Daktari bingwa wa moyo aonya madhara yatokanayo na kuacha kutumia dawa za presha
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze Dkt.
Allen Mlekwa akiwatambulisha wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa wananchi wa Chalinze kabla ya kuanza kwa upimaji wa magonjwa
ya moyo na kisukari unaofanyika katika
Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze ya Msoga Mkoani Pwani.
Meneja wa kampuni ya waingizaji wa wasambazaji wa dawa za
binadamu ya Sun Pharma nchini Tanzania Sapajan Sorajam akiwaambia wananchi dawa
ambazo kampuni hiyo itazitoa bila malipo kwa watu watakaokutwa na magonjwa ya
moyo, kisukari na shinikizo la juu la damu wakati wa upimaji uliyofanywa na
wataalam wa JKCI kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze katika Hospitali ya Msoga Mkoani Pwani.
Afisa lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna
Faraji akitoa elimu ya lishe kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze waliofika
katika Hospitali ya Msoga kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo
na kisukari unaofanywa na wataalam wa afya kutoka JKCI.
Afisa Uhasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Mohamed Isimbuye akiwagawia vipeperushi vinavyoelezea huduma za matibabu
zinazotolewa na JKCI wananchi waliofika katika Hospitali ya Halmashauri ya
Chalinze iliyopo Msoga kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo unaofanywa
na wataalam wa moyo kutoka JKCI katika Halmashauri hiyo iliyopo wilayani
Bagamoyo mkoani Pwani.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mwanahela
Ally akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyefika katika Hospitali ya wilaya
hiyo iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa
ya moyo uliokua ukifanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi wa
Chalinze.
Mfamasia kutoka Kampuni ya uagizaji na usambazaji dawa za
binadamu ya Sun Pharma Simon Salum akimuelezea matumizi ya dawa mwananchi
aliyekutwa na tatizo la sukari wakati wa upimaji uliofanywa na wataalam wa afya
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa wananchi wa Hamashauri ya
Chalinze katika Hospitali ya Msoga. Kampumi ya Sun Pharma imetoa dawa bila
malipo kwa wananchi wote waliokutwa na magonjwa ya shinikizo la damu, kisukari
na moyo.
Fundi sanifu wa moyo (Mteknolojia) kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Jasmine Keria akimpima mfumo wa umeme wa moyo
(Electrocardiograph – ECG) mwananchi wa Halmashauri ya Chalinze wakati wa
upimaji uliofanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi hao jana katika
Hospitali ya Msoga Mkoani Pwani.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kiwetwe (JKCI) Mohamed Alyoce akimpima mwananchi wa Halmashauri ya
Chalinze kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo-Cardiograph)
wakati wa upimaji uliofanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi hao
jana katika Hospitali ya halmashauri hiyo iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo.
Mtafiti kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zabella
Seif akifanya mahojiano na wananchi wa Halmashauri ya Chalinze waliofika katika
upimaji wa magonjwa ya moyo na kisukari uliofanywa na wataalam wa afya kutoka
JKCI jana katika Hospitali ya halmashauri hiyo iliyopo Msoga iliyopo Mkoani
Pwani.
Picha na: JKCI
**********************************************************************************************************
Kuacha kutumia dawa za shinikizo la juu la damu (Presha) kunaweza kusababisha madhara makubwa mwilini ikiwa ni pamoja na moyo na figo kutokufanya kazi vizuri kama inavyotakiwa, ugonjwa wa kiharusi, vifo vya ghafla na misuli yad amu ya moyo kutanuka.
Onyo hilo limetolewa leo na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge wakati akiongea na wananchi waliofika kupima magonjwa ya moyo na kisukari katika hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha mafunzo na utafiti wa Taasisi hiyo alisema wataalamu wa JKCI wako katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuwapima wananchi na kutoa uelewa wa magonjwa ya moyo, matumizi sahihi ya dawa za moyo na lishe bora.
“Siku ya jana tumefanya upimaji kwa watu 185 wengi wao walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu lakini wameacha kutumia dawa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa dawa, kutokuwa na uwezo wa kununua dawa na kutokuwa na uelewa wa matumizi sahihi ya dawa. Kuna ambao tumewakuta misuli yao ya damu ya moyo imetanuka hii yote ni madhara ya kuacha kutumia dawa za presha”,.
“Tumewaanzishia dawa na kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya dawa kwani wengi wanatumia dawa na kuziacha hawajui kuwa matumizi ya dawa za presha ni maisha pia tumewaambia madhara wanayoweza kuyapata pale watakapoacha kutumia dawa za presha”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema huduma
wanazozitoa katika upimaji huo ni za kupima urefu na uzito, kuangalia uwiano
baina ya urefu na uzito, kiwango cha sukari mwilini, shinikizo la damu,
kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi na kuangalia jinsi
moyo unavyofanya kazi, kutoa elimu ya lishe bora kwa afya ya moyo na
matumizi sahihi ya dawa za moyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata kwani wameweza kupima vipimo vya moyo, kisukari pamoja na kupewa dawa bila malipo yoyote yale.
“Nilikuwa nikilala usiku nasikia moyo wangu unadunda kwa nguvu nikapata hofu kuwa ninatatizo la moyo, baada ya kusikia wataalamu wa moyo wako hapa nimekuja kupima na kukutwa moyo wangu hauna shida ila nina tatizo la presha ambayo iko juu nimeandikiwa dawa za kwenda kutumia “, alishukuru mzee Salum Funua mkazi wa Msoga.
Juliana Selemani mkazi wa Chalinze Mbwilingu alishukuru kwa huduma aliyoipata na kusema anatatizo la presha kwa muda wa miaka mitatu na huwa anatumia dawa lakini pale anapojisikia kuwa na naafuu anaacha kuzitumia.
“Leo hii baada ya daktari kunifanyia vipimo amenikuta na tatizo la kutanuka kwa misuli ya moyo ameniambia tatizo hii limetokana na kuacha kutumia dawa kwani presha imeuumiza moyo wangu. Baada ya kupewa elimu hii sintaacha kutumia dawa, ninawashauri wagonjwa wa presha kama mimi wasiache kutumia dawa hata pale wanapojiona kuwa na naafuu”, alisema Mama Juliana.
Kwa upande wake fundi sanifu wa moyo (Technician) kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jasmine Keria alisema upimaji huo umesaidia kuweza kutumika kwa mashine nzuri na ya kisasa ya kupima mfumo wa umeme wa moyo ambayo ilikuwepo katika Hospitali hiyo.
“Hospitali hii inamashine nzuri ya kisasa ya kupima mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiogram - ECG) lakini hawakuwa wanaitumia hii ni kutokana na kutokuwa na utaalamu nayo, nimeifungua mashine hii nimeiset program na tumeitumia kuwapima wagonjwa”,.
“Nimewafundisha jinsi ya kuitumia na hapa tulipo tunashirikina na wataalamu wa hapa kuwapima wagonjwa kwa kufanya hivyo kutasaidia wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali hii kuweza kupata huduma hii ya vipimo”, alisema Jasmin.
Naye Mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Dkt. Allen Mlekwa alishukuru kwa huduma inayotolewa kwa wananchi ya kupimwa magonjwa ya moyo na kisukari pamoja na wafanyakazi wa hospitali ya halmashauri hiyo kufundishwa jinsi ya kutumia mashine ya mfumo wa umeme na moyo pamoja na kuwapima wagonjwa.
Upimaji huo wa siku mbili
unafanywa na wataalamu wa Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na
wenzao wa Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga, kampuni ya dawa
za binadamu ya Sunpharma ambayo inatoa dawa kwa watu wanaokutwa na tatizo la
moyo, sukari, maumivu, upungufu wa damu na kampuni ya ulinzi ya K4 Security
ambao wanahakikisha uwepo wa usalama kwa wananchi pamoja na mali zao.
Comments
Post a Comment