RC MAKALA: Kampeni ya kupima afya bure imekuwa na mafanikio makubwa
- Awataka wananchi
kuanza matibabu kwa wale waliogundulika na magonjwa yasiyoambukiza
-
Awashukuru Clouds
Media Group, Madaktari na wadau wengine waliofanikisha kampeni ya Afya Check
-
Aelekeza uwepo wa
Hospitali tembezi kwa madaktari bingwa katika kila Wilaya.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos
Makalla leo Juni 13 amehitimisha zoezi la siku kumi za upimaji Afya bure ambapo
mpaka kufikia siku ya jana Juni 12 zaidi ya wananchi 7,030 walihudumiwa na
madaktari bingwa na wabobezi kutoka Hospitali kubwa za Mkoa huo.
Akihitimisha zoezi hilo RC Makalla amesema
zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa ambapo kati ya wananchi 7,030
waliohudumiwa wananchi 1,522 walipima Shinikizo la damu, 247 Kisukari, 808 walipimwa
tatizo la moyo, uchangiaji wa damu unit 203, kipimo cha ultrasound 1,726, 189
tezi dume,949 walipata chanjo ya Uviko – 19, 601 walipima Saratani ya shingo ya
kizazi, 1,369 walipima tatizo la meno na macho wananchi 1,673.
Kutokana na mwamko kuwa mkubwa, RC Makalla
amemuelekeza Katibu Tawala wa Mkoa huo kuanzisha huduma ya Hospitali
inayotembea “Mobile hospital” kwa kutumia gari maalum litakalokuwa limesheheni
madaktari bingwa.
Aidha RC Makalla ametumia zoezi hilo kutoa
wito kwa wananchi kujiwekea utaratibu wa upimaji afya mara kwa mara kutokana na
takwimu kuonyesha wananchi wengi waliogundulika kuwa na matatizo ya afya
hawakuwa wakitambua.
Hata hivyo RC Makalla amewasisitiza wananchi
kufanya mazoezi ili kujiepusha na hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukizwa
ikiwemo kisukari, shinikizo la damu, saratani na magonjwa mengine.
Pamoja na hayo RC Makalla amewashukuru wadau
waliofanikisha zoezi hilo wakiwemo Clouds Media Group kupitia kipindi cha afya
check ambao ndio waratibu wa zoezi hilo.
Comments
Post a Comment