JKCI yafungua Kliniki Oysterbay
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza na mwananchi aliyefika JKCI Kliniki ya Oysterbay
iliyopo Oyster Plaza Haile Salassie barabara ya Ali Bin Said leo wakati kliniki
hiyo ilivyoanza kutoa huduma.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anord
Mushi akimpima shinikizo la damu (BP) mwananchi aliyefika JKCI Kliniki ya Oysterbay
iliyopo Oyster Plaza Haile Salassie barabara ya Ali Bin Said leo wakati kliniki
hiyo ilivyoanza kutoa huduma.
Mtunza kumbukumbu za afya (DPO) wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Mercy Msuya akimpa maelekezo mwananchi aliyefika JKCI Kliniki ya
Oysterbay iliyopo Oyster Plaza Haile Salassie barabara ya Ali Bin Said leo
wakati kliniki hiyo ilivyoanza kutoa huduma.
Na: JKCI
**************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefungua tawi jipya
kuwapa wananchi nafasi kuwa karibu na huduma ili pale wanapopata changamoto za
kiafya wasichukue muda mrefu kufuata huduma zilipo.
Tawi hilo lililopo katika jengo la Oyster Plaza Haile
Salassie barabara ya Ali Bin Said limeanza kutoa huduma bobezi za moyo leo
lengo likiwa kuwapa fursa wananchi kupata huduma katika maeneo tofauti na ilipo
taasisi hiyo na kupunguza msongamano uliopo katika makao makuu ya taasisi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
alisema JKCI imekuwa ikiwafikia wananchi walipo kwa kuwafuata mikoani na kuwapa
huduma bobezi za uchunguzi na matibabu ya moyo.
“Tumekuwa tukiwafuata wananchi mikoani kuwapa huduma sasa
tumeamua kuanzisha matawi ya Taasisi, hii pia ni sehemu ya kuwafuata wananchi
mahali walipo kwani hapa tulipo leo tunawapa nafasi wananchi wa eneo hili
kupata huduma kwa karibu lakini pia hata wale wanaotoka mbali tunawapa nafasi
ya kupunguza msongamano uliopo makao makuu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema JKCI pia inaendelea kuyafikia makundi ya
watu mbalimbali kuwapa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo ili makundi yote
yanayofikiwa yaweze kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao na kuwa na tabia za
kuchunguza afya zao mara kwa mara.
“Tumekuwa tukiwafikia watu tofauti kuwafanyia uchunguzi wa
magonjwa ya moyo, kipindi hiki cha kufunga mwaka tunatoa huduma kwa wasanii, na
wanamichezo kila jumamosi na jumapili katika kliniki yetu ya Kawe, wanahabari
tulishawapa huduma hii huko nyuma ila tutakuja kuwarudia tena”
Aidha Dkt. Kisenge ametoa wito kwa wasanii na wanamichezo
kuendelea kujitokeza kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwani kinga ni bora
kuliko tiba na kama watagundulika mapema watakuwa kwenye nafasi ya kutibiwa
magonjwa hayo mapema na kupona.
Kwa upande wake mwananchi aliyepatiwa huduma katika kliniki
ya JKCI iliyopo Oyster Plaza Haile Salassie ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuwa
na maono ya kusogeza huduma karibu na jamii na kuipa jamii ari ya kufanya
uchunguzi wa magonjwa ya moyo.
Mwananchi huyo ambaye hakutaka jina lake lifahamike alisema
huduma za afya zikiwa karibu na jamii zinatoa motisha kwa jamii kufika
hospitali na kufanya uchunguzi wa afya hivyo kupunguza matumizi ya dawa yasiyo
sahihi.
“Mara nyingi tumekuwa tukipata hali za maumivu ama kuumwa
kichwa, mafua, kikohozi, kifua tunaenda duka la dawa kununua dawa tu bila ya
kufanya uchunguzi lakini kama tutakuwa karibu na Hospitali itatusaidia kwenda
kupima kwanza na kupata ushauri wa daktari kabla ya kununua dawa”, alisema.
Naye msimamizi wa kliniki hiyo Nyanjura Nyaruga alisema
kliniki hiyo imeanza kwa kuwa na mwitikio mkubwa wa watu waliofika kupata
huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Nyanjura ambaye pia ni Afisa Muuguzi mbobezi wa magonjwa ya
moyo alisema katika kliniki hiyo wanatoa huduma za kliniki ya moyo, kliniki ya
mishipa ya damu, kliniki ya magonjwa ya moyo kwa watoto, huduma za maabara,
huduma za mazoezi kwa wagonjwa wa moyo na huduma za dharura.
“Wananchi wasisite kufika katika kliniki yetu hii kwani
tumejipanga kufikisha huduma bora kwenu na tutakuwa tukitoa huduma zetu kwa
muda wa masaa ishirini na nne”, alisema Nyanjura
Comments
Post a Comment