411 wapimwa moyo Halmashauri ya Handeni Mjini
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya ya Handeni Dkt. Laurence
Meshilieki akizungumza na wananchi waliojitokeza kufanya uchunguzi na matibabu
ya magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanywa na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika hospitali hiyo iliyopo mkoani Tanga.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Mlagwa Yango akimpatia dawa mwananchi wa Handeni aliyepata
huduma za uchuguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanyika katika Hospitali ya
Wilaya ya Handeni iliyopo mkoani Tanga. Kushoto ni daktari wa Hospitali ya
Wilaya ya Handeni Antony Mwale
Afisa Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Makrina
Komba akimpima wingi wa sukari kwenye damu mwananchi aliyefika katika Hospitali
ya Wilaya ya Handeni wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Wilaya
Handeni.
Wananchi wa Wilaya ya Handeni wakisoma vipeperushi
vinavyoelezea lishe bora wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni.
Wananchi wa Wilaya ya Handeni wakiendelea kupata huduma za
vipimo vya awali wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Wilaya ya
Handeni.
Na: JKCI
Watu 411 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya
moyo wakati wa kambi maalumu iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya
Handeni Mjini na kumalizika jana.
Uchunguzi huo umefanyika katika kambi maalumu ya siku mbili
ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka
Hospitali ya Wilaya ya Handeni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Handeni Daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto na mratibu wa kambi hiyo kutoka Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda alisema
katika watu 411 waliofanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo watu wazima walikuwa
356 na watoto 55.
“Upande wa watu wazima tumewakuta watu 164 na matatizo
mbalimbali ya moyo yakiongoza matatizo ya shinikizo la juu la damu na upande wa
watoto tumewakuta watoto 18 na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yakiwemo matundu
na mishipa ya damu ya moyo kuziba”, alisema Dkt. Eva
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma
katika kambi hiyo wameishukuru Taasisi ya Maendeleo Handeni (MMAHA) kwa
kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kufikisha huduma kwani
wengi wao imekuwa mara ya kwanza kuchunguza mioyo yao.
Aisha Athuman alisema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo
la juu la damu na kuambiwa na wataalamu kufanya uchunguzi wa moyo wake, kupitia
kambi hiyo ameweza kuona jinsi moyo wake ulivyo.
“Kwakweli nitoe shukrani zangu za dhati kwa taasisi hizi
mbili kuungana na kufikisha huduma kwetu wananchi wa Handeni, leo nimefanyiwa
vipimo vya moyo na baada ya vipimo nimepewa dawa bure”, alisema Aisha
Kwa upande wake daktari kutoka Hospitali ya Wilaya ya Handeni
Fatuma Ridhiwani amewashukuru wataalamu wa JKCI kwakuwa na ushirikiano na kutoa
ujuzi kwa wataalamu wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni wa namna ya kuwatambua
wagonjwa wa moyo.
Dkt. Fatuma alisema kupitia kambi hiyo ameweza kujifunza vitu
vingi ambayo ataenda kuvitumia na kuifanya fani yake kukua tofauti na
alivyokuwa awali.
“Kupitia wataalamu hawa najiona naenda kuwa marketable, kwani
nitaenda kutumia ujuzi nilioupata hapa kwa wagonjwa wanaofika katika Hospitali
yetu”, alisema Dkt. Fatuma
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Marafiki wa
Maendeleo Handeni (MMAHA) Maria Mwanilwa alisema Taasisi hiyo imezindua wa wiki
ya kutoa huduma za kijamii kwa wananchi wa Halmashauri ya Handeni mjini na
Handeni vijijini.
Mariam alisema moja ya huduma inayotoa ni huduma za afya kwa wananchi
wa wiliaya ya Handeni mjini kwa siku mbili na wananchi wa Handeni vijijini kwa
siku mbili kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI).
“Leo tunavyomaliza kutoa huduma hizi za uchunguzi na matibabu
ya magonjwa ya moyo hapa Handeni mjini, kesho tutakuwa katika Halmashauri ya
Wilaya ya Handeni vijijini kule Mkata ili wananchi wa huko nao waweze kupata
huduma hizi za kibingwa”, alisema Mariam
Comments
Post a Comment