JKCI kuanzisha huduma za moyo Hospitali ya Kitete Tabora
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
akizungumza na watumishi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora - Kitete
wakati wa kikao cha kujadili kuhusu ushirikiano kati ya JKCI na Hospitali ya
Kitete leo katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo
cha Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Thadei Kavishe akiwaelezea
namna maabara ya kisasa inayotomia roboti inavyofanya kazi watumishi kutoka Hospitali
ya Rufaa Mkoa wa Tabora – Kitete walipotembelea maabara hiyo kwaajili ya
kujifunza.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Mganga Mfawidhi
wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora - Kitete Dkt. Joachim Eyembe pamoja na
watumishi kutoka JKCI na Kitete wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika
kwa kikao cha kujadili kuhusu ushirikiano kati ya JKCI na Hospitali ya Kitete leo
katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya
wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wataalam wa afya kutoka
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora - Kitete wakisikiliza wakati wa kikao cha kujadili
kuhusu ushirikiano kati ya JKCI na Hospitali ya Kitete kilichofanyika leo
katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Afisa uhakiki na
udhibiti Ubora kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Adelphina
Ncheye akiwaonesha maeneo ya taasisi hiyo wataalam wa afya kutoka Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Tabora - Kitete kabla ya kikao cha kujadili kuhusu ushirikiano
kati ya JKCI na Hospitali ya Kitete kilichofanyika leo katika ukumbi wa Taasisi
hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Na JKCI
********************************************************************************************************
Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora - Kitete zimeingia
makubaliano kuanzisha huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo
katika hospitali hiyo hatua inayolenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na
wananchi wa Tabora na mikoa jirani.
Akizungumza
wakati wa makubaliano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema mpango wa ushirikiano kati JKCI na
Kitete unakuja baada ya wataalamu wa Hospitali ya Kitete kufanya ziara ya
mafunzo JKCI na kujadili kuhusu namna ambavyo wanaweza kushirikiana kufikisha
huduma za bingwa moyo mkoani Tabora.
Dkt. Kisenge
alisema katika hatua za awali JKCI itawajengea uwezo wataalamu wa afya wa
Kitete kupitia mafunzo maalum huku ikishirikiana na hospitali hiyo kuboresha
mazingira ya kutolea huduma za moyo kama ilivyo kwenye matawi mengine ya JKCI.
“Kama Taasisi tunataka
kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo karibu na wananchi.
Tutawajengeeni uwezo na kuboresha mazingira ya huduma ili wananchi wapate
huduma bora bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufata huduma hizo hapa
JKCI”, alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt.
Kisenge alisema JKCI itawekeza katika huduma kwa wateja ili kuhakikisha
wananchi wa Tabora na mikoa ya jirani ikiwemo Mwanza, Shinyanga na Singida
wanapata huduma bora za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Kwa upande
wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora - Kitete Dkt.
Joachim Eyembe aliushukuru uongozi wa JKCI kwa kukubali kushirikiana nao na
kuahidi kuendeleza ushirikiano huo katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata
huduma za matibabu ya moyo kwa urahisi.
“Naomba nikuhakikishie
kuwa tutashirikiana kwa karibu na Taasisi hii kuhakikisha huduma bingwa za matibabu
ya moyo zinapatikana mkoani Tabora kwa wakati kupitia Hospitali yetu ya Kitete
ili kusaidia kuokoa maisha ya watanzania”, alisema Dkt. Eyembe.
Naye Afisa
uhakiki na udhibiti Ubora kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Adelphina Ncheye alisema pamoja na makubaliano hayo wataalam hao pia wamefanya
ziara katika maeneo mbali mbali ya taasisi hiyo, hivyo kupata fursa ya
kujifunza mifumo ya JKCI katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa hususan huduma
kwa mteja na ubora wa huduma.
Ushirikiano kati ya JKCI na
Hospitali ya Kitete unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za moyo kwa
wananchi wa Tabora na mikoa ya jirani, huku ukiimarisha uwezo wa wataalamu wa
afya kutoa huduma bora na za kisasa.





Comments
Post a Comment