Dawa za Shilingi 16,196,119 zatolewa bila malipo kwa wananchi wa Handeni
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda akimpima kipimo
cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mtoto
wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba
mkoba iliyokuwa ikifanyika katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni
iliyopo Wilaya ya Handeni vijijini mkoani Tanga.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group Daniel Mkuyu akimfanyia kipimo cha kuangalia jinsi mfumo
wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiograph – ECG) mkazi wa Mkata
wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba
mkoba iliyokuwa ikifanyika katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni
iliyopo Wilaya ya Handeni vijijini mkoani Tanga.
Fundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group Eliza Shuma akimfanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mkazi wa Mkata wakati wa kambi
maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa
ikifanyika katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni iliyopo Wilaya
ya Handeni vijijini mkoani Tanga.
Wananchi wa Wilaya ya Handeni Vijijini wakisubiri kupatiwa
huduma wakati wa wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanyika katika Hospitali ya Halmashauri
ya Wilaya ya Handeni iliyopo Wilaya ya Handeni vijijini mkoani Tanga. Jumla ya
wananchi 497 wa Wilaya ya Handeni vijijini wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya
magonjwa ya moyo.
Na: JKCI
********************************************************************************************************
Dawa za moyo, shinikizo la damu na sukari zenye thamani ya
shilingi 16,196,119 zatolewa bila malipo kwa wananchi wa Wilaya ya
Handeni mjini na Handeni vijijini waliokutwa na magonjwa hayo.
Dawa hizo zimetolewa wakati wa kambi maalumu ya siku nne ya
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwakushirikiana na wenzao wa Hospitali ya
Wilaya ya Handeni iliyopo Handeni mjini na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya
ya Handeni iliyopo Handeni vijijini mkoani Tanga.
Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group na
mratibu wa kambi hiyo Eva Wakuganda alisema kupitia kambi hiyo wamewakuta watu
wengi wakiwa na matatizo ya shinikizo la damu, sukari na magonjwa ya moyo
lakini kutokana na hali zao za maisha kushindwa kununua dawa.
“Tumekuja na dawa zenye thamani ya shilingi milioni
16,196,119 ambazo zote tumezitoa kwa wananchi ambao tumewakuta na matatizo ya
moyo, shinikizo la damu na sukari kwani wengi wao walitumia dawa pale
walipogundulika tu kuwa na magonjwa haya na baada ya hapo hawakuendelea kutumia
dawa hizo kutokana na vipato vyao kuwa vya hali ya chini”, alisema Dkt. Eva
Dkt. Eva aliongeza kuwa katika kambi hiyo jumla ya watu 908
walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo ambapo kati yao watu 411 walikuwa
kutoka Wilaya ya Handeni mjini na watu 497 walikuwa kutoka Wilaya ya Handeni
vijijini.
“Hapa Handeni vijijini tumewakuta watu 133 wakiwa na shida mbalimbali
za moyo ambapo kati yao wapo watoto 9 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo,
tumewaanzishia dawa na wengine tumewapa rufaa kufika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwaajili ya matibabu zaidi”, alisema Dkt. Eva
Kwa upande wa wananchi waliopata huduma katika kambi hiyo
wameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kufikisha huduma za kibingwa kwa
wananchi waliopo katika Wilaya kwani wao wamekuwa wakisahaulika huku huduma
nyingi zikipelekwa kwa wananchi wanaoishi kwenye mikoa.
Ridhiwan Abdi alisema kuwa wamekuwa wakisikia vitu vingi vya
kijamii vikifanyika katika mkoa wa Tanga lakini huduma hizi za upimaji
zimewafikia wananchi wa Wilaya ya Handeni bila kuwabagua wale waliopo Handeni
vijijini.
“Serikali yetu inatujali sana wananchi wake, mimi leo
nimepata huduma hapa bila gharama yoyote na sikuishia hapo nikapata na dawa
pia”, alisema Ridhiwani
Naye Mwanaidi Suleimani alitoa shukrani zake kwa Serikali na kwa
wataalamu waliojitoa kutoa huduma kwa wananchi hadi usiku bila ya kuchoka na
pale walipohitaji ufafanuzi zaidi wataalamu hao walitoa ushirikiano kutoa
maelezo zaidi.
Mwanaidi alisema mara nyingi wagonjwa wakienda hospitali
wamekuwa na uoga wa kuzungumza yale wanayopitia lakini kupitia kambi hiyo
wananchi wameweza kujieleza vizuri kutokana na wataalamu walioshiriki katika
kambi hiyo kuwajali wananchi na kuwa nao karibu.
“Ninaiomba Serikali na wakati mwingine itukumbuke tena kwani
bado wapo wananchi wengi hawajaweza kufika katika siku hizi mbili kupata huduma
hivyo ikijipanga tena na kuja itakuwa imesaidia watu wengine wengi zaidi”,
alisema Mwanaidi
Comments
Post a Comment