Dkt. Kisenge: Wanamichezo na Wasanii pimeni afya za mioyo yenu
**********************************************************************************************************
Wanamichezo na wasanii wametakiwa kufanya uchunguzi wa afya za mioyo yao mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa hayo ambayo yanaweza kuwasababishia kupata tatizo la shambulio la moyo au kifo cha ghafla.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza
katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC).
Dkt. Kisenge alisema kupima afya ya moyo ni muhimu kwani mtu
anaweza kuwa na matatizo hayo bila ya kuwa na dalili hivyo kuwataka wanamichezo
kutoanza michezo ghafla kwani mwili unaweza kutengeneza mabadiliko ambayo
yanaweza kuleta madhara ikiwemo kupata shambulio la moyo au kifo cha ghafla.
Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema ni muhimu wanamichezo wakafanya
uchunguzi wa afya za mioyo yao kabla hawajaanza kushiriki michezo ili kujikinga
na madhara yanayoweza kutokea wakati wa michezo kutokana na mabadiliko ya
mapigo ya moyo, presha kwenye damu, pamoja na mabadiliko ya oksijeni
inayotakiwa kuwepo kwenye damu wakati wa michezo.
“Ili kuwapa motisha ya kufanya uchunguzi wa afya wanamichezo na wasanii Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Kliniki ya Kawe itatoa huduma ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo
kwa wanamichezo na wasanii kwa punguzo la asilimia 20 kwa kipindi cha wiki moja ya tarehe 11-16/11/2024”.
“Ili wananchi wengi wapate
huduma ya kibingwa ya matibabu ya moyo JKCI ina kampeni maalumu ya kutoa huduma
ya upimaji na matibabu ya moyo kwa watu mbalimbali. Kampeni hii ilianza wiki
iliyopita kwa wahariri kutoka vyombo vya habari hapa nchini, wiki hii tutakuwa
tunatoa huduma kwa wanamichezo na wasanii kwa punguzo la asilimia 20”, alisema
Dkt. Kisenge.
Mtaalamu huyo wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu alisema mwitikio
wa wanamichezo wa mpira wa miguu katika kufanya uchunguzi wa afya ya moyo
umekuwa mkubwa kwani timu za ligi kuu zimekuwa zikifanya uchunguzi wa afya mara
kwa mara zikiwemo timu za Yanga na Simba lakini bado kuna timu nyingine pamoja
na vikundi vya mazoezi ya jogging haviweki mkazo katika suala ya kuchunguza
afya.
“Ukitembea umbali unaochukua nusu saa mara tatu kwa wiki
ukatoka jasho inatosha kukulinda na madhara yanayoweza kusababisha magonjwa ya
moyo, ni vyema kujikinga na magonjwa haya kuliko kusubiria kuumwa kwani gharama
za matibabu ni kubwa na mara nyingi tunaipa serikali mzigo wa kugharamia matibabu
yake jambo la muhimu la kuzingatia kabla hujaanza kufanya mazoezi ukumbuke
kupima afya kwanza”, alisema Dkt. Kisenge.
Comments
Post a Comment