Wanawake wa JKCI SACCOS wanaongoza kwa kumiliki hisa
Mwenyekiti wa Chama cha kuweka akiba na mikopo (SACCOS) cha
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tulizo Shem akizungumza na wanachama
wa SACCOS hiyo wakati wa mkutano mkuu wa mwaka uliofanyika leo katika ukumbi wa
Taasisi hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
na mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa mwaka wa wanachama wa Chama cha kuweka
akiba na mikopo (SACCOS) cha JKCI akiwapongeza wanachama hao kwa kuweka
jitihada za kuboresha mfuko wa SACCOS leo wakati wa mkutano huo uliofanyika
katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam
Afisa Ushirika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mihayo Malunde akielezea namna fedha zinazokusanywa na Chama cha kuweka akiba na mikopo (SACCOS) cha JKCI zinaweza kuongeza uchumi wa wanachama wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa wanachama wa SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) uliofanyika leo katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam
Mjumbe wa Chama cha kuweka akiba na mikopo (SACCOS) cha
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Magreth Mbarook akiuliza swali wakati wa
mkutano mkuu wa mwaka wa SACCOS hiyo uliofanyika leo katika ukumbi wa Taasisi
hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa Chama cha kuweka akiba na mikopo (SACCOS) cha
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Morris Obwanga akichangia mada wakati wa
mkutano mkuu wa mwaka wa SACCOS hiyo uliofanyika leo katika ukumbi wa Taasisi
hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa Chama cha kuweka akiba na mikopo (SACCOS) cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Flora Kasembe akiomba kupata ufafanuzi wa taarifa zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa SACCOS hiyo uliofanyika leo katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa Chama cha kuweka akiba na mikopo (SACCOS) cha
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Eng. Abella Rwiguza akichangia mada
wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa SACCOS hiyo uliofanyika leo katika ukumbi wa
Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
**************************************************************************************************
Wanawake wanachama wa Chama cha kuweka akiba na mikopo
(SACCOS) cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wanaongoza kwa kumiliki hisa
zenye thamani ya shilingi milioni 36.9 ukilinganisha na wanaume wanaomiliki
hisa zenye thamani ya shilingi milioni 33.
Umiliki huo umechangiwa na idadi ya wanawake kuwa 190 sawa na
asilimia 61 ukilinganisha na wanaume 151 sawa na asilimia 39 katika SACCOS, hivyo kupelekea hisa kuongezeka na kuwa na
thamani ya shilingi milioni 69.9 kutoka hisa zenye thamani ya shilingi milioni
4.8 mwaka 2020.
Akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa mwaka uliofanyika leo jijini
Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema kutokana
na mafanikio ya SACCOS hiyo menejimenti ya Taasisi iliamua kutoa ofisi kwaajili
ya uendeshaji wa shughuli za SACCOS ikiwa ni sehemu ya kuchangia ukuaji na maendeleo
ya SACCOS.
Dkt. Kisenge amewataka viongozi wa SACCOS hiyo kuendelea
kuzingatia sheria na weledi katika kuendesha shughuli za SACCOS ikiwa ni pamoja
na kufanya kaguzi za hesaba, wanachama kupewa taarifa kwa wakati, kulinda haki
za wanachama na kudumisha uwazi.
“Kumbukumbu zinaonyesha wazo la kuanzisha SACCOS hii
lilipatikana mwaka 2019 na baadae 2020 kuzinduliwa na kuanza shughuli zake
baada ya uongozi wa JKCI kuipa mtaji kama kianzio cha shilingi milioni 5 na leo
tunaona SACCOS ina uwezo wa kukopesha zaidi ya shilingi milioni 30”, alisema
Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge aliwataka viongozi wa SACCOS hiyo kuangalia
namna ambavyo SACCOS inaweza kuongeza mapato yatakayosaidia kuongeza mikopo kwa
wanachama ili wote kwapamoja waweze kufaidi matunda ya SACCOS hiyo.
Akitoa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za SACCOS hiyo
Mwenyekiti wa SACCOS ya JKCI Dkt. Tulizo Shem alisema kwa kipindi cha Januari
2024 hadi Novemba 2024 kiasi cha shilingi milioni 578 kimewekwa na wanachama
341 hivyo kufanya jumla ya akiba iliyowekwa kuwa shilingi bilioni 1.2.
“Jumla ya tozo zenye thamani ya shilingi milioni 35 zimekusanywa
hadi Novemba 2024, ukifananisha na shilingi milioni 31 zilizokusanywa mwaka
2023 hivyo kuleta ongezeko la asilimia 12”, alisema Dkt. Tulizo Shem
Dkt. Shem alisema thamani ya mkopo kwa wanachama imeongezeka
kutoka shilingi milioni 13 mwaka 2020 ikiwa ni mikopo 15 hadi kufikia shilingi
bilioni 1.12 mwaka 2023 ikiwa ni mikopo 443.
Upande wa akiba za wanachama Dkt. Shem alisema akiba za
wanachama zimeendelea kukua kutoka shilingi milioni 1.25 Januari 2020 hadi
kufika shilingi milioni 580.3 Desemba 2023.
Aidha Dkt. Shemu alisema SACCOS hiyo inakabiiwa na changamoto
ya uhitaji mkubwa wa mikopo kwa wananchama ukilinganisha na ukwasi uliopo
pamoja na ukosefu wa elimu ya mifumo ya Tehama kwa wanachama.
Kwa upande wake mjumbe wa SACCOS hiyo Vedastus Lazaro amewaomba
wafanyakazi ambao bado hawajajiunga na SACCOS hiyo kujiunga ili kuweza kutoa
michango ya mwezi inayosaidia kuweka akiba itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Vedastus alisema kupitia SACCOS hiyo ameweza kupata mkopo
ambao aliutumia katika biashara zake pamoja na kuwasomesha wadogo zake kwani
bila ya mkopo huo asingeweza kufanya hivyo.
Ziada Joram ambaye pia ni mjumbe wa SACCOS hiyo alisema
SACCOS ya JKCI imemsaidia kuwekeza fedha ambazo kama zingekuwa kwenye akaunti
yake angekuwa ameshazitumia.
Ziada alisema kupitia SACCOS hiyo ameweza kuchukua mkopo kwa
urahisi na kwa wakati hivyo kuweza kufanya majukumu muhimu ya kifamilia.
“Kwakweli wafanyakazi ambao bado hawajajiunga na SACCOS hii
wajiunge ili waweze kuwekeza na kukopa kwa maendeleo yao na taifa kwani SACCOS
yetu ina riba ndogo ukifananisha na sehemu nyingine zinazotoa mikopo”, alisema
Ziada
SACCOS ya wafanyakazi wa JKCI (JKCI SACCOS) ilianzishwa rasmi
mwezi Agosti mwaka 2019 kwa Na. DSR. 1705 kwa kuzingatia sheria ya ushirika ya
mwaka 2023 na kuanza majukumu yake Januari mwaka 2020.
Comments
Post a Comment