Wafungwa zaidi ya 600 Gereza kuu Ukonga kupimwa moyo
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza na Mkuu wa Kitengo cha Afya Nsajigwa Mwankenja akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo inayofanyika kwa wafungwa wa Gereza Kuu Ukonga leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza na Mkuu wa Kitengo cha Afya Nsajigwa Mwankenja wakitembea kuelekea eneo ambalo kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo inaendelea kwa wafungwa waliopo katika Gereza Kuu Ukonga lililopo jijini Dar es Salaam.
*******************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Picha na JKCI
Wafungwa zaidi ya 600 waliopo katika Gereza kuu Ukonga
kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya
siku sita inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Kambi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa JKCI
kusogeza huduma za kibingwa za moyo karibu na wananchi huku ikitambua
kwamba afya ni haki ya kila binadamu na msingi muhimu wa maendeleo ya mtu
na taifa kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kambi hiyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
alisema hii ni mara ya kwanza katika Serikali ya Awamu ya Sita kwa JKCI
kufikisha huduma hizo za kibingwa katika mazingira ya gerezani.
“Kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ni sehemu muhimu
ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, badala ya
kusubiri wananchi wenye changamoto za moyo kusafiri umbali mrefu kuifuata JKCI,
imechukua hatua ya kuwafikia wananchi katika maeneo walipo ikiwemo wafungwa wa
gereza kuu Ukonga”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema kambi hiyo ina umuhimu mkubwa kwa
sababu inatambua kwamba kuwa mfungwa hakumvui mtu hadhi yake ya kuwa binadamu
wala haki yake ya msingi ya kupata huduma za afya kwani wafungwa ni sehemu ya
jamii na wanapohitaji huduma za afya wanapaswa kupata huduma hizo kwa
kuzingatia utu, usawa na viwango vinavyokubalika.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza na
Mkuu wa Kitengo cha Afya Nsajigwa Mwankenja aliushukuru uongozi wa JKCI kwa
kulikumbuka kundi la wafungwa na kuwafikia kwaajili ya kuwafanyia uchunguzi wa
afya kwani wanahitaji huduma hizo.
Kamisha Nsajigwa alisema wafungwa wakimaliza kutumikia
kifungo huku wakiwa na afya duni watashindwa kulitumikia taifa kwa ukamilifu
hivyo ni vyema kwa pamoja wakashirikiana na wadau kuhakikisha wafungwa
wanapomaliza muda wa kutumikia adhabu zao wanatoka na afya njema ili waweze
kushiriki katika majukumu ya ujenzi wa taifa wakiwa imara.
“Wafungwa hawakai gerezani milele, wanapokuwa na afya njema
kunakuwa na manufaa hata kwa jamii kwani wakitoka gerezani na maambukizi hasa
ya magonjwa yanayoambukiza wanaweza kuiambukiza jamii pia”, alisema Kamishna
Nsajigwa
Kambi hiyo ya matibabu ni miongoni mwa kambi za matibabu
zaidi ya 26 ambazo JKCI imezifanya katika mikoa Tabora, Kilimanjaro, Geita, Dar
es Saalaam, Arusha, Mtwara, Lindi, Zanzibar, Dodoma, Iringa, Manyara, Bukoba,
Pwani, Kigoma, Rukwa, Songea, Mwanza, Tanga, Mbeya, Singida pamo na katika
makampuni mbalimbali nchini ambapo jumla ya watu 41,164 walifanyiwa uchunguzi
na matibabu ya magonjwa ya moyo
- Mwisho
–
Comments
Post a Comment