Watu 200 wanufaika na huduma ya uchunguzi na matibabu ya macho Arusha
Daktari bingwa wa macho wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI - ALMC) John Njelango akimpima kipimo cha kuchunguza macho mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza inayofanyika katika Hospitali hiyo iliyopo jijini Arusha.
Afisa Uuguzi wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI -
ALMC) Fabian Bura akimsaidia mkazi wa Arusha aliyefika katika kambi maalumu ya
uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza kwaajili ya kufanya uchunguzi
wa afya inayofanyika katika Hospitali iliyopo jijini Arusha.Mhudumu wa afya
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre
(JKCI - ALMC) Ombeni Daniel akimpima joto la mwili mkazi wa Arusha aliyefika katika
kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza inayofanyika
katika Hospitali hiyo iliyopo jijini Arusha.
Baadhi ya
wananchi wa mkoa wa Arusha wakisoma vipeperushi vinavyoelezea elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza wakati wa
kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza inayofanyika
katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI-ALMC) iliyopo jijini
Arusha.
Afisa huduma kwa
wateja wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran
Medical Centre (JKCI - ALMC) Josephine Butesigirwe akitoa elimu kuhusu magonjwa
yasiyoambukiza kwa wakazi wa Arusha waliofika katika kambi maalumu ya uchunguzi
na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza inayofanyika katika Hospitali hiyo
iliyopo jijini Arusha.
Na JKCI
**************************************************************************************************************
Watu 200
wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya macho kupitia kambi maalumu ya uchunguzi
na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa macho inayoendeshwa na
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre
(JKCI–ALMC) kwa kushirikiana na Kampuni ya GSM Foundation.
Akizungumza
wakati wa kambi hiyo Daktari Bingwa wa Macho wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete –
Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI–ALMC) John Njelango alisema watu
hao wamepatiwa huduma za macho ikiwemo kufanyiwa kipimo cha presha ya macho,
uchunguzi wa madhara ya kisukari kwenye macho pamoja na vipimo vya miwani.
Dkt. John
alisema kupitia kambi wataalamu wamebaini kuwa wagonjwa wenye matatizo
yanayohitaji matibabu zaidi ikiwemo mtoto wa jicho na presha ya macho ni wengi
huku baadhi wakigundulika kuwa na matatizo ya macho ambayo huenda walidhani
hayatibiki.
“Ikiwa leo ni
siku ya tatu tangu kambi hii ianze tayari tumeshawaona watu 200 waliohitaji
huduma za uchunguzi wa macho. Watu wote hawa tumewafanyia vipimo na wale
waliogundulika kuwa na matatizo tumewapa huduma kutokana na matatizo
waliyonayo”, alisema Dkt. John.
Dkt. John alisema
huduma hizo zimewasaidia wataalamu kubaini mahitaji mbalimbali ya wagonjwa ambapo
wengi wameonekana kuhitaji miwani ya kutembelea na kusomea huku wengine
wakibainika kuwa na matatizo yanayohitaji ufuatiliaji na matibabu zaidi.
“Kuna uhusiano kati ya magonjwa ya kisukari na
presha ya macho, magonjwa haya yanaweza kuathiri macho, ni muhimu watu
wakaendelea kufika katika Hospitali yetu kupata huduma katika kambi ili waweze
kupima macho na magonjwa mengine yanayotolewa katika kambi yetu”, alisema Dkt.
John.
Kwa upande wake mkazi
wa Arusha Joyce Molel alisema amefurahishwa na huduma alizopata katika kambi
hiyo akibainisha kuwa kupitia kambi hiyo ameweza kujitambua na kufahamu tatizo
lililokuwa likimsumbua.
“Nimehudumiwa
vizuri nimepata majibu yangu hapohapo na kujua tatizo linalonisumbua kwa miaka
mingi, lakini pia nimeshauriwa miwani ambayo natakiwa kuvaa ili iweze
kunisaidia katika shughuli zangu”, lisema Joyce.
Charles Manga
mkazi wa Arusha alisema kambi kama hizo ziwe zinafanyika mara kwa mara
kuwasaidia wananchi kupata huduma za afya bila gharama na hata kuweza kutatua
changamoto za kiafya walizonazo.
“Kama kuna watu
bado hawajafika katika kambi hii basi wasisite kufika kwani wataondoka hapa
wakiwa na furaha kufuatia huduma watakazozipata”, alisema Charles.
Kambi
hiyo inalenga kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza
yakiwemo magonjwa ya moyo na macho karibu na wananchi wa Kanda ya Kaskazini huku
ikitoa fursa kwa wananchi kutambua mapema changamoto za afya na kuchukua hatua
stahiki.




Comments
Post a Comment