Wasanii watakiwa kuelimisha jamii kujikinga na magonjwa ya moyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akisikiliza mapigo ya moyo ya msanii wa bongo movie na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steven Mengele wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayofanywa na Taasisi hiyo kwaajili ya kuwafanyia uchunguzi na matibabu ya moyo wasanii katika Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe jengo la Mkapa Health jijini Dar es Salaam.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Devotha
Mapunda akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi
(Echocardiography – ECHO) msanii aliyefika katika Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe
jengo la Mkapa Health wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya tiba mkoba ya
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo jijini Dar es Salaam.
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ingrid
Nyabenda akitoa elimu ya lishe kwa wasanii wa bongo movie waliofika katika
Taasisi hiyo Kliniki ya Kawe wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya tiba
mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo jijini Dar es Salaam.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nicholaus Steven akimsomea majibu msanii wa bongo movie Jenipha Kyaka aliyefika katika Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayofanywa na Taasisi hiyo kwaajili ya kuwafanyia uchunguzi na matibabu ya moyo wasanii leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akiwapongeza wasanii kwa kujitokeza kupima afya zao leo
wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan inayofanyika katika kliniki ya JKCI Kawe jengo la Mkapa Health plaza jijini
Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Gervas
Kasiga.
Na: JKCI
***************************************************************************************************************
Wasanii wametakiwa kutumia sanaa kufikisha elimu ya namna ya
kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo katika jamii inayowazunguka.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa kambi maalumu ya siku
mbili ya tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayofanyika katika
Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe jengo la Mkapa Health Plaza jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kisenge alisema kambi hiyo imefanyika kwa ushirikiano na
Bodi ya Filamu Tanzania na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kuwafikishia
huduma za kibingwa wasanii kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi kufikia mwisho wa
mwezi Januari 2025.
“Wasanii wamekuwa kioo katika jamii yetu, tukaona ni wakati
sasa kuwatumia ili waweze kutusaidia kuielimisha jamii namna ya kujikinga na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo kwani magonjwa haya yamekuwa
yakichangia vifo vingi duniani”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema wasanii wanapoyaelewa magonjwa hayo
inasaidia kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia njia mbalimbali za sanaa ikiwemo
maigizo, muziki na sanaa nyinginezo.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu
Tanzania Dkt. Gervas Kasiga alisema limekuwa jambo la kipekee mwaka huu wasanii
kufunga mwaka wakiwa wamefanya uchunguzi wa afya zao na kupata elimu ya namna
ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Dkt. Gervas aliwataka wasanii kutumia fursa hiyo kwa umuhimu
kwani nafasi kama hiyo huwa haijitokezi mara nyingi hivyo pale inapojitokeza
inapaswa kutumiwa vizuri na kwa maslahi binafsi.
“Kupitia upimaji huu unaotolewa kwa wasanii itatusaidia
katika tasnia kujua afya zetu ili tunavyoenda kufanya kazi zetu tuweze
kuzifanya kwa ubora kufikia matarajio yetu na matarajio ya nchi yetu”, alisema
Dkt. Gervas
Naye msanii wa bongo movie na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama
Ongea na Mwanao Steven Mengele amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa hiyo kwa wasanii kupima
afya zao.
“Taifa lenye watu dhaifu linaweza kukosa watu wenye fikra za
kulijenga, lakini taifa lenye watu jarisi uongozwa na watu wenye afya imara
hivyo kupitia fursa hii wasanii tusiipuuze tujitokeze”, alisema Steven
Steven alisema watu wengi wakiwemo wasanii wamekuwa
wakitembea na maradhi bila ya wao kujijua kutokana na kutokuwa na mazoea ya
kufanya uchunguzi wa afya hadi pale changamoto za kiafya zinapojitokeza.
“Tumepata fursa hii kama wasanii tukiwemo wasanii wa bongo
flavor, bongo movie, washereheshaji (MC), wanamichezo mbalimbali kupima afya
zetu, Tunamshukuru Rais Dkt. Samia ametusaidia tufunge mwaka 2024 tukiwa na
afya bora bila ya kutumia fedha kupima afya zetu”, alisema Steven
Akitoa shukrani zake msanii wa bongo movie Devotha Mbaga
amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwathamini wasanii na kuwapa fursa ya kupima
afya ya moyo bila gharama.
“Moyo ndio injini ya mwili wa binadamu hivyo ukipata shida ya
moyo lazima mwili wote utakuwa dhoofu ndio maana nilipoona nafasi hii nilifika
mapema kufanya uchunguzi na kupata elimu ya namna nitaweza kujikinga na
magonjwa ya moyo”, alisema Devotha
Devotha alisema huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo zinaweza
kumfanya mgonjwa asijione kama yupo hospitali kwani wataalamu katika maeneo
yote wamejipanga kutoa huduma na kumfanya mgonjwa ajisikie huru.
“Toka nifiki hapa nimepata huduma zote bure na baada ya
vipimo kuonyesha kuwa na changamoto kidogo nimepewa dawa bila gharama,
nawashukuru sana”, alisema Devotha
Comments
Post a Comment