Ufahamu ugonjwa wa shinikizo la juu la damu

 

Mkurugenzi wa Huduma ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya akimpima Salome Majaliwa shinikizo la damu (BP) ikiwa ni maadhimisho ya siku ya shinikizo ja juu la damu duniani ambayo kila mwaka hufanyika tarehe 17 mwezi wa tano.


Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  Gudila Swai akionesha mashine inayopima shinikizo la damu (BP) na kiwango cha oxygen mwilini ikiwa ni maadhimisho ya siku ya shinikizo la juu la damu duniani ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 17 mwezi wa tano.

Mfamasia wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Miraji Dhahiri akiwa ameshika dawa za shinikizo la juu la damu zinazotolewa kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya shinikizo la juu la damu duniani ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 17 mwezi wa tano.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce  akimpima Rebecca Kengele ambaye ni msimamizi wa masijala za Taasisi hiyo shinikizo la damu (BP) wakati wa  maadhimisho ya siku ya shinikizo ja juu la damu duniani ambayo kila mwaka hufanyika tarehe 17 mwezi wa tano.

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa wamebeba kauli mbiu ya  siku ya shinikizo la juu la damu duniani ambayo kila mwaka hufanyika tarehe 17 mwezi wa tano. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Pima msukumo wa damu kwa usahihi, iweke Presha yako sawa, Ishi maisha marefu”.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Honoratha Maucky akijadili athari za shinikizo la juu la damu na Afisa Muuguzi wa Taasisi hiyo Ziada Joram wakati wa maadhimisho ya siku ya shinikizo la juu la damu duniani ambayo kila mwaka hufanyika tarehe 17 mwezi wa tano.

************************************************************************************************************************************************************************************

1.     Shinikizo la juu la damu ni nini?

Shinikizo la juu la damu hutokea wakati nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa ya moyo kuwa  kubwa kuliko kawaida. Ongezeko hilo husababisha moyo kufanya kazi kupita kiasi ili uzungushe damu katika mishipa ya moyo. Kwa kawaida halina dalili, ila likidumu lina madhara makubwa kwa afya. Wakati mwingine kuna dalili ndogo ndogo ambazo zinaweza kukujulisha kuwa upo salama au una ugonjwa huu.

Dalili hizo ni maumivu ya kichwa, macho kuona kiza, maumivu ya misuli ya shingo, kutoka damu puani na wakati mwingine kupoteza fahamu za upande mmoja wa mwili (kiharusi).

Ugonjwa huu wa shinikizo la juu la damu unaweza kuwapata watoto na watu wazima.

2.     Aina za Shinikizo la juu la damu

Kuna aina mbili za shinikizo la juu la damu ambazo ni shinikizo la juu la damu la asili  na shinikizo la damu linalosababishwa na magonjwa mbalimbali. Kati ya asilimia 90 hadi 95 ya wagonjwa wanasumbuliwa na shinikizo la juu la damu la asili hii inamaana kuwa  wana ugonjwa huu bila kuwa na chanzo cha kisayansi kinachofahamika.

Aina hii ya Shinikizo la juu la damu haina sababu inayoeleweka na mara nyingi inaweza kusababishwa na mgonjwa kuwa na historia ya ugonjwa katika familia yao, uzito mkubwa kupindukia, matumizi ya chumvi nyingi, kutokufanya mazoezi ya mara kwa mara, uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi na umri mkubwa. Asilimia kubwa ya watu wanaopata Shinikizo la juu la damu huwa katika kundi hili .

Shinikizo la juu la damu linalosababishwa na magonjwa mbalimbali yaliyopo katika mwili wa binadamu kama figo, mishipa ya moyo na mfumo wa homoni. Aina hii ya shinikizo la juu la damu  huathiri asilimia 5 hadi 10 iliyobaki ya watu wenye shinikizo la juu la damu. Kwa mfano, mara nyingi aina hii ya Shinikizo la damu huweza kuwatokea wanawake wakati wa ujauzito  na huondoka mara baada ya kujifungua.

3.     Madhara ya Shinikizo la juu la damu

Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu husababisha mwili kupooza, shambulio la moyo, moyo kushindwa kufanya kazi, kutanuka kwa ukuta wa mishipa ya moyo, ugonjwa  wa figo, kupunguza nguvu za kiume na kupunguza muda wa kuishi.

4.     Jinsi ya kuepuka kupata shinikizo la juu la damu

Unaweza kuepuka kupata shinikizo la juu la damu kwa kufanya mazoezi, kuzingatia  lishe bora kwa kula  matunda, mboga mboga, vyakula vyenye madini ya potassium vile vile punguza kula vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta  na chumvi. Kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri, kutambua  kiwango cha sukari katika mwili wako, kutambua msukumo wako wa damu na kiwango cha mafuta mwilini.

Kwa kufanya vipimo na kufutilia mwenendo wa  mwili wako mara kwa mara unaweza ukazuia kifo cha ghafla kinachotokana na shinikizo la juu la damu. Kupima mapigo ya moyo mara kwa mara kunaweza kukakusaidia kujua kama una tatizo hili au la.

5.     Hatua mbalimbali zilizochukuliwa ili kukabiliana na ugonjwa huu

Kutokana na takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO)  za mwaka 2017 kuna  zaidi ya wagonjwa bilioni moja  wenye tatizo la shinikizo  la juu la damu kundi kubwa la wagonjwa hawa walitoka katika nchi za Afrika. Kwa mwaka huo huo wa 2017 ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ndiyo ulioongoza kwa kuuwa watu wengi Duniani.

Kwa upande wa Tanzania hakuna idadi  kamili ya namba za watu wanaosumbuliwa na tatizo hili kwa nchi nzima. Kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo ni Hospitali pekee ya moyo hapa nchini kati ya wagonjwa 100,853 waliotibiwa mwaka 2021 asilimia 60 (60,776) walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu. Hii inamaana kuwa kwa kila wagonjwa 10 tuliowaona sita walikuwa na tatizo la la shinikizo la juu la damu au matokeo ya ugonjwa huu.

Hapa nchini kuna watu wengi wanaosumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu lakini hawatambui kuwa na ugonjwa huo kwani hawajapima. Asilimia 30 tu ndiyo waliopima na  wanaojijuwa kuwa na ugonjwa huo. Asilimia 9 (tisa) wanajijuwa kuwa na ugonjwa huu na wako katika matibabu kati ya hawa asilimia 4 wameweza kudhibiti msukumo wao wa damu mwilini (Blood Pressure).

Tarehe 17/05/2022 ni siku ya maadhimisho ya shinikizo la juu la damu Duniani. Katika kuadhimisha siku hii wataalamu wa afya kupitia vyombo mbalimbali vya habari wanatoa uelewa wa jinsi ya kuepukana na ugonjwa huu pamoja na kufanya upimaji kwa wananchi bila malipo yoyote yale. Kwa kupima afya kunasawaidia wananchi kujua kama wanamatatizo ya shimikizo la juu la damu au la na hivyo kuanza matibabu mapema.

6.     Matumizi ya dawa za shinikizo la juu la damu

Matumizi sahihi ya dawa ni kufuata kanuni, taratibu na maelekezo yote yaliyotolewa na mtaalamu wa afya. Kwa kawaida, kuna utaratibu tofauti wa kutumia dawa, kuna za kutumia kila baada ya saa 24, 12 au saa nane, na baada au kabla ya chakula.Mgonjwa akienda kinyume na maelekezo haya atakuwa anafanya matumizi yasiyo sahihi na anaweza kukumbwa na athari ikiwamo kupoteza uhai, kudhoofika, kuibua aina nyinginezo za magonjwa au kupata ulemavu wa kudumu.

Vilevile, inashauriwa kutotumia dawa usiyoshauriwa au kuandikiwa na mtaalamu wa afya au kabla ya kufanya vipimo kamili. Mjulishe mtaalamu kama unatumia au umetumia dawa za tiba mbadala kwani zinaweza kusababisha mwingiliano unaoweza kukusumbua.

Mgonjwa anashauriwa kubeba orodha au vyeti vya dawa anazotumia kila aendapo kliniki, kumtaarifu mtaalamu wa afya mara apatapo madhara ya dawa anazotumia na akisahau kumeza dawa basi anywe mara tu atakapokumbuka. Awapo safarini, mgonjwa asiziache dawa zake, na ajaze upya dawa zake wiki moja kabla hazijaisha. 

Usiache kutumia dawa hata kama utapata nafuu wala usiruke dozi, usinywe dawa mara mbili kama ulisahau na ziweke dawa zako sehemu maalum uweze kuziona kila siku na kuzikumbuka kwa urahisi na zingatia muda wa kuzitumia. Dawa za usiku zitumike usiku mfano zile za kuzuia kuganda kwa damu na dawa za kupunguza mafuta mwilini.

Ujumbe wa Siku ya Shinikizo la juu la damu kwa mwaka huu wa 2022 ni “Pima msukumo wa damu kwa usahihi, iweke Presha yako sawa, Ishi maisha marefu”.

 

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024