Jumla ya watu 561 wamepimwa viashiria vya magonjwaya moyo bila malipo katika upimaji maalumuliofanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo wanawake waTaasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Mtunza
kumbukumbu za afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nuru Muhidini
akimjazia fomu kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya ya moyo mkazi wa Mbagala
wakati wataalam wa afya wanawake wa Taasisi hiyo walipokuwa wakitoa huduma ya vipimo
hivyo bila malipo leo kwenye Viwanja wa Mbagala Zakheem katika kuadhimisha siku
ya Wanawaje Duniani.
Afisa
Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hildergard Karau akimpima
shinikizo la damu makazi wa Mbagala aliyefika katika viwanja vya Mbagala Zakheem
leo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo uliofanywa na wataalam wa
afya wanawake wa JKCI katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Daktari
bingwa wa magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Honoratha
Maucky akimpima mapigo ya moyo mkazi wa Mbagala aliyefika katika viwanja vya
Mbagala Zakheem kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo uliofanywa na
wataalam wa afya wanawake wa taasisi hiyo jana kuadhimisha siku ya Wanawake
Duniani.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi
akizungumza na wakazi wa Mbagala waliofika katika viwanja vya Mbagala Zakheem
kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo uliofanywa na wataalam wa afya
wanawake wa JKCI Jana katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Diwani
wa Kata ya Mbagala Kuu Mhe. Shabani Abubakari akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wilaya
ya Temeke walioungana na wataalam wa afya wanawake kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) jana katika Viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya
kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya moyo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya
Wanawake Duniani tarehe 8/3/2021. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa
JCKI Prof. Mohamed Janabi
Jumla ya watu 561 wamepimwa viashiria vya magonjwa ya moyo bila
malipo katika upimaji maalum uliofanywa
na wataalamu wa magonjwa ya moyo wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI).
Upimaji huo ulioenda sambamba na
utoaji wa matibabu pamoja na kupewa rufaa kwa wale waliokutwa na matatizo ulifanyika
kwa muda wa siku mbili katika viwanja vya Mbagala Zakheem vilivyopo wilayani
Temeke ulikuwa ni maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani tarehe 8, Machi 2021.
Akizungumza na waandishi wa
habari hizi leo katika viwanja vya Mbagala Zakheem Mwenyekiti wa Wanawake wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na
wagonjwa mahututi Anjela Muhozya alisema katika upimaji huo pia walitoa elimu ya
lishe bora kwa afya bora ya Moyo.
Dkt. Anjela alisema kati ya watu 561 waliowapima asilimia 80
walikutwa na shinikizo la juu la damu kati ya hawa asilimia 50 walikuwa
wanajijua kuwa na tatizo lakini hawakuweza kuendelea na huduma za matibabu
kutokana na sababu mbalimbali za maisha, asilimia 30 hawakuwa wanajijua kabisa
kama wanatatizo hilo hawa walianzishiwa matibabu.
Waliokutwa na matatizo asilimia 40
waliweza kukamilisha huduma ya matibabu katika viwanja hivyo hii ikiwa ni
pamoja na kupewa dawa na ushauri na asilimia 20 walipewa rufaa ya kwenda
kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na Hospitali ya Temeke.
“Kati ya watu tuliowapima
asilimia 10 hawakuwa na tatizo lolote la kiafya ila uzito wao ulikuwa mkubwa kitu ambacho ni hatari kwa afya ya moyo. Hawa
tumewapa ushauri wa kubadili mfumo wa maisha katika ulaji wao wa vyakula pamoja
kufanya mazoezi mara kwa mara”, alisema Dkt. Anjela.
Mkuu wa wilaya ya Temeke Godwin Gondwe aliwashukuru wataalamu
wa JKCI kwa moyo wao wa upendo wa kuwafikiria wananchi wanyonge na kwenda
kuwapa huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo yoyote yale.
“Ninawashukuru sana kwa upendo wenu wa kuwafuata wananchi
wanyonge na kuwapa huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo kama tunavyofahamu
matitabu haya yanagharama. Kwa kuwafuata kwenu wananchi hawa wameweza kuokoa
fedha ambazo wangelipia hospitali na kwenda kuzitumia katika matumizi yao ya
kila siku”.
“Pia Afisa Ustawi wa jamii ameweza kuwasikiliza watu wenye
shida za kijamii na kuwapa maelekezo ya jinsi gani wataweza kufika JKCI na
kupata matibabu. Hii itawasaidia kutoogopa kufika pale kwa ajili ya kutibiwa kwa
kuwa hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu”.
Gondwe alisema wilaya yake itaendelea kushirikiana na JKCI katika
kuhakikisha wananchi wanyonge wanafikiwa na wataalamu wa taasisi hiyo na
kuwaomba wananchi wa Temeke kutumia
fursa hiyo ya upimaji wa afya zao bila
malipo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed
Janabi alisema amefika katika viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya kuwaunga
mkono wanawake wa Taasisi hiyo kwa kufanya upimaji kwa wananchi.
“Kama mnavyoona tunafanya upimaji kwa wanawake na wanaume na
wale ambao wamekutwa na matatizo wameanzishiwa matibabu kwa kupewa dawa na
wengine watakuja JKCI kwa ajili ya matibabu ya kibingwa”.
“Taasisi yetu itaendelea kuhakikisha wananchi wengi zaidi
wanafikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa pamoja na kupata elimu ya magonjwa hayo ambayo siyo magonjwa ya
kuambukiza na kama mtu atakuwa na uelewa nayo ataweza kuyaepuka”, alisisitiza Prof.
Janabi.
Naye Musa Kitimla ambaye ni mkazi wa Mbagala Kibondemaji
alisema alisikia katika redio kuna
huduma za upimaji wa moyo ambao utafanyika kwa muda wa siku mbili katika
viwanja vya Mbagala Zakheem akaona ni muhimu kufika hapo kwa ajili ya kupima afya yake.
“Ninamshukuru Mungu nimefika hapa na kupata huduma mbalimbali
za kupima afya na majibu yangu yameonekana sina tatizo lolote lile. Nitaendelea kuichunga afya yangu ili iendelee
kuwa salama. Ninawasihi wananchi wenzangu wakisikia mahali kuna upimaji wa aina
hii waende kwani licha ya kupima afya zao watapata ushauri pia”, alisema
Kitimla.
Katika upimaji huo wananchi walipimwa urefu, uzito,
shinikizo la damu (BP), sukari, Virusi vya Ukimwi na kupewa ushauri wa lishe
bora. Kwa wale waliokutwa na matatizo ya moyo wamepewa rufaa ya kwenda kutibiwa
katika Taasisi hiyo na Hospitali ya Temeke ili waweze kufanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu.
Comments
Post a Comment