Mabunge wanawake wa ukanda wa maziwa makuu wananufaika na huduma za JKCI.

Mabunge wanawake wa Ukanda wa
Maziwa Makuu (WPC) wamenufaika na huduma za uchunguzi wa afya na elimu kuhusu magonjwa
yasiyoambukiza zinazotolewa na watalaamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete
(JKCI) katika mkutano unaowakutanisha wawakilishi kutoka mataifa 12 ukanda huo.
Huduma
hizo zinatolewa katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere
(JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam ambapo washiriki wanapata fursa ya
kupimwa shinikizo la damu, kuchunguzwa mfumo wa umeme wa moyo (ECG) ECG pamoja
na kupima uwiano wa uzito kwa urefu.
Akizungumza
wakati wa mkutano huo daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Moses Manumbu alisema uchunguzi wa afya mara kwa mara ni
muhimu katika kubaini mapema vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo
magonjwa ya moyo ili kujikinga na kupata matibabu kwa wakati.
“Ni
muhimu kila mmoja kuwa na utaratibu wa kupima afya yake hata kama hajisikii
kuumwa kwani baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu
yanaweza kutokuwa na dalili za wazi katika hatua za awali hivyo kwa kufanya
uchunguzi wa mara kwa mara tunaweza kubaini vihatarishi na kuchukua hatua
mapema,” alisema Dkt. Manumbu
Kwa
upande wake mratibu wa Utalii Tiba wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jalack
Milinga alisema ushiriki wa JKCI katika mkutano huo ni sehemu ya juhudi za kufikisha
huduma za kibingwa na bobezi za matibabu ya moyo katika mataifa mbalimbali ya
Afrika ili kuhamasisha umuhimu wa kujali afya.
“JKCI
ni taasisi pekee katika ukanda wa Afrika mashariki ambayo inaongoza kwa kutoa
huduma bora za moyo hivyo kupitia mkutano huu tumepata fursa ya kuwafikia
wabunge wanawake ambao tumewaongezea uelewa wa matumizi ya tekinologia za
kisasa katika kutibu moyo,” alisema Jalack.
Mmoja
wa washiriki wa mkutano huo Mery Kizota kutoka Dodoma alishukuru JKCI kwa
kuendelea kujali afya, kutoa huduma za uchunguzi na elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza
kwani inawasaidia kupata uelewa na umuhimu wa kufuatilia afya.
“Nimepata
nafasi ya kufahamu zaidi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, vihatarishi vyake na
umuhimu wa kupima afya yangu mara kwa mara nitazingatia na kuchukua hatua”,
alisema Mery.


Comments
Post a Comment