Wasanii waishukuru Serikali upimaji moyo Kawe
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Flora
Zacharia akimpima Shinikizo la damu, mapigo ya moyo na kiwango cha oksijeni
mwilini msanii wa muziki kutoka lebo ya WCB Wasafi Zuhura Othman Soud (Zuchu)
alipofika katika Kliniki ya Taasisi hiyo iliyopo Kawe kwaajili ya ufanya uchunguzi
wa magonjwa ya moyo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza na msanii wa muziki kutoka lebo ya WCB Wasafi
Zuhura Othman Soud (Zuchu) mara baada ya kufanya vipimo vya moyo katika Kliniki
ya Taasisi hiyo iliyopo Kawe jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimpatia majibu yake msanii wa muziki kutoka lebo ya WCB
Wasafi Mbwana Yusuph Kilungi (Mbosso) mara baada ya kufanya vipimo vya moyo
katika Kliniki ya Taasisi hiyo iliyopo Kawe jijini Dar es Salaam. Kushoto ni
msanii kutoka lebo ya WCB Wasafi D Voice
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mashirikiso ya
muziki, sanaa, maonesho, maigizo na wanamuziki mara baada ya kufika katika
kliniki ya Taasisi hiyo iliyopo Kawe kwaajili ya kupima moyo.
Na: JKCI
*******************************************************************************************************
Wasanii kutoka lebo ya WCB Wasafi wajitokeza kufanya
uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika Kliniki ya Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Kawe.
Mwitikio kutoka kwa wasanii hao umekuja baada ya kampeni
inayofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupitia kambi maalumu ya
tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwafanyia uchunguzi na matibabu
ya moyo wasanii na wanamichezo nchini kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa
na magonjwa hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
alisema JKCI itaendelea kuihamasisha jamii kupima magonjwa yasiyo ya kuambukiza
yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Wasanii kutoka lebo ya WCB Wasafi ambao ni Zuchu, Mbosso na
D Voice leo wamifika hapa katika kliniki yetu kupima moyo na kuhamasisha wenzao
kuwa na tabia ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwani magonjwa haya
husababisha vifo vingi duniani huku wengine wakipoteza maisha wakiwa na umri
mdogo”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge aliwataka wasanii kuendelea kujitokeza katika
kliniki ya JKCI iliyopo Kawe na Oysterbay kupata elimu juu ya magonjwa ya moyo,
kupimwa afya ya moyo na kupata elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo.
Msanii kutoka lebo ya WCB Mbwana Yusuph Kilungi (Mbosso) amemshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa
fursa hiyo kwa wasanii kuchunguza afya zao kwani wengi wao hawana tabia ya
kufanya uchunguzi wa afya kama hawana dalili za kuumwa.
Mbosso alisema yeye amekuwa mhanga wa magonjwa hayo ya moyo
ambapo huko awali alishakutwa na tatizo hilo na kupatiwa matibabu hivyo kuamini
kuwa amepona.
“Nawashukuru wataalamu wa Taasisi hii, leo nimefika hapa
nimefanyiwa uchunguzi na tatizo langu nililokuwa nalo awali kuonekana bado
lipo, Namshukuru Dkt. Kisenge ameniahidi kuwa tatizo hili ni dogo na
atalisimamia nipate matibabu na kupona kabisa”, alisema Mbosso
Kwa upande wake Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) Dkt. Kedmon Mapana ameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao kuwezesha huduma za uchunguzi
wa magonjwa ya moyo kwa wasanii nchini.
Kipekee nawashukuru marais wa mashirikisho ya sanaa ambao wao
wamejitokeza kwa wingi akiwemo rais wa shirikisho la muziki Tanzania, rais wa
shirikisho la sanaa za ufundi, kaimu katibu wa shirikisho la sanaa za maonesho,
na rais wa shirikisho la filamu Tanzania kujitokeza kwao ni sehemu ya kuwahamasisha
wadau wao kutumia fursa hii vizuri”, alisema Dkt. Mapana
Dkt. Mapana amewashukuru wasanii wakiwemo ma gwiji na nguli
wa muziki Tanzania kama Diamond Platnum kuhamasisha wasanii wenzao kupima afya
na wengine kufika kupima bila ya kuwa na uoga kama ambavyo amefanya Zuchu, D
Voice na Mbosso.
“Kupima afya kabla ya ugonjwa ni muhimu, Rais wetu anataka
sisi wasanii tufanya kazi vizuri tukiwa na afya bora kwani afya yetu ndio mtaji
wetu na sanaa zetu ndio ajira zetu”, alisema Dkt. Mapana
Naye Makamu Mwenyekiti Chama cha Muziki wa Injili Tanzania
Dkt. Catherine Lukindo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu
wa kuwapatia wasanii nafasi ya kupima afya zao.
Dkt. Lukindo amewaomba waimbaji wa nyimbo za injili nao kuwa
mstari wa mbele kujitokeza kupima afya kwani kupitia chama hicho wapo wasanii
waliopoteza maisha yao kutokana na tatizo la shinikizo la juu la damu pamoja na
magonjwa ya moyo.
“Fusra hii tusiichezee mimi binafsi katika familia yangu tumekuwa
wahanga wa magonjwa haya ya moyo, kuna siku kaka yangu alifika Hospitali Tanga
akiwa na maumivu makali ya kifua akaambiwa ana tatizo la moyo na kupewa gari
kukimbizwa hapa JKCI ambapo alipatiwa matibabu na kupona, hivyo tusisubiri hadi
tufikie katika hatua hiyo ndio twende hospitali”, alisema Dkt. Lukindo
Dkt. Lukindo alitoa shukrani zake kwa uongozi wa Taasisi hiyo
kwa kuwapokea wasanii, kuwapa elimu ya magonjwa ya moyo na kuwapa huduma za
matibabu bila ubaguzi.
Comments
Post a Comment