Dkt. Kisenge : Wasanii jitokezeni kupima moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Da es Salaam kuhusu huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo
itakayotolewa kwa wasanii kwa mwezi wa
Desemba 2024 na Januari 2025 katika
kliniki ya Taasisi hiyo iliyopo Kawe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana, Kaimu Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Gervas Kasiga na viongozi wa vyama vya wasanii kabla ya kuanza kwa mkutano kati yao na waandshi wa habari kuhusu huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo itakayotolewa kwa wasani kwa mwezi wa Desemba 2024 na Januari 2025 katika kliniki ya Taasisi hiyo iliyopo Kawe.
**********************************************************************************************************************************************************************************************
Wasanii wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo itakayofanyika hivi karibuni katika Kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Kawe.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo
itakayotolewa kwa wasanii.
Dkt. Kisenge alisema kutokana na tatizo la
magonjwa ya moyo kuwa kubwa Taasisi hiyo imeona ishirikiane na wasanii katika
kuhamasisha jamii ili kuona umuhimu wa kupima magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.
“Katika kufanikisha hili kutakuwa na zoezi la
upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo kwa wasanii katika kliniki yetu ya Kawe
kwa mwezi wa huu wa Desemba na Januari 2024 kila siku za Jumamosi na Jumapili”.
“Baada ya kumalizika kwa zoezi hili kutakuwa na
utaratibu maalumu kwa wasanii ambao hawana bima za afya watakaokuja kutibiwa
katika kliniki yetu watapata punguzo la gharama za matibabu”, alisema Dkt.
Kisenge.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji
wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana aliishukuru Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuona umuhimu wa kupima afya za mioyo ya wasanii
na kuwapa elimu ya jinsi ya kujiepusha na magonjwa hayo bila ya gharama zozote
zile.
“BASATA tutasimamia zoezi hili
la upimaji kwa wasanii wetu ili kila mmoja anufaike na upimaji huu kama
mlivyosikia gharama za matibabu ya magonjwa ya moyo ni kubwa hivyo basi ni
muhimu mkachukuwa hatua za kupima mapema kabla ya kusubiri kuugua”, alisisitiza
Dkt. Mapana.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji Bodi
ya Filamu Tanzania Dkt. Gervas Kasiga alisema upimaji huo ni wa muhimu kwani
utawapa hamasa wasanii ya kupima mioyo yao na kuchukuwa hatua baada ya kupata majibu ya
vipimo hivyo.
“Ninawasihi mtumie vizuri fursa
hii kwa kupima mioyo yenu na kupata elimu ya jinsi ya kujiepuka na magonjwa
haya pia elimu mtakayoipata muitumie kuielimisha jamii inayowazunguka kwani
uwezo wa kufanya hivyo mnao”, alisema Dkt. Gervas.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steven Mongele
ambaye ni mratibu wa zoezi hilo la upimaji aliishukuru Serikali ya awamu ya
sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika tiba ya
moyo nchini jambo linalowafanya wananchi wakiwemo wasanii kufaidika na huduma
za matibabu ya kibingwa.
“Gharama za matibabu ya kibingwa yakiwemo ya moyo ni kubwa lakini
hivi sasa huduma hizi zinapatikana hapa nchini na hakuna haja ya kupeka
wagonjwa nje ya nchi. Jambo la muhimu ni kupima afya zetu mapema na kama
utajigundua unashida utajua jinsi gani utaishi pia tujenge tabia ya kusaidiana tunapoona wenzetu
wanahitai msaada wa fedha za matibabu”, alisema Mongele.
Mongele alisema wataangalia namna ambavyo wasanii walioko mikoani watafikiwa na huduma hiyo ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo bila malipo.
Comments
Post a Comment