Wananchi 437 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kisukari ambapo asilimia 60 wamekutwa na matatizo
Mwananchi wa Halmashauri ya Chalinze akisoma jarida la
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa upimaji maalum unliofanywa kwa
wananchi hao kwa ajili ya kuchunguza magonjwa ya moyo na kisukari katika
Hopitali ya Halmashauri hiyo iliyopo
Msoga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Afisa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aliston
Jovin akiwagawia vipeperushi vinavyoelezea huduma za matibabu zinazotolewa na
JKCI wananchi waliofika katika Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo
Msoga kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo uliofanywa na
wataalam wa moyo kutoka JKCI katika Halmashauri hiyo iliyopo wilayani Bagamoyo
mkoani Pwani.
Afisa Uuguzi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Rahabu Tamba akimpima urefu na uzito mwananchi aliyefika katika Hospitali ya Halmshauri
ya Chalinze iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa
magonjwa ya moyo uliokua ukifanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi
wa Chalinze.
Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Magreth Ng’ondya
akimuelezea mwananchi umuhimu wa kutumia dawa za shinikizo la damu wakati wa
upimaji wa magonjwa ya moyo, kisukari na shinikizo la damu uliofanywa na
wataalam wa moyo kutoka taasisi hiyo kwa wananchi wa Chalinze kwa siku mbili na
kumalizika jana katika Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo msoga
Wilayani Bagamoyo.
Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari akisoma majibu ya vipimo vilivyofanywa na mwananchi wa Chalinze baada ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kisukari wakati wa upimaji uliyofanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze iliyopo wilayani Bagamoyo.
Wataalam wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa upimaji maalum uliofanyika kwa siku mbili kwa wananchi wa Chalinze kuchunguza magonjwa ya moyo, kisukari na shinikizo la damu katika Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo msoga wilayani Bagamoyo
**********************************************************************************************************************************************************************
Wananchi 437 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na
kisukari ambapo asilimia 60 wamekutwa
na tatizo la shinikizo la juu la damu (Presha) na asilimia 20 ya waliokutwa na
tatizo hilo tayari walishapata madhara ya shinikizo la juu la damu ikiwa ni
pamoja na moyo kutokufanya kazi vizuri na kutanuka kwa misuli ya damu ya moyo.
Wananchi wengine walikutwa na
matatizo ya matundu kwenye moyo, mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika
mpangilio wake, matatizo kwenye vyumba vya moyo na mishipa ya damu ya moyo
kushindwa kupitisha damu vizuri.
Hayo yamesemwa jana na daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter
Kisenge wakati wa kufanya tathimini ya zoezi la upimaji wa magonjwa ya
moyo na kisukari lililofanyika katika hospitali ya Halmashauri ya Chalinze
iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni mkuu wa
kitengo cha mafunzo na utafiti wa Taasisi hiyo alisema wagonjwa 27 walikutwa na
matatizo ya moyo yaliyohitaji uchunguzi na matibabu ya kibingwa na hivyo kupewa
rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
“Katika upimaji huu tulifanya
upimaji kwa watoto 22 ambapo watatu kati yao walikutwa na matatizo ya moyo ya
kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokuwa katika
mpangilio wake wa kawaida, watoto hawa tumewapa rufaa ya kuja kufanyiwa
kufanyiwa uchunguzi zaidi na kutibiwa katika Taasisi yetu”,.
“Zoezi la upimaji limeenda vizuri
mwitikio ni mkubwa wananchi wamekuja kwa wingi na wamefurahia kupata matibabu
kutoka kwa wataalamu wetu. Kwa kuwa tatizo la shinikizo la juu la damu ni kubwa
nawashauri wananchi waepuke uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe uliopitiliza na
kutokula vyakula vyenye mafuta mengi pia wazingatie lishe bora na ufanyaji wa
mazoezi kwa kufanya hivi wataepuka kupata magonjwa ya moyo”, alisema Dkt.
Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete inaunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi
wanafikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa kwa kuwafuata wananchi mahali
walipo kwa ajili ya kutoa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo na kisukari
bila malipo yoyote yale kwa kufanya hivi wananchi wengi wataweza kufikiwa na
huduma za matibabu ya kibingwa ya magonjwa hayo kwa haraka zaidi.
Naye Mganga mkuu wa Halmashauri ya
Chalinze Dkt. Allen Mlekwa aliwashukuru wataalamu waliotoa huduma za
upimaji na matibabu kwa wananchi na kusema upimaji huo ulihusisha madaktari
bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI pamoja na wenzao wa Hospitali ya Msoga.
Dkt. Mlekwa alisema waliokutwa na
matatizo ya moyo wengine walikuwa na kliniki katika hospitali mbalimbali
na walikuwa wanatumia dawa lakini waliacha kutokana na sababu mbalimbali na
baada ya kufanyiwa vipimo vya moyo wamekutwa mioyo yao imetanuka na wengine
wamekutwa na ugonjwa sugu wa kisukari. Baadhi yao hawakuwa wanafahamu kabisa
kuwa na tatizo la moyo na hivyo waliwaanzishia dawa za kutumia.
“Kuwepo kwa zoezi hili la upimaji
kumetufanya tufahamu kunatatizo kubwa la watu wenye matatizo ya moyo na
kisukari hivyo basi nasi tumejipanga kuboresha kliniki yetu ya moyo na
kisukari iliyopo katika Hospitali ya Msoga kwa siku ya alhamisi ili wagonjwa
waliokuwa wanakwenda kutibiwa Hospitali za Tumbi, Amana, Mwananyamala na
Muhimbili waje kutibiwa hapa”,.
“Kwa kuwa tuna mashine za kupima
vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) na
kuchunguza mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography - ECG) tutawafanyia
wagonjwa wenye shida ya moyo vipimo hivi hapa hapa na kama tutawakuta na
matatizo makubwa tutawarufaa kwenda kutibiwa katika Hospitali kubwa zaidi”,.
“Wananchi wengine wametoka kilomita
zaidi ya 100 karibu kabisa na Tanga na Mvumero wamekuja hapa kwa ajili ya
kufuata huduma hii ya upimaji, tutajipanga ili tuweze kufanya mobile kliniki za
kwenda kutoa huduma za upimaji katika vituo vya afya vya Msata, Kibindu, Lugoba
na Miono kwa kufanya hivi wananchi wengi watafikiwa na huduma za matibabu ya
moyo na kisukari”, alisema Dkt. Mlekwa.
Kwa upande wa wananchi waliopata
huduma hiyo walishukuru kwa huduma ya uchunguzi na matibabu ya bila
malipo waliyoipata na kusema imewapunguzia gharama ya kusafiri na
kuwafuata wataalamu Dar es Salaam pamoja na kulipia matibabu hayo.
Fredrin Ikumbera mkazi wa Lugoba
alisema alipima vipimo na kukutwa moyo uko sawa lakini amekutwa na shida ya
presha amepewada dawa za kutumia pamoja na ushauri wa lishe bora na
kuambiwa apunguze matumizi ya vyakula vya wanga pamoja kupunguza kunywa pombe
kwani ni hatari kwa afya ya moyo wake.
“Nilikuwa ninawasiwasi kuhusu moyo
wangu kwani mazingira niliyokuwa naishi hayakuwa salama. Ninawasihi wananchi
wenzangu kutumia nafasi za upimaji pindi zinapotokea kwa kwenda kupima
afya zao pia kwa upande wa Serikali iendelee kuhakikisha wananchi walioko
vijijini wanapata huduma za matibabu ya kibingwa kwani kutokana na mazingira
yao ni vigumu kufikiwa na huduma hizi”, alisema Ikumbera.
Comments
Post a Comment