Wanawake wenye matatizo ya kifafa cha mimba epukeni kubadilisha wenza: Dkt. Raya

 


Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na wajawazito wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Raya Chambali akitoa elimu kuhusu magojwa ya wanawake kwa wagonjwa wanaopata huduma katika Hospitali hiyo iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam. 

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na wajawazito wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Raya Chambali akiandika taarifa za mgonjwa aliyefika kupata huduma katika hospitali hiyo iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam. 

*************************************************************************************                                        ***************************************

Na JKCI


Wanawake wenye matatizo ya kupata kifafa cha mimba wakati wa ujauzito wameshauriwa kutobadilisha mwenza baada ya kujifunga mtoto wa kwanza ili kuepuka vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

Rai hiyo imetolewa na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na wajawazito wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospital ya Dar Group Raya Chambali wakati akitoa elimu kwa wanawake wajawazito wanaotibiwa na Hospitali hiyo.

Dkt. Raya alisema baadhi ya vifo vya wanawake wajazito hutokana na kifafa cha mimba kinachosababishwa na tatizo la shinikizo la damu kuwa juu kipindi cha ujauzito.

“Kifafa cha mimba kinaweza kuepukika endapo mama atazingatia ushauri wa watalaamu wa afya na kutobadilisha mwenza wa kuzaa naye kwasababu ugonjwa huo ni wa kijenetiki ambao chanzo chake hutoka kwa mwanaume” alisema Dkt. Raya

Aidha Dkt. Raya aliwataka wanawake kuwa na tabia ya kufanya maandalizi ya mapema ya kitatibu kabla ya kupata ujauzito ili waweze kuuandaa mwili na kuwa salama kubeba ujauzito.

“Mama akizingatia ushauri wa kitalaamu kuna uwezekano mdogo wa kupata shinikizo la juu la damu na kuepuka kifafa cha mimba kwani atashauriwa kuzingatia lishe bora na kupunguza matumizi ya chumvi nyingi wakati wa ujauzito”, alisema Dkt. Raya

Naye mama wa watoto watatu anayepata huduma katika Hospitali ya JKCI Dar Group Judith Nelson alisema amewahi kupata tatizo la kifafa cha uzazi mara baada ya kujifungua mtoto wa kwanza lakini baada ya kupata ushauri kutoka kwa madaktari wa JKCI Dar Group tatizo hilo halijawahi kumrudia tena.

“Ni kweli usipobadilisha mwenza unakuwa katika hali salama ya kutokupata tena kifafa cha uzazi na mimba, kwa sasa nimeweza kupata watoto wengine wawili na sijapata ugonjwa huo kwasababu nilizingatia ushauri wa daktari” alisema Judith.

Judith alisema tatizo la kifafa cha mimba ni hatari kwa afya ya mama na mtoto kwani kinaweza sababisha kiharusi kwa mama kutokana na shinikizo la damu kuwa juu sana, lakini pia kupelekea mtoto kuzaliwa kabla ya wakati.


Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma