Afanyiwa upasuaji wa kuziba tobo lililokuwa kwenye chemba ya moyo
Wataalamu wa upasuaji mkubwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Cardio Start International la nchini Marekani wakimfanyia upasuaji wa kurekebisha mshipa mkubwa wa damu (Aorta) mgonjwa ambaye mshipa wake mkubwa umetanuka wakati wa kambi maalumu ya siku tano iliyofanyika katika Taasisi hiyo na kumalizika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.
Na:JKCI
***************************************************************************************************
Kijana mwenye umri wa miaka 19 amefanyiwa upasuaji mkubwa wa
moyo kuziba tobo lililokuwa kwenye chemba ya chini ya moyo upande wa kushoto
hivyo kupelekea damu kuzunguka nje ya moyo (LV Pseudo aneurysm).
Upasuaji huo umefanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa
moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwakushirikiana na wenzao kutoka
Shirika la Cardio Start International la nchini Marekani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii daktari bingwa wa
upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Willium Ramadhani alisema baada ya kumfanyia uchunguzi mgonjwa huyo waligundua
kuwepo kwa tobo kwenye chemba ya chini ya moyo lililopelekea kutengeneza
mabonge ya damu katika eneo hilo.
“Katika moyo wa mgonjwa chemba ya chini ya moyo upande wa
kushoto inayofanya kazi ya kusukuma damu sehemu zote za mwili kulikuwa na tobo
kubwa lililokuwa linatoa damu nje ya moyo ambalo lilishikiliwa na ngozi
inayofunika moyo (pericardium) na kama ngozi hiyo ingeachia mgonjwa angeweza
kupoteza uhai wake”, alisema Dkt. Willium.
Dkt. Willium alisema upasuaji wa moyo kwa mgonjwa huyo
ulihusisha mashine maalumu inayotoa damu kwenye moyo kupeleka kwenye mashine
(cardiopulmonary bypass machine) ili moyo uweze kufanyiwa matibabu bila
kuingiliana na msukumo wa damu.
“Katika upasuaji wake tulifanikiwa kuweka vifaa bandia kuziba
sehemu yenye tobo lililoleta hitilafu ambapo baada ya upasuaji huo mgonjwa
amepona na sasa amesharuhusiwa kurudi nyumbani”, alisema Dkt. Willium
Dkt. Willium alisema baada ya kupata taarifa ya kina kutoka
kwa mgonjwa inaonesha mgonjwa alipata ajali ya gari iliyomsababishia kutupwa
nje ya gari na kuangukia sehemu ya kifua kitu ambacho wataalamu wa afya
wanahisi tukio hilo ndilo lililopelekea kutoboka katika chemba ya chini ya moyo.
“Tatizo hilo linaweza kusababishwa na mambo mengi mengi ikiwemo
homa au maambukizi ya mara kwa mara, kwa huyu mgonjwa tunahisi ni ajali ya gari
kwani baada ya ajali hiyo alianza kupata dalili za kuchoka wakati akitembea na mapigo
ya yake ya moyo kwenda kasi jambo ambalo halikuwa kawaida kwake”, alisema Dkt.
Willium.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji mkubwa wa moyo kwa
watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Felix Shonyela alisema
wamefanya upasuaji wa moyo kwa watoto 15 katika kambi maalumu iliyofanywa na
wataalamu wa JKCI na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids lililopo nchini
Marekani.
Dkt. Shonyela alisema katika kambi hiyo wamewafanyia upasuaji
mkubwa wa moyo watoto waliokuwa na matatizo ya mishipa ya damu iliyotokea
sehemu tofauti na inapotakiwa kutokea (Arterial Switch Operation), matatizo ya
kuwa na mshipa mmoja unaotoa damu kwenye moyo badala ya kuwa na mishipa miwili
(Truncus Repair), na matatizo ya mishipa ya damu kuziba na kuwa midogo pamoja
na tundu kwenye moyo (TOF Repair).
“Upasuaji wa moyo kwa watoto wote 15 umefanyika kwa mafanikio
makubwa kwani wote tumefanikiwa kuwaondolea matatizo waliyokuwa nayo”, alisema
Dkt. Shonyela.
Comments
Post a Comment