Benki ya CRDB yachangia shilingi milioni 100 matibabu ya watoto wanaotibiwa JKCI.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 100 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge leo katika viwanja vya Posta Kijitonyama vilivyopo jijini Dar es Salaam. Hundi hiyo imetolewa na Benki ya CRDB kupitia fedha zilizokusanywa kwa washiriki wa mbio za CRDB msimu wa saba kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akifanya mazoezi ya viongo pamoja na baadhi ya viongozi walioshiriki katika mbio za CRDB msimu wa saba zilizofanyika leo katika viwanja vya Posta Kijitonyama vilivyopo jijini Dar es Salaam. Benki ya CRDB imechangia shilingi milioni 100 matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI kupitia mbio hizo
Benki ya CRDB yachangia shilingi milioni 100 kwaajili ya matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotoka katika familia zisizokuwa na uwezo wa kugharamamia matibabu wanaotibiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Fedha hizo zimetolewa kupitia mbio za CRDB msimu wa saba zilizofanyika leo katika viwanja vya Posta kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa mbio hizo Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alisema utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 umeanza kuonekana kwa vitendo kupitia juhudi za kuokoa maisha ya watanzania ikiwemo kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo.
“Milioni 100 zilizotolewa na CRDB ni moja ya mpango mkakati wa kutekeleza dira ya maendeleo ya Taifa 2050 kwani fedha hizi zinaenda kuokoa maisha ya watoto wanaotibiwa JKCI na kuleta matumaini mapya kwa familia”, alisema Mhe. Abdulla
Mhe. Abdulla alisema suala la afya linahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali hivyo kutoa rai kwa wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi yenye tija ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
“Kushiriki mazoezi kwa ukubwa huu ni jambo lakupongezwa kwani magonjwa mengi yasiyoambukiza yanaweza kuepukika kwa kufanya mazoezi hivyo wananchi wafanye mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa hayo”, alisema Mhe. Abdulla.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema benki hiyo itaendelea kutumia majukwaa mbalimbali kama sehemu ya kuisaidia jamii.
“Tangu mwaka 2020 tumekusanya zaidi ya bilioni tano ili kusaidia jamii na tayari watoto 400 waliotibiwa na JKCI wamenufaika na fedha hizo na kupewa nafasi nyingine ya kuishi”, alisema Nsekela.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema matatizo ya moyo kwa watoto ni mengi hivyo mchango unaotolewa na Benki ya CRDB kupitia mbio hizo ni uwekezaji mkubwa katika kuokoa maisha ya watoto hao.
“Kila watoto milioni mbili wanaozaliwa elfu 13 wana matatizo mbalimbali ya moyo na watoto zaidi ya elfu moja wapo katika foleni ya kusubiria huduma za upasuaji wa moyo hivyo mchango huu ni msaada mkubwa kwa jamii ya watanzania”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisisitiza umuhimu wa wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara na kuwataka wananchi kutembea angalau nusu saa mara tatu kwa wiki.
- Mwisho -

Comments
Post a Comment