Atakayebainika kuomba au kupokea rushwa kwa wagonjwa atachukuliwa hatua kali za kinidhamu

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi hiyo (hawapo pichani) wakati wa kikao cha wafanyakazi cha kujadili utendaji kazi kwa mwaka 2021 kilichofanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utawala na Rasilimali watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ghati Chacha akielezea mafanikio na changamoto za Kurugenzi hiyo wakati wa kikao cha wafanyakazi cha kujadili utendaji kazi kwa mwaka 2021 kilichofanyika jana Jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia majadiliano yaliyokuwa yanaendelea wakati wa kikao cha wafanyakazi cha kujadili utendaji kazi kwa mwaka 2021 kilichofanyika jana Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Idara ya watoto wenye magonjwa ya moyo na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) Sulende Kubhoja akitoa maoni yake wakati wa kikao cha wafanyakazi cha kujadili utendaji kazi wa mwaka 2021 kilichofanyika jana Jijini Dar es Salaam.

Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Joshua Ogutu akitoa maoni yake wakati wa kikao cha wafanyakazi cha kujadili utendaji kazi wa mwaka 2021 kilichofanyika jana Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimkabidhi fedha taslim shilingi 500,000/= Askari wa Kampuni ya Ulinzi ya Ng’e anayelinda katika Taasisi hiyo Aisha Twalibu ikiwa ni zawadi ya uaminifu aliouonesha baada kuokota begi la ndugu wa mgonjwa lililokuwa na zaidi ya Tshs.milioni 10 na kumkabidhi muhusika baada ya kugundua kuwa amelipoteza na kulikuta kwa mlinzi huyo. Makabidhiano hayo yamefanyika katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika jana Jijini Dar es Salaam.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kujiepusha na mazingira yatakayowapelekea kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa kwa kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi. 

Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam. 

Prof. Janabi alisema iwapo mfanyakazi wa Taasisi hiyo ataomba na kupokea rushwa atajulikana hiyo ni kutokana na kuwepo kwa namba za simu za kutoa maoni na malalamiko zilizowekwa kwa ajili ya wananchi ambazo zimebandikwa katika maeneo mbalimbali ya Taasisi hiyo.

 “Usifikirie kuwa utakapoomba na kupokea rushwa hautajulikana hata kama utafanya jambo hilo kwa siri kumbuka hela za mgonjwa zinachangwa na ndugu wengi hivyo basi yule aliyekupa rushwa ili apate huduma naye pia ataenda kuwajulisha ndugu zake kuwa nimetoa hela na hivyo kulifanya jambo hilo kutokuwa la siri tena”, alisema Prof. Janabi. 

Mkurugenzi huyo Mtendaji pia aliwataka wafanyakazi hao kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao kwani mafanikio ya Taasisi hiyo yanatokana na wafanyakazi wa kada zote waliopo katika Taasisi hiyo. 

“Kama una maoni au changamoto katika eneo lako la kazi mjulishe kiongozi wako ili ayafikishe katika vikao vya menejimenti na kupatiwa ufumbuzi ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma tunazozitoa kwa wananchi”, alisisitiza Prof. Janabi.

 Aidha Prof. Janabi aliwasisitiza wafanyakazi ambao hawajachanja chanjo ya ugonjwa wa UVIKO – 19 kuchanja kwani chanjo ziko za kutosha na kusema kuwa ingawa chanjo ni hiari, ni muhimu kwao wakachanja hii ni kutokana na mazingira wanayofanya kazi ambayo yanawafanya wao kuwa rahisi kupata maambukizi ya ugonjwa huo kutoka kwa wagonjwa wanaowahudumia. 

Akitoa maoni yake katika mkutano huo Mkuu wa Idara ya magonjwa ya Moyo kwa watoto Dkt. Sulende Kubhoja alisema mafunzo ya huduma kwa mteja yanahitajika kutolewa mara kwa mara kwa wafayakazi kwani jinsi utakavyompokea mtu na kumsaidia ndivyo mgonjwa atakavyoridhika kwa huduma aliyoipata. 

Katika kikao hicho pia Prof. Mohamed Janabi alikabidhi fedha taslim Tshs. 500,000/= kwa Askari wa Kampuni ya Ulinzi ya Ng’e anayelinda katika Taasisi hiyo Aisha Twalibu ikiwa ni zawadi ya uaminifu aliouonesha baada ya kuokota begi la ndugu wa mgonjwa lililokuwa na zaidi ya Tshs.milioni 10 na kumkabidhi muhusika baada ya kugundua kuwa amelipoteza na kulikuta kwa mlinzi huyo. 

Prof. Janabi aliwasihi wafanyakazi wengine kuiga mfano wa uaminifu aliouonesha mlinzi huyo. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Aisha alisema wiki iliyopita majira ya usiku wakati anaenda kuwasha taa katika eneo lake la lindo alilikuta begi hilo likiwa limesahaulika mahali wanapokaa wagonjwa wanaosubiri kufanyiwa vipimo vya moyo. 

“Nililichukuwa begi hilo na kumjulisha mlinzi mwenzangu baada ya kulifungua ndani kulikuwa na fedha za kitanzania, dola za kimarekani pamoja na simu ya mkononi. Nilibaki na begi hilo nikiwasubiri wahusika. 

Baada ya muda kupita walifika na kuuliza kama nililiona begi. Tuliwahoji maswali kadhaa na kuridhika na majibu yao niliwakabidhi, walilikagua na kuona kuwa liko sawa, walishukuru wakaondoka”, alisema Aisha. 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari