Madaktari watatu wa magonjwa ya moyo kutoka China kutoa huduma za matibabu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwakaribisha madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya moyo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambao kupitia wizara ya Afya wametumwa nchini  kwaajili ya kutoa huduma za matibabu katika Taasisi hiyo. Mwaka 2022 Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imewatuma nchini madaktari bingwa 11 ambao watatoa huduma za matibabu JKCI, Hospitali yaTaifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.



Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  Prof. Mohamed Janabi akizungumza na kiongozi wa timu ya madaktari kutoka nchini China  Daktari Bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi  Meng Yong mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kuwapokea madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya moyo kutoka nchini humo waliopangiwa kufanya kazi katika Taasisi hiyo. Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia wizara ya Afya imewatuma nchini madaktari bingwa 11 ambao watatoa huduma za matibabu JKCI, Hospitali yaTaifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Taasisi hiyo na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambao  kupitia wizara ya Afya wametumwa nchini kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu ya moyo katika Taasisi hiyo. Mwaka 2022 JKCI imewapokea madaktari watatu ambao ni wa wagonjwa mahututi, upasuaji wa moyo na watoto.

************************************************************************************************************************************************************************************************************

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imewapokea madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya moyo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambao wametumwa katika Taasisi hiyo kwaajili ya kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nchini.

Akizungumza  katika hafla fupi ya kuwakaribisha  madaktari hao iliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwatuma madaktari hao wa moyo kutoa huduma katika Taasisi hiyo na kuahidi kushirikiana nao kwa muda wote watakaokuwepo hapa nchini.

Prof. Janabi alisema Taasisi hiyo kila baada ya miaka miwili imekuwa ikiwapokea madaktari bingwa wa Moyo kutoka nchini China ambao kwa kiasi kikubwa wamesaidia kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wagonjwa na hivyo kuokoa maisha yao.

“Tumewapokea madaktari watatu ambao ni daktari bingwa wa wagonjwa walioko katika chumba cha uangalizi maalum (ICU), daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto na daktari bingwa wa upasuaji wa moyo ambao watashirikiana na wataalamu wetu katika kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa”, .

“Wataalamu wetu pamoja na wenzetu kutoka nchini China ambao tumewapokea leo watafanya kazi kwa pamoja hii itawasaidia kubadilishana ujuzi wa kazi waliokuwa nao  na hivyo kuboresha zaidi huduma tunazozitoa”, alisema Prof. Janabi.

Kwa upande wake kiongozi wa madaktari hao ambaye ni Daktari Bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi  Meng Yong alishukuru kwa mapokezi waliyoyapata na kusema kuwa wamefurahi kuja nchini kutoa huduma kwa watanzania na kuahidi kushirikiana kwa pamoja na wataalamu wa JKCI ili wagonjwa waendelee kupata huduma bora za matibabu.

Kila baada ya miaka miwili Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia wizara ya Afya  inawatuma madaktari bingwa kuja kutoa huduma za matibabu ya kibingwa hapa nchini hii ikiwa ni sehemu ya mahusiano na diplomasia katika sekta ya Afya kati ya Tanzania na China,  ambapo uhusiano huo ulianza tangu uongozi wa Rais wa awamu ya kwanza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha China Hayati Mao Zedong.

Kwa mwaka huu wa 2022 Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imewatuma nchini madaktari bingwa 11 ambao watatoa huduma za matibabu ya kibingwa JKCI, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari