DC Handeni aishukuru JKCI kwa kugusa mioyo ya wananchi
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Albart Msando akizungumza na
wananchi wa Wilaya hiyo leo wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanywa na wataalamu wa afya kutoka Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kufanyika kwa siku mbili katika Hospitali ya
Wilaya ya Handeni iliyopo mkoani Tanga.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Albart Msando akipima
shinikizo la damu leo baada ya ufunguzi wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanywa na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kufanyika kwa siku mbili katika Hospitali ya
Wilaya ya Handeni iliyopo mkoani Tanga.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Eva Wakuganda akielezea namna taasisi hiyo imejipanga kuwafikia wananchi wote leo wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanyika kwa siku mbili katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni iliyopo mkoani Tanga.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Marafiki wa Maendeleo Handeni
(MMAHA) Mariam Mwanilwa akielezea namna taasisi hiyo imejipanga kuisaidia jamii
kupata huduma za afya wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanywa na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa siku mbili katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni
iliyopo mkoani Tanga.
Daktari wa huduma za dharura kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Nicole Kinyawa akizungumza na mkazi wa Handeni mara baada ya
kufanya vipimo vya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya
Handeni iliyopo mkoani Tanga. Kulia ni Dkt. Philipina Marandu wa Hospitali ya
Wilaya ya Handeni.
Na: JKCI
********************************************************************************************************************
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa
kuendelea kutoa huduma na kugusa maisha ya wananchi wanaohitaji huduma za
kibingwa zikiwemo huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe.
Albart Msando wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya siku nne ya Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanywa na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Wilayani Handeni.
“Kwa niaba ya wananchi wa Handeni pamoja na Taasisi ya
Marafiki wa Maendeleo Handeni (MMAHA) waliowezesha zoezi hili, tunawashukuru
sana wataalamu kutoka JKCI kwa kuwezesha matibabu haya kufanyika katika wilaya
yetu, kazi mnayoifanya ni kubwa sana na mmekuwa mkiifanya kwa kujitoa bila
kuchoka”, alisema Mhe. Msando
Mhe. Msando alisema ofisini kwake mara nyingi wanapokea watu
wanaofika kuomba msaada wa matibabu, ambapo ofisi huwapa barua ambayo inawapasa
wapite katika mnyororo mrefu hadi waweze kufikia hatua ya mwisho ya kupata
msamaha wa matibabu hatua ambazo huchukua muda mrefu.
“Katika Wilaya yetu ya Handeni kama wewe ni mzima unaweza
usijue changamoto kubwa walizonazo wananchi inapokuja katika masuala ya
ugonjwa, afya uliyonayo ni zawadi ambayo Mungu ametujalia lakini wapo watu
ambao wanateseka sana katika Wilaya yetu kutokana na magonjwa mbalimbali”,
“Wapo wananchi wetu wanatoka Handeni wanaenda Dar es Salaam
kwaajili ya matibabu na huko hawana ndugu, hivyo kuteseka lakini kupitia ujio
wenu hapa tunarahisisha upatikanaji wa huduma hizi za kibingwa”, alisema Mhe.
Msando
Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Eva Wakuganda alisema timu ya wataalamu
bingwa wa moyo kwa watoto na watu wazima ikiwa na vifaa tiba vya kisasa imeweka
kambi ya siku nne mkoani Handeni kuwafanyia uchunguzi wananchi wa Wilaya hiyo.
Dkt. Eva alisema mbali na kutoa huduma za uchunguzi wa
magonjwa ya moyo wale wote watakaokutwa na magonjwa ya moyo, shinikizo la juu
la damu (BP) na sukari watapatiwa dawa bila gharama.
“JKCI imekuwa ikiona wagonjwa mbalimbali wa moyo na wakati
mwingine tumekuwa tukiwaona wakiwa wamechelewa hivyo ikaanzisha kambi maalumu
ili tuweze kuwagundua wagonjwa wa moyo mapema na kuwapa matibabu”, alisema Dkt.
Eva
Dkt. Eva alisema JKCI imekuwa ikitoa huduma za uchunguzi wa
magonjwa ya moyo kwa wananchi katika ngazi ya mikoa na sasa hivi imeshuka
katika ngazi ya wilaya na hapo baadaye itaweka miundombinu ya kuwafikia
wananchi katika ngazi ya vitongoji.
“Hatua hizi tunazozifanya ni katika kuona namna tatizo la
moyo jinsi lilivyo, hali za wagonjwa wa moyo katika ngazo hizo na namna ambavyo
tutaweza kuwasaidia kwa wakati”, alisema Dkt. Eva
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni Magreth
Kilo alitoa shukrani za dhati kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kwa wananchi wakiwemo wananchi wa Handeni
“Wananchi wengi wamekuwa wakifika katika Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya kuomba msaada wa matibabu na hasa matibabu ya moyo kwa watoto na watu
wazima, ujio wenu unaenda kutusaidia kupunguza changamoto hii ya upatikanaji wa
matibabu”, alisema Magreth
Magreth alisema wataalamu wa JKCI wanaweza kuona wanafanya
jambo dogo katika kutoa huduma hizo lakini kwa wananchi wa Handeni wamefanya
jambo kubwa linalogusa mioyo ya wana Handeni wengi.
Naye mwananchi aliyepata huduma katika kambi hiyo Idd Hassan
ameushukuru uongozi wa Wilaya ya Handeni kwa kuwezesha wataalamu wa JKCI kufika
katika wilaya hiyo na kutoa huduma bila gharama kwa wananchi wa Handeni.
“Tunawashukuru sana viongozi wetu, leo tumepata huduma za
kuchunguza mioyo yetu kwakweli tumefurahi sana”, alisema Idd
Comments
Post a Comment