji wa vituo vya
huduma za afya imeboreshwa kiasi kwamba wananchi nao ni sehemu ya bodi za
ushauri, uendeshaji na kamati za ushauri na uendeshaji kuanzia hospitali za
kitaifa hadi zahanati. Hii ni pamoja na taasisi zote katika sekta ya afya. Hivyo,
mipango, utekelezaji na tathmini vinafanywa siyo na wataalamu tu bali na
wananchi wenyewe, fedha za mipango ya maendeleo na uendeshaji kwenye sekta ya
afya sasa zinapelekwa moja kwa moja kwenye akaunti za vituo zinazosimamiwa na
wananchi wenyewe (DHFF kwa ajili ya uendeshaji na kwa miradi ya ujenzi kupitia
Force Account). Maendeleo haya ni
makubwa yanahitaji kusimuliwa kwa sauti kubwa na kukumbukwa daima huku
tukijivunia, kuyafurahia na
kuyaenzi.
Ndugu Wanahabari, Hata sasa serikali ya awamu ya sita chini ya
uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, kazi ya kuboresha huduma za afya inaendelea kwa kasi kubwa Kama
mlivyosikia hivi karibuni, juhudi za Mheshimiwa Rais katika kupambana na madhara
ya UVIKO-19 zimewezesha Nchi kupata mkopo wa masharti nafuu wa Dola za
Kimarekani milioni 567.25 sawa na
Shilingi trilioni 1.362 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambapo, tarehe 10/10/2021 wakati akizindua kampeni ya
Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19 alitenga
Shilingi Bilioni 466.781 (34%) kwa ajili ya Sekta ya Afya ziende;
1.
Kuimarisha huduma za
dharura, wagonjwa mahtuti na wanaohitaji uangalizi maalum; itakayogharimu Shilingi
bilioni 254.4.
2.
Kuimarisha huduma za
maabara, mionzi na tiba mtandao; itakayogharimu Shilingi bilioni 111.5
3.
Kuimarisha huduma
za chanjo dhidi ya UVIKO - 19 na elimu ya afya kwa umma dhidi ya kujikinga na
maambukizi ya ugonjwa huo; itakayogharimu Shilingi bilioni 43.2
4. Kuimarisha miundombinu katika vituo vya kutolea huduma za
Afya; itakayogharimu Shilingi
bilioni 41.8
5. Kufanya tafiti za kitaalam kuhusu Virusi vya
Korona pamoja na kuwajenga uwezo watoa huduma za Afya; itakayogharimu Shilingi
bilioni 15.9.
Hii ni
kudhihirisha kuwa, mapambano dhidi ya adui maradhi bado yanaendelea hata kwenye
serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, Rais wa JMT.
Ndugu Wanahabari, mapambano haya miaka kadhaa iliyopita baada ya
uhuru yalipelekea kuzaliwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM-2007-2017)
uliochangia;
1. Kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za afya
nchi nzima;
2. Kupungua kwa vifo vya watoto;
3. Kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa na vifaa
tiba katika vituo vyote;
4. Kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi;
5. Kuongezeka kwa ajira ya wataalam waliopelekwa
katika ngazi zote za vituo vya kutolea huduma katika Halmashauri, Mikoa, Kanda
na Taifa.
Vilevile,
mapambano dhidi ya adui maradhi baada ya uhuru yaliifikisha nchi kwenye kuanzishwa
kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ambapo kama nilivyosema awali hivi
sasa tunazo hospitali 12 za ubingwa daraja la juu zinazotoa huduma ikiwemo;
1. Upasuaji mkubwa wa moyo,
2. Huduma za usafishaji na upandikizaji wa figo,
3. Matibabu ya kisasa ya Saratani,
4. Matibabu ya mifupa na huduma nyinginezo nyingi ambazo zimepunguza rufaa
ya wagonjwa kwenda nje ya nchi na hivyo kuokoa fedha nyingi za kigeni ambazo
zingetumika kuhudumia rufaa hizo.
Ndugu Wanahabari, katika kuendeleza mapambano na adui maradhi, Serikali
ya Awamu ya Sita katika mwaka huu wa 60 pia
imetenga jumla ya Shilingi bil 149 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi kwenye
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya
Nyanda za Juu Kusini (META), Hospitali ya Kanda Chato Awamu ya Kwanza pamoja na
hospitali mpya za Rufaa za Mikoa ya Njombe, Simiyu, Geita, Songwe, Katavi na
Sekou Toure, Mwanza. Vilevile, Manyara, na Mara – Hospitali ya Kumbukizi ya
Mwalimu Nyerere (Kwangwa), Kazi inaendelea.
Ndugu Wanahabari, ukiacha maendeleo ya miundombinu baada ya
Uhuru, vilevile, maendeleo makubwa yamepatikana kwenye vifaa tiba vya kisasa na
wataalamu bobezi wa tiba ambao, wamefanya kazi nzuri
iliyopunguza rufaa za nje ambapo katika kipindi cha Julai, 2020
hadi Juni 2021, ni wagonjwa 2 tu
walipatiwa rufaa nje ya nchi, ukilinganisha na wagonjwa 554 waliopatiwa rufaa nje ya nchi mwaka 2015/16.
Haya ni mapinduzi
makubwa kwa kipindi cha miaka 60 tangu tupate uhuru.
Zifuatazo
ni baadhi ya alama za mapinduzi haya kwenye baadhi ya hospitali za ubingwa
bobezi nchini Tanzania kama ifuatavyo kwa ufupi;
Hospitali ya Taifa
Muhimbili huduma mpya zimeanzishwa zikiwemo;
1. Kusafisha damu kwa
wagonjwa wenye matatizo ya figo (Dialysis) ambazo pia zimeenea hospitali
mbalimbali nchini hadi hospitali za rufaa za mikoa;
2. Kuanza upandikizaji
Figo (Renal Transplant) ambapo hadi sasa wananchi 64 wamenufaika na huduma hiyo
pia huduma hii inapatikana katika hospitali zingine kama BMH na zingine ziko
mbioni kuanza;
3. Upandikiza vifaa vya
kusaidia watoto kusikia (Cochlear Implant) kupitia Hospitali za umma katika
ukanda wa Afrika Mashariki na zaidi ya watoto 32 na watu wazima wawili
wamenufaika na huduma hizi; na
4. Tiba Radiolojia
(Interventional Radiology) ambapo kwa miaka mingi wagonjwa waliokuwa na uvimbe
kwenye kinywa na mataya walianza kufanyiwa upasuaji hapa nchini.
Hospitali ya Saratani Ocean
Road (ORCI);
1.
Sasa
tunazo mashine za kisasa za teknolojia ya 3D za tiba mionzi za LINAC na CT
simulator zilizogharimu Tsh 9.5 Bilioni zinazotibu saratani kwa sayansi ya
kisasa na sahihi zaidi.
2.
Serikali Imetoa jumla ya Tsh 14.5 Bilion za Mradi wa
Jengo, na Mashine za Cyclotron na PET CT scan ili kuimarisha vipimo vya
ugunduzi na uchunguzi wa saratani ambapo kwa sasa havifanyiki nchini wala
Ukanda wa Africa mashariki na Kati.
Aidha, kuimarishwa kwa utoaji wa huduma
hasa tiba mionzi, kumeendelea kuwavutia wagonjwa kutoka nje ya nchi kuja nchini
kwa ajili ya tiba. Katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Juni, 2021 jumla ya
wagonjwa wapya 55 kutoka nje ya nchi walipatiwa huduma za uchunguzi na tiba ya
saratani. Maboresho yote haya yamepunguza rufaa za wagonjwa wa saratani nje ya
nchi kwa asilimia 90% na Serikali imeokoa takribani Tshs 10 bilioni ambazo
zingetumika kwa matibabu nje ya nchi.
Hospitali ya tiba ya
mifupa, ubongo na mishipa ya fahamo (MOI); hivi karibuni serikali imenunua na kufunga
mashine ya kupasua ubongo bila kufungua kichwa (Angio Suite iliyogharimu bilioni 7.9). Ikumbukwe, kufikia
Januari 2021 mashine hii ilipofungwa hakukuwa na kama hii Afrika Mashariki bali
ilikuwepo Afrika Kusini. Kufikia leo
imeshawafanyiwa operesheni ya ubongo wagonjwa 68 bila kufungua kichwa.
Hospitali ya tiba ya
moyo (JKCI); huduma
nyingi mpya za kisasa za matibabu ya moyo zimeendelewa kutolewa na pia upo mtambo wa kisasa wa Cathlab na Carto
3 wa uchunguzi na kutibu magonjwa ya moyo wenye thamani ya Shilingi bilioni 4.6 ambapo, wagonjwa 6,513 wameshafanyiwa upasuaji wa moyo
kupitia tundu dogo na 2,436 wametibiwa matatizo ya mishipa ya damu.
Hospitali ya Rufaa
Kanda ya Ziwa (Bugando); huduma mbalimbali mpya za kibingwa zimeendelea
kutolewa na zaidi;
1.
Hospitali imenunua mashine ya tiba ya mionzi inayoitwa
brachytherapy, mtambo wa kusafisha damu (renal dialysis), CT-Scan na mtambo wa
kuzalisha maji tiba.
2.
Umefanyika ununuzi wa MRI yenye Thamani bilioni 2.43
(Euro 900,000) katika Hospitali hii vilevile, imeanzisha huduma za upasuaji kwa Watoto wachanga waliozaliwa na ulemavu
(Congenital Malformations).
Hospitali ya Rufaa
Kanda ya Kaskazini (KCMC).
1. Imewezeshwa kwa mashine
za kisasa za uchunguzi wa magonjwa ikiwa ni pamoja na MRI, CT-Scan yenye ukubwa
wa Slice 128.
2. Serikali inatekeleza
mradi wa bilioni 4 wa ujenzi wa idara ya matibabu ya saratani kwa mionzi.
Hospitali ya Kanda ya Kati ya (BMH) Dodoma;Pamoja kuanza huduma
mwaka 2017, imekua kwa kasi na kuanza kutoa huduma za ubingwa bobezi mathalani;
1. Imeshapandikiza figo
wagonjwa 23 na kati ya hao 16 wamepandikizwa na madaktari wazawa.
2. Inatoa matibabu ya
magoti kwa kutumia matundu madogo kwa watu wenye matatizo ya miguu,
3. Inazo huduma za kuondoa
mawe kwenye figo kwa kutumia vifaa maalumu bila kulazimika kufanya upasuaji kwa
mgonjwa;
4. Imeweza kutoa huduma
ya kupandikiza Betri kwenye moyo kwa watu wazima wawili (2).
Hospitali ya Rufaa Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini (Mbeya).
Hii ilifunguliwa
mwaka 1985 na Mtoto wa Malkia wa Uingereza (Prince Anne) na kufikia miaka 60
baada ya uhuru imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo;-
1. Kutoa huduma za
kibingwa kama upasuaji wa kawaida na upasuaji kwa njia ya vitundu “Laparascopic
Surgery” pamoja na usafishaji wa figo (haemodialysis).
2. Kumiliki maabara ya
kisasa iliyopewa Ithibati “Accredation” yenye uwezo wa kufanya vipimo vya ngazi
ya kimataifa pia ina uwezo wa kupima magonjwa ya Ebola na mengine yanayofanana
na hayo.
3. Kuanzisha huduma ya
Mkalimani wa Viziwi jambo ambalo limepelekea mafanikio kwa Taasisi na Jamii kwa
ujumla. Imeweza kutoa huduma ya upasuaji mkubwa kwa viziwi sita (6) na kutoa
huduma ya elimu ya uzazi wa mpango na kuepusha mimba zisizo tarajiwa kwa watu wenye
matatizo ya kusikia.
4. Imeboresha miundombinu
kwa kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa MAJI TIBA (Infusion).
Aidha, hospitali zote hizi pia zinatumia mifumo ya
kisasa ya kidigitali katika kuhudumia wateja na kuweka kumbukumbu zao pia
kudhibiti mapato na matumizi ya taasisi hivyo, kwa kiasi kikubwa zimepunguza
utegemezi kwa serikali lakini pia zimeboresha huduma kwa mteja ukilinganisha na
miaka kdhaa nyuma.
Hospitali ya Afya ya
Akili Mirembe (Dodoma).
Kabla ya Uhuru huduma za Afya
ya Akili zilikuwa duni sana ikilinganishwa na hivi sasa. Aidha, idadi ya
Wataalam wauguzi “Mental Nurses” katika eneo la Afya ya akili walikuwa 12.
Wagonjwa kutoka sehemu mikoa yote ya Tanganyika walikuwa wakipelekwa Hospitali ya
Mirembe na Isanga (Broadmoor).
Wagonjwa walisongamana sana
katika hospitali hiyo na wengi walitibiwa mbali na ndugu zao bila mawasiliano
na nyumbani kwao.
Baada ya Uhuru Serikali
imefanikiwa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo.
1. Kuanzisha kozi za “certificate na diploma in psychiatric nursing”
katika hospitali ya Mirembe mwaka 1973 – 1980s. Katika miaka hiyo ya 1980
ikaanzishwa kozi ya AMO Psychiatry.
2. Kuanzishwa kwa masomo ya udaktari na udaktari bingwa wa magonjwa
ya akili katika Chuo cha Sayansi ya Tiba Muhimbili ambapo hadi sasa tuna
madaktari bingwa zaidi ya 40.
3. Kuanzishwa kwa Sheria ya
Afya ya Akili ya mwaka 2008 “The Mental Health Act, 2008. Act No 21,
2008”. Sheria hii ina madhumuni ya kuratibu na kusaidia Wagonjwa wa afya ya
akili nchini na kuweka huduma za kinga dhidi ya magonjwa ya akili, na
kushirikisha jamii katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa akili.
4. Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Ulimwenguni
ilanzisha mpango wa Huduma ya Afya ya Akili Ngazi ya Msingi. Mradi huo ulifanywa
kwa majaribio mikoa ya Kilimanjaro na Morogoro na ukawa wa mafanikio makubwa.
5. Kati ya 1980 hadi 1990, mikoa ilieendelea kuhimizwa kuanzisha wodi
za wagonjwa wa akili pamoja na vijiji vya utengemao.
6. Vitengo vya wagonjwa wa akili vilianzishwa katika mikoa ya Dar es
Salaam, Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Tabora, Mwanza, Kigoma,
Kagera na Kilimanjaro ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Mirembe.
7. Mikoa yote Tanzania bara sasa ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa wa
akili katika wilaya zao, hadi ngazi ya zahanati. Mafunzo ya kueneza stadi za
kuwahudumia wagonjwa ngazi ya msingi zinapatikana katika vituo vya afya na
zahanati.
8. Kuanzishwa tiba ya saikolojia ambayo inasaidia wagonjwa
wanaoendelea na tiba za kibaolojia waendelee kuimarika na kurudi kataka kazi
zao za kijamii.
Hospitali ya Udhibiti
wa Maambuki Kibong’oto (Kilimanjaro).
Hospitali hii ilianzishwa
mwaka 1926 kwa lengo la kukinga na kudhibiti kifua kikuu na magonjwa ambukizi.
Aidha, mwaka 1952 ilibadilishwa rasmi kuwa hospitali ya TB na Lady Twining –
Mke wa Gavana wa Tanganyika. Mafanikio yaliyopatikana ni kama ifuatavyo;-
1. Kabla
ya uhuru ilikuwa na wodi 3 zenye uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa sasa
hospitali ina wodi 7 zenye vitanda 300 vya kulaza wagonjwa, ambapo vitanda 120
ni kwa ajili ya wagonjwa wa TB sugu, vitanda 120 wagonjwa wa TB ya kawaida na
vitanda 60 kwa wagonjwa wengine
2. Hospitali
iligatua matibabu ya kifua kikuu sugu toka hospitali 1 ya kibongoto 2009 hadi
kufikia vituo 179 nchini
3. Serikali
imenunua mashine maalumu ya kisasa (Migit) yenye uwezo wa kupima usugu wa dawa
za kifua kikuu na kuotesha vimelea vya kifua kikuu cha kawaida na kifua kikuu
sugu ndani ya muda mfupi (wiki 3 hadi 4) badala wiki nane mpaka 10 kwa kutumia
njia ya kawaida ilivyokuwa kabla uhuru.
4. Uboreshwaji
wa huduma za uchunguzi wa vinasaba (whole genomic sequencing) na kuweza
kubainisha anuai ya virusi vinavyosababisa corona nchini ambako kabla ya uhuru
huduma hii haikuwepo
5.
Pamoja na huduma hizi katika hospitali,
inatoa huduma za kijamii kwa njia ya
mkoba kwa kutumia gari maalumu la kisasa lenye kiliniki tembezi.
6. Serikali
inaendelea na ujenzi wa maabara kubwa ya kisasa ya afya ya jamii yenye hadhi ya
Biosafety level 3 ambayo
inagharimu jumla ya shilingi 11,337,672,870.88.
Ndugu Wanahabari, katika kuzingatia upatikanaji wa huduma za
kibingwa karibu zaidi na wananchi na kwa uwiano wa kijiografia nchini tofauti
na kabla ya uhuru au miaka kadhaa iliyopita, Serikali inajenga zingine mpya
ikiwemo Hospitali ya Kanda ya Chato na Hospitali ya Kanda ya Kusini Mtwara.
Aidha,
inapanua miundombinu kwenye Hospitali kongwe za Mikoa, Kanda, Maalumu na Taifa
kama ifuatavyo;
1.
Mbeya; ujenzi
wa jengo la ghorofa Sita (6) la afya ya uzazi na mtoto Mbeya (META).
2.
KCMC; Ujenzi wa wodi ya wagonjwa wa saratani,
upanuzi
wa Idara ya kusafisha damu na figo (Hemodialysis) na kitengo cha Endoscopy
3.
Kibong’oto; Ujenzi wa Maabara ya
Afya ya Jamii ngazi ya tatu (BSL3). Jengo la Maabara husika lina ghorofa tatu
(Ground + 3 floors)
4. Mawenzi; jengo la afya
ya uzazi na mtoto pia jengo la huduma za dharura.
Ndugu Wanahabari, katika kipindi hiki cha baada ya uhuru ukiacha
ujenzi wa hospitali mpya za mikoa nilizotaja awali za Njombe, Songwe,
Simiyu, Geita, Manyara, Songwe na Mara – Kwangwa na upanuzi wa hospitali kongwe za rufaa za mikoa, maendeleo mbalimbali
yanafanyika ikiwemo;
1. Usimikaji wa mitambo
ya kuzalisha hewa tiba kwa thamani ya shilingi bilioni 8.7 unaendelea katika
Hospitali za Rufaa za Mikoa Saba (7) ambayo ni Geita, Manyara, Dodoma, Dar es
Salaam-Amana, Mtwara, Ruvuma-Songea na Mbeya.
2. Ufungaji CT scan,
Ultra Sound na vifaa vya mama na mtoto, upasuaji, utakasaji, incinerator umefanyika
katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekoutoure kwa thamani ya Shilingi.
2,228,448,375.00.
3. Ununuzi na usimikaji
wa CT Scan yenye thamani ya shilingi bilioni 1,444,500,000 umefanyika katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa (Mwananyamala RRH).
4. Ununuzi na sambazaji
wa vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni
6 vya Mradi wa ORIO (Fluoroscopy, Digital X-ray, ultrasound, incinerator
n.k) unaendelea kwenye hospitali tisa (9) hapa nchini; (Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa Temeke, Kitete - Tabora, Shinyanga, Kigoma (Maweni), Bukoba - Kagera, Mara,
Hospitali ya Wilaya Bukombe, Chato na Misungwi).
5. Ununuzi wa mashine za
kidigitali za X-ray katika hospitali zote 28 za rufaa za mikoa kupitia mradi wa
ORIO unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Uholanzi.
6. Umefanyika ununuzi wa
mashine za kisasa “GeneXpert” 239 za kupima Kifua kikuu zinazotoa majibu ndani
ya masaa mawili ikilinganishwa na hadubini zinazotoa majibu baada ya masaa 24.
7. Baadhi ya miundombinu
inayopanuliwa iweze kutoa huduma bora zadi kwenye hospitali hizi za mikoa ni
pamoja na;
i.
Ujenzi
wa jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala lenye
ghorofa nne na pia Mawenzi Kilimanjaro.
ii.
Ujenzi wa jengo la kutolea huduma za
dharura (EMD katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.
iii.
Ujenzi wa jengo la Methadone lenye ghorofa tatu katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tanga.
iv.
Ujenzi wa jengo la huduma za upasuaji katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa Kigoma – Maweni.
v.
Ujenzi wa jengo la huduma za dharura
(EMD) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Iringa
vi.
Ujenzi
wa jengo la huduma za dharura katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora – Kitete
vii.
Ujenzi wa Jengo la Wodi ya
wagonjwa walio chini ya uangalizi maalum, Wodi ya Upasuaji, jengo la huduma
ya Upasuaji na utakasaji vifaa tiba pamoja na ununuzi wa vifaa kwa ajili ya
majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya
Ndugu Wanahabari, Serikali haikuzisahau hospitali za ngazi ya halmashauri,
vituo vya afya na zahanati ambapo, baada ya uhuru kupitia MMAM ilitoa msukumo
mkubwa kwa ufupi kama ifuatavyo;
1. Ukilinganisha
na kabla ya huru, hivi sasa kuna jumla ya Zahanati 7,242 Vituo vya Afya 926 na
Hospitali za Halmashauri 178. Jumla ya Vituo vya Afya 487 kati ya vilivyopo
vinafanya upasuaji wa dharura kwa maana hiyo, watumishi wa kada mbalimbali
muhimu wanapatikana hadi ngazi ya vituo vya afya tofauti na kabla ya uhuru.
2. Huduma
za uchunguzi wa maabara na mionzi nazo zimeimarika. Umefanyika ununuzi wa Xray za kidigitali (Digital X-ray 18) kwa gharama ya
Shilingi za kitanzania 5,290,000,000.00 sawa na shilingi 264,500,000.00 kila
moja na kusambazwa hospitali 14 za halmashauri; (Mangaka, Tunduru, Mbinga, Kasulu, Nyamagana, Butiama, Makambako,
Makete, Mbarari, Tukuyu, Itumba, Nkasi, Usangi, na Same) na hospitali 4 za
Wilaya (Kisarawe, Songwe/ Mwambani,
Namtumbo, na Musoma/ Mwl.Nyerere memorial Hospital). Ununuzi huu
umefadhiliwa wadau wa maendeleo Global Fund.
3. Huduma za uchunguzi
kupitia Ultra Sound zimeanza kutolewa kwenye vituo vya afya 125 katika Halmashauri
mbalimbali nchini.
4. Vipimo mbalimbali vya
maabara vinafanyika ngazi zote za vituo vya afya ya msingi.
Ndugu Wanahabari, katika miaka sitini (60) ya Uhuru Serikali
inaratibu uendeshaji wa huduma za afya kidigitali kupitia mkakati wa TEHAMA
(Digital Health Strategy 2019-2024) ambapo mpaka sasa;
1. Imepeleka Mkongo wa Taifa wa
mawasiliano (fiber optic cable) na kujenga miudombinu ya mtandao (Loca Area
Network) kwenye hospitali zote za rufaa kuanzia ngazi ya Taifa, Kanda, Mkoa na
hospitali maalumu (specialized hospital).
2. Imeboresha upatikanaji wa mtandao wa
uhakika katika vituo vya ngazi ya msingi.
3. Imesambaza vifaa vya TEHAMA kama
Kompyuta, “Server “, printer na vishikwambi katika vituo vya kutolea huduma za
afya ili kurahisiha matumizi ya mifumo ya kieletroniki katika kutolea
huduma na kukusanya taarifa.
4. Kwa mifumo hii, udhibiti wa
raslimali fedha na bidhaa za afya na uwajibikaji pamoja na upatikanaji wa
taarifa kwa wakati unaendelea kuimarika ulikinganisha na miaka kadhaa
iliyopita.
Ndugu Wanahabari, katika kuimarisha huduma za afya baada ya uhuru
serikali imefungua taasisi mbalimbali
saidizi kama ifuatavyo;
I.
Taasisi ya Mfuko wa taifa wa Bima ya Afya; Kabla
ya uhuru huduma za matibabu zilikuwa bila malipo hadi kufikia miaka ya 1997
zilipoanza kutolewa kwa sera ya uchangiaji na msamaha kwa wasio na uwezo. Hata
hivyo, mfumo huu ulibainika kupitwa na wakati hivyo serikali kuanzisha bima za
afya ili kuwawezesha wananchi wananchi
kumudu gharama za matibabu. Hivi sasa, Serikali inayo Bima ya
Afya ya Taifa (NHIF) na Bima ya Afya ya Jamii (CHF). Aidha, zipo na Bima
mbalimbali za binafsi.
Kupitia mifuko hii ya
bima za afya;
1. Hifadhi ya jamii
imeimarika ambapo jumla ya watanzania 8,224,271 sawa na asilimia 14.7 ya
watanzania wote wananufaika na huduma za mifuko ya bima ya afya. Kati ya
wananchi waliojiunga na mfumo wa bima ya afya, asilimia 8 wamesajiliwa na NHIF,
asilimia 5.4 wanahudumiwa na iCHF, asilimia 0.3 wananufaika na huduma kupita
SHIB-NSSF na asilimia 1 wamejiunga na
bima ya afya inayotolewa na makampuni ya bima binafsi za afya.
2. Hadi kufikia Juni 2021
jumla ya vituo 8,482 vya ngazi ya Zahanati hadi Taifa, vya Serikali, Mashirika
ya Dini na Binafsi vinahuhumia wanachama wa NHIF ikilinganishwa na vituo 3,197
vya mwaka 2001/02. Mwanachama wa NHIF kwa kutumia kadi yake anatibiwa popote
Tanzania Bara na Zanzibar katika vituo hivi vilivyosajiliwa. Hivyo, Kadi ya
NHIF haina mipaka ya kimikoa.
Ndugu Wanahabari, Hivi sasa Mfuko
umeweka utaratibu rahisi kwa kila kundi kuchangia, kujiunga na kuanza kunufaika
kwa hiari ikilinganisha na kundi la watumishi wa umma tu ambalo liliwezeshwa
kujiunga wakati Mfuko unaanzishwa.
Wanachama wa mfuko wa
taifa wa bima ya afya wanapata manufaa mbalimbali ikiwemo;
1.
Kupata huduma kuanzia za afya ya msingi hadi za
kibingwa ikiwemo matibabu ya moyo, figo, saratani, upandikizaji wa viungo,
vipimo vikubwa kama CT Scan na MRI. Awali huduma kwa wanachama zilikuwa chache
mathalan idadi ya vipimo ilikuwa 9 na dawa 440 wakati mfuko unaazishwa mwaka
2001.
2. Sasa hivi kitita cha
huduma kina jumla ya dawa 975 zikiwemo za magonjwa ya Sukari, Moyo na Saratani
na vipimo 354 vikiwemo vikubwa na vidogo kulingana na maendeleo ya teknolojia
ya tiba. Huduma za upasuaji mkubwa 210 na mdogo 167 na wa kibingwa 148. Aidha
huduma za kulazwa, kujifungua, macho, meno, n.k zinatolewa kwa wanachama wa
NHIF kulingana na miongozo ya tiba iliyopo.
3. Kulingana na mahitaji
ya wanachama waajiri, Mfuko umeweka utaratibu unaowezesha waajiri kulipia
watumishi wao huduma za ziada (Suplimentary package) ambazo hazipo kwenye
kitita cha mafao cha NHIF. Mathalani, Huduma za Uokozi (Air and ground
evacuation), dawa za majina ya kibiashara, huduma za miwani, n.k
Ndugu Wanahabari, kwa kutambua kuwa
wananchi wengi (takriban asilimia 85.3) wako nje ya mfumo wa bima ya afya,
Serikali inaendelea kukamilisha muswada wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote na
imefikia hatua kubwa. Huu ni mwelekeo mzuri wa nchi katika kipindi cha miaka 60
ya uhuru.
II.
Taasisi ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD);
Ndugu Wanahabari, Ili kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba
na vitendanishi, baada ya uhuru serikali ilianzisha taasisi ya MSD ambayo
imeendelea kuboresha utekelezaji wake kwenye mambo makubwa kama ifutavyo;
1. Kuagiza dawa moja kwa
moja kutoka kwa wazalishaji; hatua hii imewezesha kupata bidhaa hizo kwa
gharama nafuu ambapo hadi sasa upatikanaji wa bidhaa za afya umeimarika kwa
asilimia 55.
2. Kuingia mikataba na
watengenezaji wa vifaa vya maabara na vitendanishi vyake, na mashine za kuchuja
damu. Hatua hii imepunguza gharama za bidhaa hizo kwa asilimia 50 -100 na hatua
hii inatarajiwa kuokoa shilingi bilioni 9.7 kwa mwaka.
3. Ujenzi wa kiwanda cha
barakoa ambapo bei ya barakoa moja imeshuka kutoka kuuzwa shilingi 1,600 hadi kuuzwa
shilingi 600 na kuokoa shilingi milioni 683,980,500 ambazo zingetumika kwa
kuagiza kutoka nje ya nchi;
4. Kuanza uzalishaji wa
bidhaa za afya ikiwa ni pamoja na Kiwanda cha Keko Pharmaceutical Limited
(ambacho MSD imepewa jukumu la kukisimamia), Kiwanda cha Keko Pharmaceutical
kina uwezo wa kuzalisha aina 10 za vidonge ambavyo kati ya hivyo, aina mbili ni
vya maumivu na nane ni vya kuua vimelea vya magonjwa, yaani Antibiotics na moja
ya kutibu fangasi.
5. Kujenga viwanda vinne
vya uzalishaji dawa na vifaa tiba huko Idofi Makambako. Kiwanda cha mipira ya
mikono, Vidonge, vidonge vya rangi mbili na dawa za majimaji (syrup) ambapo
vitaipinguzia gharama Serikali kwa kuokoa kiasi cha shilingi Bilioni 33 kwa
mwaka.
6. Serikali imeongeza
bajeti ya fedha za kununulia dawa hadi kufikia shilingi Bilioni 277.49 mwaka
huu.
III.
Taasisi
ya Udhibiti wa Dawa na Vifaa tiba (TMDA); taasisi
hii imepata mafanikio makubwa yakiwemo;
1.
Hadi
kufikia Juni, 2021, Mamlaka ilikuwa imesajili jumla ya viwanda vya ndani 36,
ambapo 11 vya dawa, viwanda 14 vya vifaa tiba na 11 vya gesi tiba vinavyofanya
kazi ukilinganisha na kiwanda kimoja cha dawa kilichokuwa kimesajiliwa wakati
wa Uhuru mwaka 1961.
2.
Idadi ya bidhaa
za dawa, zilizosajiliwa hadi kufikia mwaka 2020/21 ni 16,467 ikilinganishwa na
265 zilizosajiliwa mwaka 2003/04 ikiwa ni ongezeko 6,214%.
3.
Idadi ya majengo yaliyosajiliwa ya biashara za bidhaa
za dawa zinazodhibitiwa na Mamlaka hadi mwaka 2020/21 ni 11,156 ikilinganishwa
na majengo 1,504 yaliyosajiliwa mwaka 2007/2008 sawa na ongezeko la 742%.
IV.
Taasisi ya Mkemia Mkuu
wa Serikali (GCLA); taasisi hii inahusika na kufanya uchunguzi wa kimaabara juu
ya masuala mbalimbali ya kisayansi. Taasisi hii imeendelea kuimarika kutoka
utumiaji wa mbinu duni za makaratasi ya uchunguzi hadi mbinu zinazotumia mitambo
na vifaa vya kisasa. Mitambo hii imeifanya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali
kuwa ya pili katika maabara zenye vifaa vya kisasa katika nchi za Afrika
Mashariki, Kati, Kusini mwa Afrika ikitanguliwa na maabara chache za Afrika
Kusini.
V.
Taasisi ya Utafiti Afya
(NIMR); taasisi hii inahusika na Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu ambapo imeweza kufanya
tafiti katika maeneo mbalimbali hapa nchini kuhusu Malaria, kifua kikuu
(TB), UKIMWI, afya ya mama na mtoto, magonjwa ya kitropiki yaliyokuwa hayapewi
kipaumbele, magonjwa ya mlipuko, magonjwa yasiyoambukiza, muungano wa magonjwa
ya kuambukiza na yasiyoambukiza (co-morbidities), viashiria vya afya vya kijamii
pamoja na, magonjwa mtambuka ya binadamu na wanyama (One Health). Pia Taasisi
imeendelea kutekeleza miradi ya utafiti inayolenga kuimarisha mifumo ya afya na
tafiti hizo zililenga katika kutafiti na kusaidia kutatua changamoto ya
upatikanaji wa dawa hata pale ambapo madawa katika bohari ya dawa yanapatikana.
VI.
Taasisi ya Chakula na
Lishe (TFNC); Taasisi hii inahusika na
kuishauri serikali, wananchi pamoja na wadau wote wa lishe nchini namna ya
kupambana na aina zote za utapiamlo.
Katika
miaka 60 ya Uhuru, TFNC kwa kushirikiana na sekta nyingine imechangia
kutekeleza afua ambazo zimepelekea kupunguza viwango vya utapiamlo kwa kiasi
kikubwa kama ifuatavyo;-
1.
Udumavu kwa Watoto chini ya
miaka mitano kutoka zaidi ya asilimia 50 kabla ya uhuru kufikia asilimia 31.7
mwaka 2018;
2.
Ukondefu kwa watoto chini ya
miaka mitano umepungua kutoka asilimia 6 mwaka 1992 hadi kufikia asilimia 3.5
mwaka 2018;
3.
Uzito pungufu kwa watoto chini
ya miaka mitano kutoka asilimia 29 mwaka 1992 hadi kufikia asilimia 14 mwaka
2018:
4.
Upungufu wa damu kwa wanawake
walio katika umri wa kuzaa (miaka 15-49) kutoka asilimia zaidi ya 50 hadi
kufikia asilimia 28 mwaka 2018.
5.
Pia Taasisi imewezesha
kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa watoto wenye umri chini ya
miezi sita kutoka asilimia 24 hadi kutikia asilimia 59 mwaka 2018.
Ndugu Wanahabari, zifuatazo
ni takwimu chache za utumiaji wa vituo vya kutolea huduma kwa rejea ya Huduma
za Afya ya Uzazi (Mama) na Mtoto;-
1.
Ongezeko la wajawazito
waliohudhuria mahudhurio manne au zaidi ya kiliniki hadi kufikia mwezi Machi
mwaka 2021, asilimia 93.4 ya wajawazito walihudhuria kliniki.
2.
Ongezeko la akinamama
kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya limefikia hadi asilimia
83.1 mwaka 2020 ambayo ni zaidi ya lengo la Mpango Mkakati wa Nne wa Sekta ya
Afya (HSSP IV) la asilimia 65.
3.
Idadi ya akinamama waliojifungua
na kurudi kiliniki siku mbili baada ya kujifungua imefikia asilimia 62.
Mwitikio huu ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa mama na mtoto, kwa kuwa
asilimia 60 ya vifo vitokanavyo na uzazi hutokea kipindi cha baada ya
kujifungua kutokana na matatizo ya kupoteza damu, kifafa cha mimba na
maambukizi ya bakteria.
4.
Hadi kufikia Machi 2021, jumla
ya akina mama 332,620 walifanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa
kizazi kwenye vituo 794 vya uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi.
Baadhi ya vashiria vingine vya
mafanikio ni pamoja na;
1.
Chanjo kwa watoto vhini ya miaka
mitano imeendelea kutolewa kwa wastani wa 95% kwa miaka mitano mfululizo kutoka
mwaka 2015.
2.
Ugonjwa wa Polio (Acute Flaccid
Paralysis) (kupooza ghalfa kwa watoto) tumefanikiwa kuumaliza kwa chanjo na
hivyo Tanzania kutangazwa kuwa huru dhidi ya ugonjwa huu toka mwaka 2015 na
kupewa cheti cha kuwa huru miaka mitano baadae yaani mwaka 2020.
3.
Vifo vya watoto chini ya miaka
mitano vimepungua kutoka 112 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2004/05 hadi vifo 50
kila vizazi hai 1000 mwaka 2020. Tukumbuke mwaka 2013 Tanzania ilikuwa miongoni
mwa nchi ambazo zilifanikiwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano
kufikia malengo ya milenia ya nne (MDG 4).
4.
Vifo vya watoto chini ya mwaka
mmoja (Infant Mortality) vimepungua kutoka 94 kwa vizazi hai 1000 mwaka 1992
hadi vifo 36 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2020 (DHS projection 2020).
5.
Vifo
vya watoto wachanga ndani ya siku 28 (neonatal
mortality) vimepungua kutoka vifo 32 kwa kila vizazi hai 1000 (2004/05) hadi
vifo 20 kwa kila vizazi 1000 (2020).
6.
Vifo vya wajawazito vimepungua kutoka vifo 870 kwa kila vizazi
100,000 (1990) kufikia vifo 321 kwa kila vizazi hai 100,000 (2020).
7.
Kuenea
kwa malaria (prevalence) kumepungua kwa 50% kati ya miaka ya 90s hadi kufikia
7.5% mwaka 2017 (MIS - 2017). Vilevile, idadi ya wanaofariki kwa malaria
imepungua kwa 61% kutoka vifo 6,311 mwaka 2015 hadi vifo 2,460 mwaka 2020.
8.
Hali ya ugonjwa wa Ukoma imepungua kutoka wagonjwa 1889 (2015)
mpaka wagonjwa 1217 kwa mwaka 2020.
9.
Hali ya matibabu ya Kifua Kikuu nchini inazidi kuimarika ambapo
tumeongeza uibuaji wa wagonjwa kutoka 62,180 (2015) mpaka 85,597 (2020). Aidha
vifo vimepungua kutoka 55,000 (2015) mpaka 26,800 (2020). Hii inatokana na
uwepo wa njia zilizoboreshwa za uchunguzi na elimu kwa jamii na Serikali
kupeleka huduma za uchunguzi na tiba mpaka kwenye ngazi ya jamii.
Mafanikio haya pia
yanajieleza kwa kuongezeka kwa umri wa kuishi wa mtanzania toka miaka 36 mwaka
1961 hadi miaka 66 mwaka 2020 ambayo inaashiria kuimarika kwa mifumo ya utoaji
huduma za afya nchini. Hili ni ongezeko la mara mbili kwenye umri wa kuishi
mtanzania.
Ndugu Wanahabari, katika kipindi hiki cha baada ya uhuru serikali
imejiendeleza na kujiimarisha zaidi katika kukabiliana na magonjwa
yanayozuilika (kinga) yakiwemo yanayoambukiza na yasiyoambukiza. Kwa upande wa
mgonjwa yanayoambukiza mifumo ya kubaini, kuzuia na kudhibiti imeimarika hadi
sehemu za mipakani ambapo sasa tuna vituo 40. Maabara kuu ya taifa imeimarika
na ina vifaa vya kisasa na imefungua matawi yake manne katika Mikoa ya Dodoma,
Mwanza, Mbeya na Arusha.
Kuhusu magonjwa yasiyoambukiza serikali
imejielekeza kwenye mkakati mtambuka shirikishi wa sekta zote ili kuimarisha
mapambano eneo hili. Hivi sasa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia
magonjwa ya kuambukiza ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria na Ukoma ndiyo imepewa
na jukumu la kusimamia magonjwa yasiyoambukiza. Huu ni mtazamo chanya na shirikishi kwenye vita hivi tofauti na awali
kabla ya uhuru.
Baadhi
ya changamoto.
1. Kuongezeka kwa wimbi la magonjwa mapya yanayoambukiza
(Communicable Disease) na yasiyoambukiza (NCD).
2. Uchache wa raslimali kwa ajili ya uendeshaji
huduma za afya hususan watumishi, dawa, vifaa Tiba na vipimo.
3. Baadhi ya Wananchi kushindwa kumudu gharama za
tiba kutokana na kukosa Bima.
4. Utendaji wa mazoea wa baadhi ya waliopewa fursa
ya kuwa watumishi wa umma sekta ya afya jambo linalohitaji maboresho makubwa
kwenye mifumo ya motisha na uwajibikaji.
Mwelekeo mpya.
1. Kuwekeza kwenye ubora
wa huduma baada ya uwekezaji wa miundombinu (software engineering) sambamba na
kuimarisha mifumo ya uwajibikaji wenye matokeo kwa kupima viashiria vya matokeo
(performance merits by scorecards).
2. Kuimarisha Mifumo ya
Tehama ili kuweza kuimarisha udhibiti wa raslimali na uwajibikaji pia
kuharakisha huduma kwa mteja.
3. Sheria ya Bima ya Afya
kwa Wote (UHI)
4. Kuweka mazingira mazuri ya kuvutia
wawekezaji wa sekta binafsi katika Huduma za tiba na Viwanda vya dawa na vifaa
tiba.
5. Kuendelea kupanua huduma za kibingwa
na bingwa bobezi sambamba na raslimali watu na hivyo kufungua njia ya medical
tourism.
6. Sambamba na kuendelea na maboresho
ya afya ya msingi, kujikita kwenye afya kinga dhidi ya magonjwa yanayoepukika
kwa kuimarisha ushirikishaji wa jamii katika kumiliki huduma za afya.
7. Kuongeza uwekezaji na Ugunduzi
katika Tafiti za Tiba, Chanjo na Tiba Asili.
IDARA KUU YA
MAENDELEO YA JAMII;
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA MAFANIKIO YA WIZARA
YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWA MIAKA 60 YA UHURU WA
TANZANIA BARA
Ndugu Wanahabari
Kwa upande wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto yafuatayo yamefanyika;-
Ndugu Wanahabari, Tangu miaka ya 1960 hadi 1980 Wataalamu wa
Maendeleo ya Jamii walikuwa chachu ya kutekeleza kampeni mbalimbali za kitaifa
zinazohitaji ushiriki wa jamii ikiwemo Uhuru na Kazi; Siasa ni Kilimo; Kisomo
Chenye Manufaa; Azimio la Arusha; Mtu ni Afya; Elimu kwa Wote; Chanjo ya Watoto
wenye Umri Chini ya Miaka Mitano; Uhai, Ulinzi na Maendeleo ya Mtoto. Miaka ya
2019-2021 wataalam hawa wanaendelea kuamsha ari ya jamii kuboresha makazi yao
kupitia Kampeni ya Ujenzi wa Nyumba Bora ambapo hadi sasa jumla ya nyumba 4,008
zimejengwa.
Ndugu Wanahabari, Katika kipindi cha Mwaka 2015 hadi 2020
Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wamewezesha kaya 617,100 kuboresha vyoo, kaya
305,724 kuboresha maeneo ya kunawa mikono, kujengwa madarasa ya shule za msingi
6,521 na sekondari 2,499, hospitali 67 za Halmashauri na miradi mingine
vijijini na mijini.
Aidha, jamii ya sasa ina mwamko wa kujiletea maendeleo kwa kuanzisha
miradi inayolenga kutatua changamoto
zinazowakabili mfano ujenzi wa barabara, maboma ya madarasa, zahanati,
vituo vya afya. Pia, jamii imeanza utaratibu wa kujitafutia mitaji kwa ajili ya
uzalishaji na kujiwekea akiba kupitia vikundi vya VICOBA, Benki za kijamii na
SACCOs. Vile vile kuna mwamko mkubwa wa jamii kutumia teknolojia ya Habari na
Mawasiliano kupeana taarifa mbali mbali zikiwemo za masoko
Ndugu Wanahabari, Serikali, kupitia wizara hii baada ya Uhuru,
imeendelea kuzalisha wataalam wa Maendeleo ya Jamii ambao ni muhimu katika
kuchochea mabadiliko na kufanya mageuzi ya kifikra miongoni mwa jamii ili
kuwawezesha wananchi kushika hatamu ya maendeleo yao. Katika kipindi cha miaka
60 ya uhuru, Serikali imepanua wigo wa kutoa mafunzo ya wataalam wa maendeleo
ya jamii ambapo miaka ya 1960 kulikuwa chuo kimoja tu cha Tengeru na leo hii
kuna jumla ya vyuo 63 ambapo, kati ya hivyo vya Serikali ni 12 na vya binafsi
ni 51. Kati ya vyuo 12 vya Serikali 9 vinasimamiwa na Wizara ambapo mafunzo
hayo yanatolewa kuanzia ngazi ya Astashahada hadi Shahada ya uzamili.
Ndugu Wanahabari, Ili kuongeza thamani ya mafunzo yanayotolewa na
vyuo vilivyo chini ya Wizara, imeanzishwa programu za uanagenzi zinazomuandaa
mhitimu kujiajiri na kuajiriwa, programu za ubunifu zinazotoa fursa kwa
wanafunzi na jamii inayozunguka vyuo kufanya kazi za ubunifu unaosaidia kutatua
changamoto mbalimbali na ajira. Hadi sasa vimeanzishwa vituo Tisa (9) vya
ubunifu wa kidigitali na programu za ushirikishwaji jamii kutatua changamoto
zinazowakabili kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka zimeanzishwa.
Ndugu Wanahabari, baada ya Uhuru Serikali imejielekeza kwenye
kuimarisha Ustawi wa Watoto ambapo, katika miaka ya mwanzo ya 1970 Wizara
ilikuwa inaratibu na kusimamia upatikanaji wa haki na ulinzi wa mtoto kwa
kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Ili kuimarisha
upatikanaji wa haki, maendeleo na ustawi wa mtoto, Serikali imeongeza wigo wa
kutekeleza masuala ya watoto kwa kuridhia na kusaini mikataba ya kikanda na
kimataifa.
Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (1989)
na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (1990). Kupitia mikataba hii
Wizara imeendelea kunufaika na usaidizi wa kitaalamu pamoja na rasilimali fedha
kwa ajili ya utekelezaji wa masuala yanayohusu upatikaji wa haki na ustawi wa
watoto.
Ndugu Wanahabari, baada ya Uhuru, Serikali imepanua wigo wa
majukwaa ya watoto katika kujadili masuala yanayowahusu ambapo, katika kipindi
cha mwanzo cha Uhuru wa Tanzania Bara, jukwaa pekee la watoto la kujadili
masuala yanayowahusu na kufikisha ujumbe ilikuwa ni kupitia shule ikijumuisha
majukwaa kama chipukizi. Mfumo huu ulijumuisha watoto wale tu waliopo shule na
kuwaacha watoto wasiokuwa shule na hivyo kutokutoa fursa sawa ya kushirikisha
watoto wote.
Ndugu Wanahabari, Ilipofika mwaka 1991 Tanzania iliridhia na
kusaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki ya Mtoto ambapo moja ya matakwa ya
mkataba ni kuanzisha majukwaa ya watoto ili kujadili masuala yanayowahusu
ikiwemo upatikanaji wa haki na ulinzi dhidi yao. Jukwaa hili huwajengea watoto
uwezo katika nyanja za uongozi na uzalendo, uadilifu, ujasiliamali, stadi za
maisha na masuala mtambuka yakiwemo utunzaji wa mazingira, Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA) na kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI
Mnamo Disemba, 2002, Serikali iliratibu uundwaji wa mabaraza ya watoto
katika ngazi zote kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa, Kata, Halmashauri, Mkoa hadi
Taifa. Aidha, Wizara inaratibu uanzishwaji wa Madawati ya ulinzi wa watoto shuleni kwa lengo la kuwashirikisha watoto
katika kutoa taarifa za ukatili dhidi yao ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi
ya wakosaji. Kupitia madawati haya watoto wanajengewa ujasiri, uwezo wa
kujieleza, kujiamini ili kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi yao.
Ndugu Wanahabari, Mara baada ya Uhuru, Serikali ilihakikisha uwepo wa Sera, Sheria,
Miongozo na mifumo ya kushughulikia masuala ya watoto ili kuimarisha mifumo ya
kusimamia haki, ulinzi na ustawi wa watoto na kuwakinga dhidi ya ukatili wa
aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia.
Sera ya kwanza ya Maendeleo ya Mtoto iliandaliwa mwaka 1996 na kurejewa 2008 ambayo imeainisha
haki tano za msingi kwa watoto; haki ya kuishi, kuendelezwa, kulindwa,
kushiriki na haki ya kutobaguliwa.
Aidha, Sheria mbalimbali za kumlinda mtoto zilitungwa ikiwa ni pamoja
na Sheria ya mtoto Na 21 ya mwaka 2009 inayosimamia upatikaji wa haki za mtoto
na kumlinda mtoto dhidi ya aina zote za
ukatili. Hadi sasa, Wizara inaratibu huduma ya simu bila malipo kwa kutumia Na.
116 kwa ajili ya utoaji wa taarifa za matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya
watoto na ushauri wa namna ya kukabiliana na matukio hayo.
Ndugu Wanahabari, Katika kuimarisha huduma za Malezi, Makuzi na
Maendeleo ya awali ya mtoto, Wizara imeratibu uandaaji wa Programu Jumuishi ya
Kitaifa ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (2021/22-2025/26) yenye
lengo la kumlea na kumkuza mtoto kwa utimilifu wake. Katika kutimiza azma hiyo,
Wizara imenzisha vituo vya kijamii 30 vya mfano ambapo lengo ni kujenga vituo
hivyo katika Vijiji/Mtaa yote nchini.
Vilevile, Serikali imesajili jumla ya vituo 2,133 vya kulelea watoto
wadogo mchana kwa ajili ya kutoa huduma za malezi na uchangamshi wa awali.
Aidha ili kukabiliana na changamoto za afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe
Wizara iliratibu uandaaji na inasimamia utekelezaji wa Ajenda ya Kitaifa ya
kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe (2021/22 – 2024/25), lengo
likiwa kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana balehe wenye umri wa
10-19 katika ya maeneo ya VVU/UKIMWI, mimba za utotoni, Ukatili, Lishe bora,
Kuendelea kuwa shuleni na kujengewa ujuzi ili kupata fursa za kiuchumi.
Ndugu Wanahabari, Katika kuimarisha malezi ya watoto na familia
katika mazingira ya sasa, Wizara kwa nyakati tofauti imekuwa ikiratibu
upatikanaji wa huduma za malezi kwa watoto. Mnamo 2019, Wizara ilizindua Ajenda
ya Kitaifa ya Malezi ya Watoto na Familia ijulikanayo kama “Familia bora, Taifa imara”
lengo likiwa ni kuhimiza wazazi/walezi na jamii kwa ujumla katika
kutekeleza jukumu lao la msingi la malezi na utoaji wa matunzo kwa watoto na
familia ili hatimaye kuwakuza katika maadili mema na uzalendo kwa Taifa lao.
Vilevile, Katika kuimarisha mahusiano katika familia na jamii, Serikali
imeendelea kuratibu utoaji wa huduma za unasihi na msaada wa kisaikolojia. Aidha, huduma za
usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia na msaada wa kisaikolojia zimekuwa
zikitolewa kwa njia ya mtandao ili kuweza kuwafikia wananchi wengi
wanaokabiliwa na changamoto hizo.
Ndugu Wanahabari, Vilevile Serikali imeimarisha huduma za malezi,
matunzo na ulinzi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi kwa kuhakikisha
uwepo wa programu za malezi mbadala kama vile huduma za malezi ya kambo, uasili
wa watoto, malezi ya watu wa kuaminika kwa watoto walio nje ya malezi ya kifamilia na wale ambao wanakabiliwa na
vitendo vya ukatili katika familia; pamoja na afua za utengemano na marekebisho
ya tabia kwa watoto walio katika mkinzano na Sheria na wale wanaoishi na
kufanya kazi mitaani.
Aidha, katika kukabiliana na changamoto ya makao ya watoto, Serikali
inaratibu na kusimamia jumla ya makao ya watoto 239 ikilinganishwa na makao
moja yaliyokuwepo mwaka 1960. Kwa upande mwingine, Serikali kwa kushirikiana na
shirika la ABBOT FUND imejenga Makao ya Watoto katika Eneo la Kikombo Mkoani
Dodoma ambayo yalizinduliwa na Mhe. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 16 Juni 2021. Makao haya yanachukua
Watoto walio katika mazingira hatarishi ikiwemo wanaoishi na kufanya kazi
mitaani kwa lengo la kuwapatia huduma za msingi, kurekebisha tabia zao kwa
lengo la kuwaunganisha na familia zao.
Ndugu Wanahabari, Serikali pia imeweka utaratibu wa Maafisa
Ustawi wa Jamii kusimamia upatikanaji wa haki kwa watoto katika mahakama 147 za
watoto ambazo zilianzishwa hapa nchini kupitia Sheria ya Mtoto Na.21 ya mwaka
2009 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2019. Mahakama hizi zimesaidia kuharakisha
upatikanaji wa haki kwa watoto waliokinzana na sheria pamoja na wale
waliofanyiwa vitendo vya ukatili na wenye changamoto mbalimbali za malezi na
uangalizi. Katika kipindi cha mwaka 2019/20, jumla ya watoto 737 walihudumiwa katika
Mahakama za Watoto nchini. Kati yao, watoto 516 waliachiwa huru na watoto 221
walikutwa na hatia.
Ndugu Wanahabari, Serikali vilevile, imeendelea kuimarisha huduma
za malezi, matunzo na ulinzi kwa Wazee katika makazi ambapo imeboresha
miundombinu na upatikanaji wa huduma za msingi kama vile chakula, mavazi,
malazi, matibabu n.k. kwa sasa Serikali inasimamia na kuratibu jumla ya makazi
15 yanayomilikiwa na Serikali yenye jumla ya wazee 277 (Me-166, Ke- 111) na
makazi 20 yanayomilikiwa na taasisi binafsi yenye jumla ya wazee 537
(Ke-242,Me-295). Serikali imeimarisha ulinzi na usalama kwa wazee kwa
kutekeleza afua mbalimbali ambazo zimesaidia kupunguza vitendo vya ukatili
ikwemo mauaji kwa wazee.
Ndugu Wanahabari, Ushiriki wa Wazee katika masuala mbalimbali ya
kijamii na kimaendeleo umeimarika baada ya Serikali kuweka utaratibu wa kuwa na
Mabaraza ya Wazee katika ngazi zote, ambayo yameanzishwa kupitia Sera ya Taifa
ya Wazee ya mwaka 2003. Mabaraza 26 yameundwa katika mikoa yote ya Tanzania
Bara na kufanya Mabaraza kufikia 20,748. Mabaraza haya yanatumika katika
kusaidia jamii kuimarisha malezi ya vijana pamoja na utatuzi wa changamoto
mbalimbali kwenye jamii.
Vilevile, wakati wa
Uhuru mifumo ya utoaji huduma za afya kwa wazee imeboreshwa ambapo Serikali
imekuwa ikifanya utambuzi wa wazee wasiojiweza na kuwapatia vitambulisho vya
matibabu bila malipo. Aidha, Serikali imewezesha uundwaji wa timu za uratibu na
usimamizi wa huduma katika hospitali na vituo vya afya nchini ili kutoa
usaidizi na kuhakikisha wazee wanapata huduma. Timu hizo zinajumuisha wataalam
watatu (3) ambao ni Daktari, Muuguzi na Afisa Ustawi wa Jamii. Aidha, Serikali
imehamasisha na kuhakikisha kila kituo kinaweka utaratibu wa kuwa na bango
linalosomeka ‘Mpishe Mzee Kwanza’ ili kukumbusha na kuhamasisha wajibu wa watoa
huduma kujali wateja wa kundi hili pamoja na jamii kuona umuhimu wa kuwapisha
wazee ili wapate huduma mapema
Ndugu Wanahabari, Katika kushughulikia Maendeleo ya Wanawake na
Jinsia, Serikali imefanya Jitihada za kuimarisha ushiriki wa wanawake katika
nafasi za uongozi ndani na nje ya nchi. Wakati
Baraza la kwanza la Mawaziri linaundwa mara baada ya uhuru halikuwa na mwanamke
hata mmoja. Mwanamke wa kwanza kuwa
Waziri ilikuwa mwaka 1965 ambapo Bi Lucy Selina Lameck Somi aliteuliwa kuwa
waziri mdogo wa Shirika na Maendeleo ya Jamii. Tangu kipindi hicho wanawake
wameendelea kuaminiwa ambapo kwa sasa idadi ya Mawaziri wanawake imefika saba (7),
Wabunge wanawake imeongezeka kutoka wabunge 127 mwaka 2015 hadi kufikia wabunge
145 mwaka 2020.
Ndugu Wanahabari, Kutokana na jitihada hizo, kwa mara ya kwanza
nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina Rais wa Awamu ya Sita ambaye ni
mwanamke Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na pia amewahi kushika nyazifa
mbalimbali kabla ya kuwa Rais. Wengine ni Mheshimiwa Anna Makinda, Spika wa
Kwanza mwanamke wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Tulia Akson ambaye ni Naibu Spika wa
sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ndugu Wanahabari, Kimataifa nchi inajivunia Mheshimiwa Getrude
Mongela aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa nne wa Umoja wa Mataifa wa kuhusu
masuala ya wanawake Duniani uliofanyika mwaka 1995 Jijini Beijing China,
Profesa Anna Tibaijuka alikuwa Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa
la Makazi Duniani (UNHABITANT) kuanzia mwaka 2006 hadi 2010; Dkt Asha Rose
Migiro amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa kutoka kwaka 2007 hadi 2012 na
Dkt Stergomena Lawrance Tax
alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya SADC kwa
kipindi cha miaka nane kutoka 2013 hadi 2021. Kwa sasa Dkt. Stergomena Tax ni
mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa.
Ndugu Wanahabari, Katika kuwezesha wanawake kiuchumi, Serikali
katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru imewezesha wanawake kushiriki kikamilifu
katika uchumi ikiwemo kuwezesha nyenzo mbalimbali ikijumuisha kutoa mikopo
isiyo na riba inayotokana na kutengwa kwa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya
Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake, Dirisha la mikopo
kwa wanawake kupitia Benki ya Wanawake na sasa Benki ya Posta, VICOBA, SACCOS,
Sekta binafsi, taasisi za fedha na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambayo
huwezesha wanawake kiuchumi.
Serikali pia imeimarisha mifumo ya kupambana na kuzuia vitendo vya
ukatili wa wanawake na Watoto kwa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili
Dhidi ya Wanawake na Watoto yaani MTAKUWWA (2017/18 2021/22). Jitihada hizi
zimewezesha kamati 18,186 mpaka sasa kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa hadi Taifa. Aidha, yameanzishwa Madawati ya Jinsia na
Watoto 420 katika vituo vya Polisi, Madawati ya Jinsia 153 katika Jeshi la Magereza na Dawati katika Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya kupambana na vitendo
vya rushwa ya ngono kupitia Kampeni ya “Vunja Ukimya.
Ndugu
Wanahabari, Serikali kupitia Wizara hii ina dhamana ya kuratibu
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Sekta ya Mashirika yasiyo ya kiserikali
haikutambulika katika kipindi cha uhuru kwani taasisi zilizojulikana kipindi
hicho ni taasisi za Dini na vyama vya wafanyakazi. Mashirika haya yalianza
kuibuka kwa kasi kuanzia miaka ya 1990 baada ya mabadiliko mbalimbali ya
kiuchumi.
Hivyo, katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru, Serikali imeweka mazingira
wezeshi kwa mashirika haya kwa kutunga Sheria Na. 24 ya mwaka 2002 ambayo ndiyo
ilianza kuweka Taratibu za uratibu na usajili wa Mashirika hayo. Aidha, katika
kuimarisha utoaji wa huduma za usajili na uratibu Serikali imefanikiwa kutengeneza Mfumo wa Kieletroniki wa Usajili na
Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NIS) kwa lengo la kuboresha
mazingira ya utendaji kazi ili kuleta ufanisi na tija katika uratibu wa
Mashirika hayo.
Ndugu Wanahabari, Mfumo huu umesaidia kupunguza gharama zilizokuwa zikitumiwa na wadau wa
Mashirika kupata huduma mbalimbali kutoka Ofisi ya Msajili na kuwezesha
upatikanaji wa taarifa muhimu zikiwepo taarifa za fedha na taarifa za
utekelezaji za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, pia kuongezeka kwa usajili
kutoka Mashirika 404 mwaka 2005 hadi kufikia Mashirika 11,731 tarehe 29 Oktoba,
2021. Mashirika hayo yamechangia kuleta maendeleo kwa kutoa huduma za kijamii
ikiwemo huduma za afya, elimu, kilimo, maji, mazingira, haki za binadamu,
jinsia, na utawala bora.
Aidha, Serikali imeendelea kujenga na kuimarisha uhusiano kati
yake na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuboresha mazingira ya Mashirika
hayo kufanya kazi pamoja na kujenga uelewa kwa Mashirika hayo kuhusu masuala ya
kodi, uhamiaji na uratibu wa pamoja wa mashirika katika ngazi zote zikiwemo
Wizara za Kisekta, Sekretarieti za Mikoa, Mashirika yenyewe na Sekta Binafsi.
Ndugu Wanahabari, Katika kuimarisha uhusiano huo, kwa mara ya
kwanza katika historia, Serikali imefanikisha Mkutano wa sekta ya Mashirika
yasiyo ya Kiserikali ambao ulihutubiwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haya ni mafanikio makubwa kwa Sekta hii
ambapo Serikali imeonesha dhamira ya kushirikiana nayo na kutambua mchango wao
ambapo kwa mwaka 2020 jumla ya trillioni 1.1 zilitumika na mashirika hayo
katika Miradi ya maendeleo na ajira za wazawa 6194 zilizalishwa na Mashirika
hayo.
Vilevile, Serikali
imefanikiwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
Na.3/2019 pamoja na kutunga kanuni tatu zenye lengo la kuweka mazingira wezeshi
ya utekelezaji wa sheria hiyo. Kuwepo kwa Sheria hii pamoja na kanuni zake
imewezesha Mashirika mengi kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria,
Taratibu, Mila na Desturi za Nchi na
kuimarisha uwazi na uwajibikaji wa mashirika hayo.
Mwisho niwatakie kila la Heri watanzania wote katika kuadhimisha miaka
60 ya Uhuru wa nchi yetu. “MIAKA 60 YA
UHURU; TANZANIA IMARA, KAZI IENDELEE”.
Imetolewa na;
Dkt.Dorothy Gwajima (Mb)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA WAZEE NA WATOTO
Comments
Post a Comment