TPDC Marathon 2026 kuokoa maisha ya watoto 100 wenye magonjwa ya moyo

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Derick Moshi wakati wa uzinduzi wa TPDC Marathon uliofanyika leo katika hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa TPDC Marathon kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI leo katika hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Derick Moshi akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa TPDC Marathon itakayofanyika tarehe 29 Novemba, 2026 katika viwanja vya Polisi Officers Mess iliyopo Masaki kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Derick Moshi, baadhi ya wafanyakazi wa JKCI na Global Medicare wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa TPDC Marathon uliofanyika leo katika hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Derick Moshi na baadhi ya wafanyakazi wa TPDC wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa TPDC Marathon uliofanyika leo katika hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam.

Na JKCI

****************************************************************************************************

Watoto 100 wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuchangiwa gharama za matibabu kupitia marathon iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) msimu wa tatu inayotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.

Marathon hiyo yenye kauli mbiu “Hatua Yako Inaokoa Maisha” ni ishara ya mshikamano wa jamii katika kulinda na kuokoa maisha ya watoto wanaotoka katika familia zisizokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu ya moyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa marathon hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema zaidi ya watoto 1,500 wenye magonjwa ya moyo wako katika foleni ya kusubiria huduma za upasuaji wa moyo huku wengi wao wakitoka katika familia zenye uwezo mdogo wa kumudu gharama za matibabu.

Dkt. Kisenge alisema hali hiyo imeifanya taasisi hiyo kuitegemea Serikali na wadau mbalimbali ili kuhakikisha watoto wenye matatizo ya moyo wanapata matibabu kwa wakati na kuokoa maisha yao.

“Tunapokea watoto wengi wenye matatizo ya moyo. Takwimu zinaonesha kuwa kati ya watoto 100 wanaozaliwa, takribani wawili huzaliwa wakiwa na matatizo ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt Kisenge alisema Serikali imeendelea kutoa msaada kwa watoto wenye magonjwa ya moyo hasa kwa kuzingatia kuwa sehemu kubwa ya wagonjwa hao hutoka katika familia zenye uwezo mdogo wa kifedha na hivyo kushindwa kumudu gharama za matibabu.

“Tunaishukuru TPDC kwa kuendelea kushiriki katika kusaidia gharama zamatibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo kupitia mpango wake wa kuchangisha fedha, mwaka 2022 TPDC ilichangia shilingi milioni 100 kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo, huku mwaka 2025 ikichangia shilingi milioni 50”,

“Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki mbio hizi. Zaidi ya kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo, kushiriki mbio hizi ni sehemu ya kufanya mazoezi, kujenga afya bora na hatimaye kuokoa maisha”, alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Derick Moshi alisema afya ni miongoni mwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya kampuni hiyo, hivyo ushiriki wao katika kusaidia sekta ya afya ni sehemu ya wajibu wao kwa jamii.

“Kaulimbiu ya TPDC marathon msimu wa tatu inatukumbusha kuchukua hatua, kuunganisha nguvu na kutumia nafasi tulizonazo kujali maisha ya wengine”, alisema Moshi.

Moshi alisema mbio hizo zitakuwa jukwaa la kuunganisha nguvu ya michezo, dhamira ya kijamii na ushiriki wa wadau mbalimbali katika kuchangisha fedha za kuboresha huduma za matibabu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo.

“Tunathamini kuona watu wanakuwa na afya njema na wanaishi, jambo la afya linalowezekana kufanyika leo lifanyike leo lisubiri kesho”, alisema Moshi.

Moshi alisema ushiriki wa TPDC katika kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo si jambo jipya bali ni mwendelezo wa jitihada za kampuni hiyo za kuirudishia jamii kupitia shughuli za uwajibikaji kwa jamii.

Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mussa Mussa aliwataka waandishi wa habari kutumia nafasi yao kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu TPDC Marathon 2026 ili kuongeza ushiriki wa wananchi na hatimaye kufanikisha lengo la kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo.

Mussa alisema kushiriki katika mbio hizo kuna faida mbili ikiwemo kuchangia katika kuokoa maisha ya watoto wenye matatizo ya moyo na kuimarisha afya za washiriki wenyewe.

“Naipongeza TPDC kwa kuanzisha na kuendeleza mpango huo, Wizara ya Nishati inafurahia kuona kampuni hii ikishiriki katika jambo lenye manufaa kwa jamii, tunatamani mpango huu uwe uendelevu”, alisema Mussa.

Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma