Wataalamu 20 kutoka Taasisi ya Moyo Uganda wajifunza utoaji wa huduma za matibabu ya moyo nchini
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya akiwaonesha maeneo ya Taasisi hiyo wageni kutoka Taasisi ya Moyo Uganda walipotembelea JKCI leo kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo pamoja na kujifunza namna ambavyo Taasisi hiyo inaendesha shughuli zake.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni Mkuu wa idara ya magonjwa ya moyo kwa watoto Sulende Kubhoja akielezea huduma zinazotolewa katika idara hiyo kwa wageni kutoka Taasisi ya Moyo Uganda walipotembelea JKCI leo kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo pamoja na kujifunza namna ambavyo Taasisi hiyo inaendesha shughuli zake.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JCKI) ambaye pia ni mkuu wa idara ya magonjwa ya moyo kwa watu wazima George Longopa akielezea huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wa moyo wanaoudhuria kliniki katika Taasisi hiyo kwa wageni kutoka Taasisi ya Moyo ya Uganda walipotembelea JKCI leo kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo pamoja na kujifunza namna ambavyo Taasisi hiyo inaendesha shughuli zake.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Tulizo Shemu akielezea huduma zinazotolewa katika chumba cha upasuaji mdogo wa moyo bila kufungua kifua (Cathlab) kwa wageni kutoka Taasisi ya Moyo ya Uganda walipotembelea JKCI kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo pamoja na kujifunza namna ambavyo Taasisi hiyo inaendesha shughuli zake.
********************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Wataalamu 20 kutoka Taasisi ya Moyo Uganda wametemblea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinatolewa pamoja na kujifunza namna ambavyo taasisi hiyo inavyoendesha shughuli zake.
Akizungumza na waandhisi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed
Janabi alisema baada ya kusikia mafanikio yaliyopatikana katika Taasisi hiyo wataalamu
hao kutoka nchini Uganda wameona ni vyema kwenda kujifunza mafanikio hayo pamoja
na changamoto zake ili nao wafikie hatua kama ya JKCI.
Prof.Janabi alisema tangu Taasisi hiyo ianzishwe mwaka 2016
imekuwa na mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo kwa
kufanya upasuaji kwa wagonjwa 8663 na kuona wagonjwa zaidi ya laki sita na hivyo kuwa hospitali bora ya Serikali inayotoa
huduma za kibingwa za matibabu ya moyo katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
“Mwaka 2017 baadhi ya wabunge kutoka nchini Uganda walitembelea
Taasisi yetu kwa ajili ya kujifunza na leo hii tumepokea wataalamu 20 kutoka
nchini humo ambao nao wamekuja kujifunza jinsi tulivyofanikiwa katika utoaji wa
huduma za matibabu ya moyo. Sisi tumefanikiwa kwa kuwa Serikali inatuunga mkono
kwa zaidi ya asilimia 120 na hata upasuaji tunaoufanya ni salama”,.
“Taasisi yetu inapokea wagonjwa kutoka nchi za Afrika ya Mashariki
na Kati ikiwemo Uganda ambapo kwa mwaka
huu tumeshafanya upasuaji wa moyo kwa watoto sita ambao walikuwa na matatizo ya
moyo ya kuzaliwa nayo. Watoto hawa wanaendelea vizuri na walisharudi nchini
mwao”, alisema Prof. Janabi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu alisema amefurahi kuona wenzao
kutoka nchini Uganda wamekuja kuwatembelea kwaajili ya kujifunza wanachokifanya na na kuwaeleza walipofikia ili
wawasaidie kutokana na mapungufu waliyokuwa nayo.
“Ukiangalia historia
ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete haitofautiani na ya kuanzishwa
kwa Taasisi ya Moyo Uganda kwani zote zimetokea katika Hospitali za Taifa, jambo la muhimu ni kuwatia moyo ili
wasikate tamaa na kuweza kufika hapa
tulipofika sisi kwani wao wako hatua tatu nyuma yetu”.
Prof. Mahalu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo
na mishipa ya damu alisema Taasisi ya Moyo Uganda ni ya Serikali, kwani huduma za matibabu ya moyo bila kushikiliwa
na Serikali zinagharama kubwa na zikiwa na utashi wa kisiasa kuwa zinawasadia watu wataweza kupata kila kitu ambacho watakitaka na hivyo kuweza
kufanya vizuri katika kutoa huduma kwa wagonjwa.
Dkt. James Magara ambaye ni Mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya
Moyo Uganda alisema wamekuja nchini kujifunza katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete ili wasifanye makosa kiutendaji kwani wao wako katika hatua za mwanzo
tangu taasisi hiyo ianzishwe na kama wataanza vizuri wataweza kufanya vizuri zaidi.
“Tanzania na Uganda tumekuwa
na mahusiano mazuri tangu miaka ya nyuma, tumefaidika na Tanzania kwani wakati
wa vita vya Idd Amin Tanzania ilikuja kutusaidia. Na sisi leo tumekuja
kujifunza kwa wataalamu wenzetu kuona ni vitu gani wamevifanya na kuweza
kufikia hatua hii kwani kuwa na Taasisi kama JKCI siyo kitu cha muda mfupi”,
alisema Dkt. Magara.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Uganda Dkt. John
Omagino alisema Serikali ya nchi hiyo imeamua kujenga kituo cha matibabu ya moyo
ili kupunguza idadi ya wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi. Pia kituo hicho
kiwe na ubora sawa na vituo vingine vya Afrika Mashariki ili wagonjwa wa moyo watibiwe
ndani ya nchi hizo ikiwemo Uganda.
Dkt. Omagino alisema taasisi yao bado ni ndogo na wanatakiwa kusonga mbele zaidi, Serikali
yao imewapa ardhi na wamepata fedha
ambazo zitawawezesha kujenga jengo kubwa la Taasisi hiyo hivyo basi ili waweze
kufanya kitu kizuri wameona watembelee vituo vingine vya moyo vilivyopo Afrika
Mashariki na kujifunza vitu ambavyo vimewafanya wamefanikiwa hii ikiwa ni
pamoja na kusomesha wataalamu wa afya.
“Gharama za matibabu ya moyo ni kubwa na wengi wanashindwa
kulipia lakini wenzetu wa JKCI wanatoa
huduma kwa watu wote wa kipato cha juu, cha kati na cha chini tumekuja kuona ni
jinsi gani wamefanikiwa katika hili”,.
“Changamoto tunayokutana nayo ni namna ya kuwasomesha
wataalamu nje ya nchi kwani wengine wanaenda kusoma muda mrefu zaidi ya miaka
mitano na wengine hawarudi pindi wanapomaliza masomo yao, lakini kama tutakuwa
na kozi za muda mfupi ndani ya nchi zitatusaidia watalamu hawa wakimaliza
masomo yao wataendelea na kazi ndani ya nchi yao”, Dkt. Omagino .
Dkt. Omagino alisema wanaangalia jinsi gani ya kuzuia magonjwa hayo na siyo
kutibu kwani kama watu watafuata mtindo bora wa maisha wataepukana na magonjwa
ya moyo hii ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kupunguza
unywaji wa pombe uliokithiri na kuacha matumizi ya tumbaku.
Wataalamu hao ambao ni wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Uganda wameambatana na watunga sheria na sera watakuwa katika Taasisi hiyo kwa muda wa siku mbili na watatembelea maeneo mbalimbali ya JKCI pamoja na kuzunguma za wakuu wa Idara ili waweze kubadilishana ujuzi wa kazi.
Comments
Post a Comment