JKCI yawanoa wataalamu wa afya jinsi ya kufanya kipimo cha ECHO
Daktari wa watoto kutoka Hospitali ya KCMC Lightness Chuwa
akiwaongoza madaktari wenzake kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) wakati wa mafunzo ya siku tano kwa
wataalamu wa afya kutoka Hospitali mbalimbali yanayofanyika katika Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwakushirikiana na Pediatric Association of Tanzania
na German Tropical Pediatrics (GTP).
Mkufunzi kutoka Utrecht nchini Netherlands Dkt. Martijn
Slieker akiwafundisha wataalamu wa afya kutoka Hospitali mbalimbali ndani na
nje ya nchi namna ya kuyatambua magonjwa ya moyo kwa watoto wakati wa mafunzo
ya siku tano ya kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi
(Echocardiography – ECHO) yanayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa kushirikiana na Pediatric Association of Tanzania na German Tropical
Pediatrics (GTP).
Na: JKCI
**********************************************************************************************************
Wataalamu wa afya 23 kutoka Hospitali mbalimbali nchini na
wawili kutoka nchini Kenya wameshiriki katika mafunzo ya kufanya kipimo cha
Kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – Echo) kwa watoto.
Mafunzo hayo ya siku tano ni mafunzo ya awamu ya saba tangu
kuanzishwa kwake mwaka 2018 yakifanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa kushirikiana na Pediatric Association of Tanzania na German Tropical
Pediatrics (GTP).
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Naiz Majani alisema kila mwaka mafunzo hayo ufanyika lengo likiwa kuwasaidia wataalamu
wa afya wanaotoa huduma kwa watoto kutambua magonjwa ya moyo kwa watoto mapema.
Mafunzo haya yamekuwa yakiudhuriwa na wataalamu wa afya
kutoka Tanzania na nchi nyingine kama vile Ujerumani na Uholanzi ambapo mwaka
huu tumepata wataalamu wa afya wawili kutoka nchini Kenya”, alisema Dkt. Naiz
Dkt. Naiz ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ubora wa Huduma
JKCI alisema mafanikio yaliyotokana na mafunzo hayo ni pamoja na kuwapa ujuzi
wataalamu wa afya kutoka hospitali za wilaya na mkoa ambao sasa wamekuwa na
uwezo wa kuyatambua magonjwa ya moyo kwa watoto mapema na kuwapa rufaa kufika
JKCI mpema.
“Kuna hospitali za mikoa ambazo tumeshazitambua na kuwapa
jukumu la kuendelea kufuatilila maendeleo ya watoto waliofanyiwa upasuaji wa
moyo ili kuwapunguzia gharama watoto hao kufuata huduma za maendeleo yao baada
ya upasuaji wa moyo huku JKCI”, alisema Dkt. Naiz
Kwa upande wake Daktari wa watoto kutoka Hospitali ya The
Karen iliyopo nchini Kenya Patrick Lydia alisema hii imekuwa mara yake ya
kwanza kushiriki mafunzo ya kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya
kazi baada ya kujaribu kuomba kushiriki mafunzo hayo mara mbili bila ya
mafanikio kutokana na idadi ya washiriki inayotakiwa kutosheleza.
Dkt. Patrick alisema mafunzo kama hayo pia yanapatikana
nchini Kenya lakini kutokana na idadi ya washiriki kuwa kubwa nafasi hizo
hutolewa kwa kipaumbele kwa wataalamu wanaofanya kazi katika Hospitali za
Serikali na wale wanaotoka hospitali binafsi husubiri kwa muda mrefu.
“Ninapenda kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto
hivyo nikaona ni fursa kwangu mimi kuanza kupata mafunzo ambayo yatanifikisha
katika malengo yangu ndio maana nikashiriki katika mafunzo haya kuona
nitafaidika kwa kiasi gani”, alisema Dkt. Patrick
Comments
Post a Comment