Hakikisheni huduma za matibabu ya moyo za kibingwa zinawafikia wananchi walioko vijijini – Mhe. Nyongo
Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii imeitaka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuhakikisha huduma za matibabu ya moyo za kibingwa wanazozitoa zinawafikia wananchi walioko vijijini.
Agizo
hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo wakati
akizungumza na menejimenti ya Taasisi hiyo mara baada ya kumaliza ziara ya
kukagua matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kama zinatumika ipasavyo pamoja na
kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Mhe.
Nyongo ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki alisema kamati yake imeridhishwa na huduma zinazotolewa na Taasisi
hiyo na kuishukuru Serikali kwa kuanzisha kituo hicho kinachotoa huduma za
kimataifa ambacho kimekuwa mkombozi na kuwasaidia watu wengi wakiwemo watanzania na wasio watanzania.
Alisema
huko vijijini kuna watu wakiwemo watoto wanamatatizo ya moyo ni vyema nao
wakapata huduma za matibabu hayo ambazo
hivi sasa zinapatikana hapa nchini. Pia wananchi waelimishwe kuhusu magonjwa
hayo na jinsi gani wanaweza kutibiwa kwa
wale ambao wanamatatizo na kwa wale ambao hawana matatizo waelekezwe jinsi ya kuyaepuka.
“Katika
ripoti yenu mmesema mmewafundisha madaktari 45 wa watoto kutoka Hospitali za
kanda jinsi ya kuwatambua watoto wenye matatizo ya moyo ni vyema sasa
mkawafundisha madaktari wa Hospitali za mikoa na wilaya ili nao waweze
kuwatambua wagonjwa wa moyo mapema ambao watapata huduma za matibabu kwa wakati kwani hivi sasa huduma hizo zinapatikana hapa
nchini”, alisema Mhe. Nyongo.
“Pia
muwe na vituo vingine vya JKCI katika Hospitali za kanda na mikoa kwa kufanya
hivyo kutawasaidia wananchi kutokusafiri umbali mrefu wa kufuata huduma za
matibabu ya moyo ya kibingwa ambazo zinapatikana Dar es Salaam”, alisisitiza.
Aliendelea
kusema huduma zinazotolewa katika Taasisi hiyo ni za kibingwa na wataalamu
waliopo ni wachache na kuiomba Serikali
kuhakikisha wataalamu hao wazalendo hawarubuniwi na kwenda kufanya kazi mahali
kwingine pia kwa wataalamu ambao hawana ajira za kudumu waajiriwe ili wawe na
uhakika na maisha yao pamoja na moyo wa kufanya kazi.
“Ninaipongeza
Compounding Unit ambao wanatengeneza dawa za watoto kutoka kidonge cha mtu
mzima hadi kuwa kwenye matumizi ya watoto, hii inasaidia kupatikana kwa dawa za
moyo za watoto kwani dawa hizo hazipatikani kwenye soko la dawa nchini kutokana
na dawa hizo kutozalishwa viwandani”,.
Kwa
upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Dkt.
Doroth Gwajima aliishukuru kamati hiyo kwa kutembelea Taasisi hiyo na kujionea
huduma zinazotolewa na kuahidi
kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyoyatoa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
wataalamu ambao wanafanya kazi za kujitolea wanaajiriwa.
“Kufika
kwenu katika Taasisi hii kumewasaidia kufahamu changamoto mbalimbali
zinazowakabili, hata Taasisi ambazo hamjazitembelea changamoto zake zinafanana.
Ninaamini tukikaa kwa pamoja tutaona ni jinsi gani tutaweza kuzitatua
changamoto hizi na kuifanya sekta ya afya iweze kusonga mbele na kutoa huduma
bora zaidi kwa wananchi.
Mhe.
Dkt. Gwajima alisema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya ni
muhimu uwekezaji uliofanyika hapo awali na unaoendelea kufanyika ikiwa ni
pamoja na kununua mashine za kisasa za kufanya vipimo pamoja na kutoa tiba ukaendelea
kuimarisha huduma ili wagonjwa wengi waje
kutibiwa kutoka nchi za jirani.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema
tangu Taasisi hiyo ianzishwe mwaka 2015 hadi 2020 imeokoa maisha ya watanzania
444,445, kuokoa fedha zaidi ya bilioni
250.7 kwa kufanya upasuaji wa moyo hapa nchini kwa wagonjwa 8009 na kupatikana
kwa dawa muda wote kwa zaidi ya asilimia 95.
Prof.
Janabi alisema Taasisi hiyo imesaini mkataba na Asasi moja ya nchini Marekani
ijulikanayo kwa jina la Childs Heart ambao badala ya kuwapeleka watoto kutibiwa
nchini India wanawapeleka katika Taasisi hiyo kwaajili ya matibabu. Hadi sasa
wameshafanya upasuaji wa moyo kwa watoto saba ambapo watatu kutoka nchini
Kenya, wawili kutoka nchini Uganda na wawili kutoka nchini Malawi na Ethiopia.
Naye
Mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Hassan Kungu ambaye ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini
alisema ni mara yake ya kwanza kufika katika Taasisi hiyo amejifunza mambo
mengi ikiwa ni pamoja na wataalamu wa kitanzania kuweza kutambua mtoto kabla
hajazaliwa kama ana tatizo la moyo au la.
“Nimejifunza Taasisi hii imeweza kununua mitambo mikubwa ya kutibu magonjwa ya moyo bila kutumia mikopo au kuwa na madeni ya wazabuni na wataalamu wengi waliopo hapa ni watanzania. Ni jambo la kujivunia tunapata huduma za matibabu hapa nchini bila ya kwenda nje ya nchi, Taasisi zingine za afya ziige mfano kutoka JKCI”, alisema Mhe. Kungu.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Doroth Gwajima
akisoma risiti ya malipo ya dawa ambayo ilitolewa kwa mgonjwa anayetibiwa katika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma
na maendeleo ya jamii ilipotembelea Taasisi
hiyo jana kwa ajili ya kukagua matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kama
zinatumika ipasavyo. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni
Mbunge wa Maswa Mashariki Mhe. Stanslaus Nyongo.
Msimamizi
wa Wodi ya Watoto waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Afisa
Uuguzi Theresia Marombe akiwaeleza
baadhi ya wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii magonjwa
ya moyo yanayowakabili watoto waliolazwa katika wodi hiyo wakati kamati hiyo
ilipotembelea Taasisi hiyo jana. Watatu kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga ambaye
pia ni mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Salma Kikwete.
Mkurugenzi
wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Angella Muhozya akiwaeleza baadhi ya wajumbe wa Kamati
ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii jinsi upasuaji wa moyo
unavyofanyika wakati kamati hiyo ilipotembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kukagua
matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kama zinatumika ipasavyo pamoja na
kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa. Kushoto ni Mbunge wa Tunduru
Kaskazini ambaye pia ni Mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Hassan Kungu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akisoma taarifa ya maendeleo ya Taasisi hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii wakati kamati hiyo ilipotembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kwa ajili ya kukagua matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kama zinatumika ipasavyo pamoja na kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Comments
Post a Comment