Watu 350 wapimwa moyo Muleba

Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja na wenzao wa Hospital ya Ndolage iliyopo Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera wakati wa kambi maalumu ya siku sita ya matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa huo.

****************************************************************************************************************

Watu 350 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupitia uratibu uliofanywa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (ELCT) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi.

Upimaji huo umefanyika kwa siku sita katika Hospitali ya Ndolage iliyopo Wilaya ya Muleba mkoani Kagera mwezi Agosti mwaka huu ikiwa ni jitihada zinazofanywa na JKCI kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi katika ngazi ya Wilaya pamoja kutekeleza Mkataba wa Makubaliano uliosainiwa kati ya JKCI na Hospitali ya Ndolage.

Akitoa taarifa ya Kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli Rweyemamu alisema tatizo la shinikizo la damu lilikuwa kati ya ugonjwa ulioongoza katika kambi hiyo ikifuatiwa na ugonjwa wa kisukari. 

“Matatizo mengine tuliyoyabaini katika kambi hiyo ni matatizo ya moyo kushindwa kufanya kazi vizuri, matatizo ya mishipa ya damu pamoja na magonjwa sugu ya figo. Upande wa watoto tulibaini baadhi ya magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo ikiwemo matundu pamoja na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo”, alisema Dkt. Rweyemamu

Dkt. Rweyemamu alisema watu 23 walipewa rufaa ya kwenda JKCI kwa ajili ya uchunguzi zaidi pamoja na kupatiwa matibabu maalumu, huku watoto watano wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo kupewa rufaa kwaajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo. 

Dkt. Rweyemamu alisema kupitia kambi hiyo wataalamu wa JKCI walifungua kliniki ndogo ya huduma za haraka (Fast track clinic) ambayo iliweza kuhudumia wagonjwa 67 na kuifanya Hospitali ya Ndolage kuvutiwa na kliniki hiyo.

Kupitia kambi hiyo wagonjwa wote waliohitaji dawa za magonjwa ya moyo na mishipa ya damu pamoja na dawa za magonjwa mengine yanayoambatana na hali hizo walipatiwa dawa jambo ambalo lilirahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi hao.

Huduma hiyo ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Ndolage iliyopo Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera imeonyesha ari ya JKCI kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo karibu na wananchi lakini pia kuwapa wananchi huduma kwa wakati na elimu ambayo itaisaidia jamii kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.


Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma