JKCI, MOI NA MNH waitwa Comoro kutoa huduma za matibabu ya kibingwa


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimuonyesha Waziri wa Ulinzi wa Comoro Mhe. Yousoufa Mohamed Ali  sehemu ya kusubiria wagonjwa wa kliniki maalumu ya VIP alipotembelea taasisi hiyo leo kwaajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.

Waziri wa Ulinzi wa Comoro Mhe. Yousoufa Mohamed Ali akizungumza na viongozi wa wizara ya Afya, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI),Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)  alipozitembelea hospitali hizo leo kwaajili ya kuona namna ambavyo zitawatuma wataalamu wake  kwenda kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa Comoro. 

Waziri wa Ulinzi wa Comoro Mhe. Yousoufa Mohamed Ali akiagana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Mhandisi Ismail Rumatila mara baada ya kukutana na viongozi wa wizara hiyo, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI),Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na  kwaajili ya kuona namna ambavyo hospitali hizo zitawatuma wataalamu wake kwenda kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa Comoro.

Waziri wa Ulinzi wa Comoro Mhe. Yousoufa Mohamed Ali na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Mhandisi Ismail Rumatila wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wizara hiyo, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI),Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) mara baada ya kumaliza ziara yake ya kuona namna ambavyo hospitali hizo zitawatuma wataalamu wake kwenda kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa visiwa hivyo.

***********************************************************************************************************************************************************************************************

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Watu wa Comoro Mhe. Yousoufa Mohamed Ali ameziomba Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ,Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwenda kutoa huduma za kibingwa za matibabu kwa wananchi wa nchi hiyo.

Mhe. Ali alitoa  ombi lake leo jijini Dar es Salaam wakati akiongea na viongozi wa Wizara ya Afya pamoja na wa hospitali hizo katika  mkutano baina yao uliofanyika kwenye  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Waziri huyo wa Ulinzi alisema wataalamu wa hospitali hizo wakienda nchini Comoro licha ya kuwasaidia wananchi kupata huduma pamoja na kubadilisha ujuzi wa kazi na talaamu wenzao lakini pia wananchi wa Comoro watafahamu wakija kutibiwa Tanzania gharama za matibabu zitakuwa kiasi gani na watatibiwa na madaktari gani.

Ushirikiano baina ya Tanzania na Comoro ni wa kihistoria kuanzia mwaka 2003, zaidi ya raia 2000 wa Comoro huingia Tanzania kwa mwezi wanakuja hapa kupata huduma za matibabu na wengine kufanya biashara”.

“Tanzania inapata dola za kimarekani milioni 100 kutoka Comoro, hii inaonesha ushirikiano wetu ni wa umuhimu nichukue fursa hii kuwaomba  mfike Comoro ili muone namna ambavyo mtaweza kutusaidia kuwatibu wananchi wetu, pia kuwajengea uwezo wataalam wetu wa afya”, alisema Mhe. Ali.

 Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Mhandisi Ismail Rumatila alisema  Tanzania ilitia saini ya ushirikiano na Jamhuri ya Watu wa Comoro Julai, 2024 katika sekta ya afya ulioruhusu uhamishaji wa wagonjwa kutoka nchini humo kuletwa katika hospitali za afya za umma za Tanzania kwa matibabu.

 “Kupitia ushirikiano huu taasisi zetu za JKCI, MOI na MNH watalazimika kwenda Comoro na kuona namna bora ya kutoa matibabu kwa wananchi na kuwajengea uwezo watoa huduma wa Comoro hatua hii ni utekelezaji wa agizo la Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutaka Tanzania iwe kituo cha umahiri wa tiba utalii barani Afrika”,  alisema  Mhandisi Rumatila.

 Akieleza huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema taasisi hiyo inatoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima, inafanya tafiti na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya.

 Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema umbali wa kutoka Comoro hadi Tanzania ambako kunapatikana huduma za kibingwa za matibabu ya moyo ni karibu pia gharama za matibabu ziko chini ukilinganisha na nchi zingine.

 “Taasisi yetu kwa mwaka mmoja imeona wagonjwa 369 kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Comoro ni muhimu wacomoro wakatumia huduma zetu za matibabu ya moyo kwani tuna wataalamu wa kutosha pamoja na vifaa tiba vya kisasa pia mazingira yetu ni sawa na ya kwao”, alisema Dkt. Kisenge.

 Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo Asha Izina alimshukuru waziri huyo kwa kutembelea taasisi hiyo na kusema kuwa JKCI itawatuma wataalamu wake kwenda nchini humu kutoa huduma kwani wao pia wanahitaji kujifunza kutoka kwao.

 Chini ya uratibu wa Wizara ya Afya hospitali hizo zikiwemo Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) na Taasisi ya Saratani ya Ocean road hivi karibuni zitakwenda kufanya kambi  kambi ya matibabu nchini  Comoro ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kukuza tiba utalii nchini.



Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024