Wateja wa CRDB kutibiwa JKCI kwa punguzo la asilimia 50%
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bruce Mwile wakibadilishana mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya JKCI na Benki ya CRDB leo wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba huo iliyofanyika katika ukumbi wa JKCI jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bruce Mwile wakimjulia hali mtoto aliyelazwa katika wodi ya watoto wenye magonjwa ya moyo kabla ya hafla fupi ya kusaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya taasisi hizo iliyofanyika katika ukumbi wa JKCI leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na viongozi wa JKCI na wenzao kutoka Benki ya CRDB wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya taasisi hizo iliyofanyika katika ukumbi wa JKCI leo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bruce Mwile akielezea namna benki hiyo itakavyoshirikiana na JKCI kufikisha huduma katika jamii wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya taasisi hizo iliyofanyika katika ukumbi wa JKCI leo jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Benki ya CRDB wakifuatilia yaliyokuwa yakiendelea wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya taasisi hizo iliyofanyika katika ukumbi wa JKCI leo jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
*************************************************************************************************
Wateja wa hadhi, wastaafu na wafanyakazi wanaopitisha
mishahara yao katika benki ya CRDB kupata punguzo la asilimia 50 wanapohitaji
kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI).
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla fupi ya kusaini
mkataba wa makubaliano kati ya JKCI na Benki ya CRDB kuendeleza ushirikiano
uliopo baina yao na kutoa huduma kwa jamii.
Dkt. Kisenge alisema Benki ya CRDB ni moja ya Taasisi za
fedha kubwa nchini inayochangia maendeleo ya jamii katika nyanja mbalimbali
ikiwemo sekta ya afya hasa kwa watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.
Benki ya CRDB ni moja ya wadau wa kwanza ambao walitambua
umuhimu wa kuwekeza katika afya hususan matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto
ambao wengi wao wanatoka katika familia ambazo hazina uwezo wa kulipia gharama
za matibabu ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema tangu mwaka 2017 Benki ya CRDB imechangia
kiasi cha shilingi milioni 775 ambazo zimetumika kulipia upasuaji wa moyo kwa
watoto 193.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB
Bruce Mwile alisema makubaliano waliyoingia na JKCI ni mwanzo wa ushirikiano
utakaoleta manufaa kwa wengi katika maeneo ya huduma za matibabu ya moyo kwa
kuwawezesha wateja wa CRDB kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
“Ushirikiano wa JKCI na Benki ya CRDB ni mfano mwingine unaoonyesha jinsi tunavyoendelea kujidhatiti kuhakikisha si tu tunawawezesha wateja wetu kutimiza malengo yao ya fedha bali pia mwenendo wao katika kutunza afya zao”, Mwile
Mwile alisema lengo la ushirikiano huo ni pamoja na kuisaidia
jamii ya watanzania kupata huduma bora za afya na kwa urahisi itakayowasaidia
kuweza kujenga uchumi imara wa nchi.
“Afya ni nguzo muhimu ya kimaendeleo na kijamii kwani bila
afya bora tunakosa nguvu na uwezo wa kufikia malengo yetu ya kiuchumi na
kijamii”, alisema Mwile
Aidha Mwile alisema JKCI imekuwa mnufaika wa muda wote
kupitia mbio za CRDB kwani kinachopatikana katika mbio hizo kiasi kikubwa
hupelekwa JKCI kwaajili ya kuwatibu watoto 100 kila mwaka.
“Mbali na ushirikiano huu tuliouanzisha leo tutaendelea kuchangia
matibabu ya watoto kila mwaka kwani tunatambua uhitaji mkubwa wa watoto wetu
wenye changamoto za magonjwa ya moyo”, alisema Mwile
Comments
Post a Comment