Wafundishwa jinsi ya kurekebisha valvu za moyo
Wataalamu wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wakishirikiana na wenzao kutoka Shirika la Open Heart
International (OHI) la nchini Australia kumfanyia upasuaji wa kurekebisha valvu
ya moyo mgonjwa mwenye matatizo ya valvu wakati wa kambi maalumu ya siku 6
inayofanyika katika taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
*******************************************************************************************************
Wataalamu wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wanapewa mafunzo ya kutibu valvu za moyo kwa kuzirekebisha
badala ya kuzitoa na kuweka valvu za bandia.
Mafunzo hayo yanatolewa na wataalamu wa afya kutoka Shirika
la Open Heart International la nchini Australia kwa kipindi cha wiki moja
wakati wa kambi maalumu inayoendelea JKCI lengo likiwa kuwapa muda wagonjwa
wenye changamoto za valvu kujenga familia zao kabla ya valvu zao kubadilishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Angela Muhozya alisema kambi hiyo ni maalumu kwaajili ya kujifunza na kuongeza
ujuzi kwa wataalamu wa upasuaji wa moyo wa JKCI.
Dkt. Angela alisema kwa kawaida mgonjwa akishabadilishiwa
valvu za moyo anatakiwa kutumia dawa za kuzuia kugandisha damu katika maisha yake yote, lakini kama wakizirekebisha inawasaidia
kutotumia dawa mapema na kwa wanawake inawapa muda ya kutengeneza familia zao na
baadaye hubadilishiwa.
“Sasa hivi kuna wimbi kubwa la watoto wenye umri kati ya
miaka 15 hadi 20 wanapata matatizo ya lavlu za moyo kuchoka na kuhitajika
kubadilishiwa valvu, tumefanya kambi hii kuwasaidia wagojwa kurekebisha valvu
zao”,
“Wanawake ambao valvu zao za moyo zimechoka na kuwekewa valvu
bandia inawazuia kubeba ujauzito kutokana na dawa wanazotakiwa kutumia katika
maisha yao yote lakini kama tutazirekebisha tutakuwa tumewapa muda wa kujenga
familia zao kwanza na baada ya muda ndio zitabadilishwa”, alisema Dkt. Angela
Kwa upande wake Daktari kutoka Shirika la Open Heart
International la nchini Australia Dareen Wolfers alisema wataalamu wa afya
kutoka shirika hilo wamekuwa wakishirikiana na wataalamu wa JKCI toka mwaka
2015 ambapo kwa sasa wanaiona taasisi hiyo kuwa taasisi bora Afrika katika
kutoa huduma za matibabu ya moyo.
Dkt. Wolfers alisema katika kambi hii wamekuja kwaajili ya
kuongeza ujuzi kwa wataalamu wote wanaomhudumia mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji
wa moyo hivyo kuleta wataalamu wa upasuaji, wataalamu wa usingizi, madaktari na
wauguzi wa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) cha wagonjwa
waliofanyiwa upasuaji wa moyo.
“Katika kambi hii tutawafanyia upasuaji wa moyo watoto kati
ya 8 hadi 10 na watu wazima kati ya 5 hadi 8 kwani kambi hii ni kwaajili ya
kujifunza Zaidi”, alisema Dkt. Wolfers
Naye afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
anayepata mafunzo kupitia kambi hiyo Lilian Peter alisema mafunzo anayopata
yanamsaidia kuweza kutambua kwa haraka changamoto anazopitia mgonjwa na kuweza
kumsaidia.
Lilian alisema ameanza kufanya kazi za kuhudumia katika
chumba cha wagonjwa wa dharura na mahututi (ICU) tangu mwaka 2019, ujuzi
anaoupata kutoka kwa wataalamu hao unazidi kumpa uwezo wa kuokoa maisha ya
wagonjwa hao.
“Kupitia mafunzo haya naweza kusimama mwenyewe, nikamuhudumia
mgonjwa na kutambua matatizo ambayo mgonjwa anayapata na kumsaidia kwa wakati”,
alisema Lilian
Lilian alisema baada ya yeye kupata mafunzo hayo atawasaidia
wataalamu wengine wa afya kuweza kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na
mahututi ili kwapamoja waweze kuokoa maisha.
Comments
Post a Comment