Wafanyakazi wapya JKCI waonywa kutojihusisha na vitendo vya rushwa
Baadhi ya wafanyakazi wapya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakila kiapo cha kufuata masharti ya utumishi wa umma wakati wa kikao cha kuwapokea kilichofanyika jana katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
*************************************************************
Wafanyakazi wapya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kutojiingiza katika vitendo vya rushwa vitakavyopelekea kudhorotesha utoaji wa huduma bora katika Taasisi hiyo.
Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na wafanyakazi hao kabla ya kuanza kazi.
Dkt. Kisenge alisema kutoa huduma kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma pamoja na kuwa na utashi kutawasaidia kurudisha furaha kwa wagonjwa ambao wamekuwa wakiwategemea.
“Hatutaki kusikia mmechukua ama mmetoa rushwa kwani hatutafurahia hata kidogo mtu mmoja aje kusambaratisha umoja wetu tulioujenga katika Taasisi yetu”, alisema Dkt. Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge aliwataka wafanyakazi hao kutumia fursa zinazopatikana katika Taasisi hiyo vizuri na kupenda kujiendeleza katika fani zao ili kuleta chachu zaidi katika kutoa huduma bingwa bobezi.
Kwa upande wake Dkt. Innocent Humay ambaye ni mwajiriwa mpya katika Taasisi hiyo ameahidi kwa niaba ya wenzake kufanya kazi kwa weledi na kuleta mafanikio zaidi ya Taasisi hiyo.
Dkt. Innocent alisema waajiriwa hao walipofika JKCI wamepokelewa vizuri na kupata mafunzo ya siku mbili ambayo yatawasaidia kufanya kazi vizuri
“Kwa niaba ya wenzangu tunahaidi kufanya kazi na kufuata miongozo tuliyopewa kuwasaidia wagonjwa wanaotibiwa hapa”, alisema Dkt. Innocent
Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepewa kibali cha kuajiri Wafanyakazi wapya 51 wa kada mbalimbali ambapo kati yao wafanyakazi 24 wamesharipoti kazini.
Comments
Post a Comment