Wasanii waishukuru JKCI kwa kuwapa huduma za matibabu ya moyo
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kliniki ya
Kawe Nicholaus Steven akizungumza na mwananchi aliyefika katika kliniki hiyo
iliyopo jengo la Mkapa Health Plaza barabara ya Tuari jijini Dar es Salaam
kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo.
Picha na: Khamis Mussa
**************************************************************************************************************
Na Khamisi Mussa - Dar es Salaam
Wasanii waishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kuwapa huduma za uchunguzi, matibabu ya moyo pamoja na elimu ya namna ya
kujikinga na magonjwa hayo.
Huduma hiyo inafanyika katika Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe
jengo la Mkapa Hearth Plaza barabara ya Tuari imelenga kuyafikia makundi ya
wasanii na wanamichezo kwa kuwapa huduma bila gharama kila jumamosi na jumapili
kwa kipindi chote cha mwezi Desemba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii muigizaji kutoka bongo
movie Khadija Kizito alisema akiwa kama msanii ambaye ni kioo cha jamii ameona
ni muhimu kuwa mfano kwa wengine kujitokeza kupima afya yake kutokana na
maradhi yasiyoambukiza kuongezeka kwa kasi.
Khadija alisema baada ya kupata taarifa ya upimaji wa
magonjwa ya moyo kwa wasanii kutoka kwa viongozi wake na kutokana na alivyokuwa
akijisikia akaona atumie fursa hiyo kufika JKCI kupima afya yake.
“Nawashukuru sana viongozi wangu akiwemo Stive Mengele pamoja
na mama Hidaya Njaidi ambao wameweza kutufanikishia sisi wasanii kuweza kupata
huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo”, alisema Khadija
Aidha Khadija amewakumbusha wasanii wenzangu kujitokeza kwa
wingi kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo ili waweze kuchukua hatua mapema
kwani pamoja na kupata elimu sahihi kutoka kwa wataalamu wa JKCI.
“Nawashukuru sana wataalamu wa JKCI nimepokelewa vizuri,
nimefika hapa nikiwa sijisikii vizuri lakini baada ya mapokezi mazuri hata hali
yangu ikaanza kuwa na nafuu”, alisema Khadija
Kwa upande wake Salma Kanige ambaye ni mkazi wa Kawe ameipongeza
Serikali ya awamu sita kwa kujali afya za wananchi wake na kuwasogezea huduma
karibu na wanapoishi.
Salma alisema hapo awali matibabu ya moyo yalivyokuwa
yakitolewa eneo la upanga ilikuwa inawapa watu uvivu kuamka na kwenda upanga
kwaajili ya kuchunguza afya lakini baada ya huduma hizo kusogezwa Kawe inakuwa
rahisi mtu kufika na kuchunguza afya yake.
“Kwakweli Serikali hii imeona umuhimu wa kupeleka huduma
karibu na wananchi kwakutuongezea kituo hiki cha Kawe, zamani tulikuwa hatuendi
kufanya uchunguzi tulikuwa tunasubiri hadi tuumwe ndio tunaenda hospitali
kwasababu upanga ilikuwa mbali”, alisema Salma
Comments
Post a Comment