Hakikisheni watoto wanapata tiba sahihi pindi wanapougua – Mtaalamu kutoa PASS
Kikundi cha wanawake kutoka Taasisi binafsi ya kuwezesha Sekta ya Kilimo Tanzania (PASS) wakimsikiliza mama ambaye mtoto wake amelazwa katika wodi ya watoto wenye magonjwa ya moyo walipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kulipia gharama za upasuaji kwa watoto wawili, kuwakatia kadi za bima watoto kumi pamoja na kutoa mahitaji madogo madogo kwa watoto waliolazwa katika wodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Meneja Rasilimali watu na Utawala kutoka Taasisi binafsi ya kuwezesha Sekta ya Kilimo Tanzania (PASS) Elita Naimani pamoja na Mkuu wa Idara ya Watoto wenye magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Sulende Kubhoja wakipitia majina ya watoto watakaosaidiwa gharama za upasuaji pamoja na kukatiwa kadi za bima ya afya baada ya wanawake kutoka taasisi hiyo kukabidhi kiasi cha Tsh. 4,540,000 kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi.
Kikundi
cha wanawake kutoka Taasisi binafsi ya Kuwezesha Sekta ya Kilimo Tanzania (PASS)
wakikabidhi zawadi za
Huggies diapers, sabuni za unga za kufulia, dawa za meno, miswaki na mafuta ya kupaka mwilini kwa ajili ya matumizi ya watoto waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kiwete (JKCI)
ikiwa ni katika kuadhimisha siku
ya wanawake Duniani.
Na: JKCI
Wazazi na walezi nchini wameshauriwa kuwapeleka
watoto wao katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu
stahiki pindi watakapoonesha viashiria
vyovyote vya ugonjwa.
Wito huo umetolewa leo na kiongozi wa kikundi cha wanawake
kutoka Taasisi binafsi ya kuwezesha sekta ya kilimo Tanzania (Private
Agricultural Sector Support-PASS) Elita Naimani walipotembelea Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) leo kwa ajili ya kuchangia gharama za matibabu kwa watoto
wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Elita Naimani ambaye pia ni Meneja Rasilimali watu na Utawala
wa PASS alisema katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani wameona ni vyema
watembelee watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo ili wawajulie hali pamoja
na kuwatia moyo mama zao wanaowauguza.
Alisema baada ya kuwatembelea watoto hao wameelezwa na
wataalamu kuna baadhi yao wanasumbuliwa na maradhi ya moyo yanayotokana na
bakteria wanaoshambulia valvu za moyo
(Rheumatic Heart Diseases).
“Tumeambiwa na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto
kuwa maradhi haya yanatokana na mtoto kuumwa homa ya mafindofindo (tonsillitis)
kama mtoto hatapata matibabu sahihi au hatamaliza dozi bakteria hao watashambulia
valvu za moyo na hivyo mtoto kuumwa maradhi hayo”,.
“Hiki kitu kimenishtua sana kwani ni mara nyingi mtoto
akiumwa unampa dawa ya maumivu pasipo kumpeleka hospitali. Ninawaomba wazazi
wenzangu tuache tabia hii ukiona mwanao hayuko sawa Kiafya mpeleke hospitali
kwa ajili ya matibabu na akipewa dawa hakikisha anakunywa kwa wakati na
kumaliza dozi yote”, alisisitiza Elita.
Aidha katika kuchangia kwao gharama za matibabu ya watoto hao
alisema waliona waiunge mkono kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake
Duniani inayosema wanawake katika
uongozi , chachu kufikia Dunia yenye usawa kwa kutimiza ndoto za watoto kwa kuwachangia
gharama za upasuaji, kuwakatia bima za afya pamoja na kuwapatia mahitaji yao ya kila siku wawapo wodini.
Elita alisema, “Watoto hawa pamoja na kuwa wanapitia katika
changamoto za ugonjwa wana ndoto zao kama ilivyo kwa watoto wengine hivyo basi
tumekuja kuwasaidia kutimiza ndoto hizo
kwa kuwachangia gharama za matibabu ili wakipona waendelee na maisha yao ikiwemo kusoma kama ilivyo kwa watoto wengine”,.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed
Janabi alikishukuru kikundi hicho cha wanawake kwa moyo wao wa upendo waliouonesha
kwa watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo kiuchumi kwa kuwachangia gharama za matibabu.
Prof. Janabi alisema matatizo makubwa ya moyo kwa watoto
wanaotibiwa katika Taasisi hiyo ni matundu, mishipa ya damu ya moyo kutokukaa
vizuri (Congenital Heart Diseases) pamoja na
maradhi ya moyo yanayotokana na bakteria wanaoshambulia valvu za moyo
(Rheumatic Heart Diseases).
“Asilimia kubwa ya wagonjwa wetu wanatoka katika familia
zenye uwezo mdogo kiuchumi na hivyo kushindwa kulipia gharama za matibabu.
Tunawashukuru kwa mchango wenu ambao utaokoa maisha ya watoto hawa na kuwarudishia tabasamu kama ilivyo kwa watoto wengine”,
alisema Prof. Janabi.
Akizungumza kwa niaba ya kinamama ambao watoto wao wamelazwa
katika wodi hiyo Anganile Mwaisaka aliwashukuru wanawake hao kutoka PASS kwa
kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto, kuwalipia bima za afya pamoja na kuwapatia zawadi mbalimbali.
Kikundi hicho kimetoa shilingi milioni nne kwa ajili ya
upasuaji wa moyo kwa watoto wawili, Tshs. 540,000/= kwa ajili ya kulipia kadi
kumi za bima ya afya kwa ajili ya watoto na kutoa zawadi za Huggies diapers, sabuni
za unga za kufulia, dawa za meno, miswaki , mafuta ya kupaka mwilini kwajili ya matumizi ya watoto waliolazwa katika wodi hiyo.
Comments
Post a Comment