Watoa msaada kwa watoto wenye magonjwa ya moyo
Msimamizi
wa wodi ya watoto ambaye pia ni afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Tedy Tarimo akimshukuru Mdau ambaye ana tatizo la moyo Enelisa Songa
(kushoto) kwa kujitoa kwake kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya
moyo wakati wa kusherehekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa Jana katika
Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam
Rafiki wa mdau ambaye ana tatizo la moyo Mercy Kobelo akimpatia zawadi mbalimbali mama ambaye mtoto wake amelazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya matibabu ya moyo Rauhia Rajabu wakati wa kusherehekea kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa ya rafiki yake Enelisa Songa Jana katika Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam
Mdau
ambaye ana tatizo la moyo Enelisa Songa akikata keki kwa kushirikiana na baadhi
ya watoto waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya
matibabu ya moyo wakati wa kusherehekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa Jana katika Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam
Jamii imeombwa iendelee kuwasaidia watoto
wenye magonjwa ya moyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo kutoa msaada wa
mahitaji muhimu kwani watoto hao wanatoka katika maeneo tofauti ya Tanzania na
kukaa hospitali muda mrefu hivyo kupata changamoto ya mahitaji yao ya muhimu
Hayo yamesemwa na Msimamizi wa wodi ya watoto
ambaye pia ni afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKIC) Tedy
Tarimo wakati akipokea zawadi mbalimbali kutoka kwa mdau ambaye ana tatizo la
moyo alipofika katika Taasisi hiyo kusherehekea siku yake ya kuzaliwa pamoja na
watoto waliolazwa JKCI Jana Jijini Dar es Salaam
“Tunamshukuru sana Enelisa pamoja na marafiki
zake kwa zawadi walizoleta kwa ajili ya watoto pamoja na mama zao kwa sababu
haya ni mahitaji ambayo wagonjwa wetu wanayahitaji, hakika leo ni furaha kwa
wagonjwa wetu kupitia zawadi hizi”,
“Upendo uliounesha unatuunganisha kuanzia sasa
wewe ni mwenzetu, tunakuombea kwa Mungu changamoto ya tatizo la moyo ulilokuwa
nalo liweze kupatiwa matibabu na kuweza kupona kabisa”, alisema Tedy
Aidha Tedy ameiomba jamii kuwafanyia uchunguzi
wa afya watoto chini ya miaka 18 mara kwa mara hii itasaidia kugundua kama
mtoto ana sumbuliwa na maradhi mapema na kupatiwa huduma za tiba kwa wakati.
“Utakapomfanyia uchunguzi wa afya mwanao na
kugundulika na tatizo la moyo ni vyema ukamfikisha Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete ili aweze kupatiwa matibabu stahiki na kwa wakati kwani mabingwa wa
moyo wapo JKCI”, alisema Tedy
Kwa upande wake mdau ambaye ana tatizo la moyo
Enelisa Songa alisema katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa aliona ni vyema
afike Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ikiwa ni sehemu ya kutoa shukrani zake kwa
watoto wenye matatizo ya moyo kwasababu yeye pia ni mhanga wa ugonjwa huu wa moyo.
“Nimeleta mahitaji mbalimbali ambayo
nimejaliwa na mwenyezi Mungu yatakayowasaidia watoto pamoja na mama zao kwani
humu wodini kuna wagonjwa ambao wametoka maeneo mbalimbali ikiwemo mikoani na naamini
wanahitaji mahitaji haya”,
“Leo nimesindikizwa na marafiki zangu
ambao baada ya kusikia kuwa nakuja kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa
hawakubaki nyuma nao wakanichangia hivyo mafanikio haya ni pamoja na wao”,
alisema Enelisa.
Naye mama mzazi wa mdau ambaye ana
tatizo la moyo Nuru Kasaki alikiri kushangazwa na kitendo alichokifanya mtoto
wake cha kujitoa kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo kwani hakufikiria
kuwa ipo siku mwanaye atafanya kitendo alichokifanya katika kusherehekea siku
yake ya kuzaliwa.
“Mwanangu alinipigia simu na kuniomba
leo nimsindikize JKCI, nilijua tunakuja kwa ajili ya kliniki zake za kawaida za
moyo, kumbe amekuja kunifanyia surprise
ya kutoa zawadi kwa watoto, namshukuru Mungu naimani mwanangu atapona”, alisema
Nuru
Comments
Post a Comment