JKCI kuanzisha Kitengo cha matibabu ya moyo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe (NRRH).

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na kamati ya kuanzisha huduma za matibabu ya moyo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Njombe (NRRH) wakati wa kikao cha kujadili ushirikiano kati ya JKCI na NRRH kilichofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), wataalamu wa afya wa mkoa wa njombe na wafanyakazi wa hospitali ya rufaa ya mkoa Njombe (NRRH) wakisikiliza wakati wa kikao cha kujadili ushirikiano wa kuanzisha huduma za matibabu ya moyo kati ya JKCI na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Njombe jana jijini Dar es Salaam.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Juma Mfanga akizungumza na kamati ya kuanzisha huduma za matibabu ya moyo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Njombe (NRRH) wakati wa kikao cha kujadili ushirikiano kati ya JKCI na NRRH kilichofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Hospitali ya JKCI Dar Group Dkt. Tulizo Shemu akizungumza na kamati ya kuanzisha huduma ya magonjwa ya moyo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Njombe (NRRH) wakati wa kikao cha kujadili ushirikiano kati ya JKCI na NRRH kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa JKCI jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Hospitali ya JKCI Dar Group Dkt. Tulizo Shemu, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Juma Mfanga, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe Dkt. Gilbert Kwesi na baadhi ya wataalamu wa afya kutoka JKCI na NRRH wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kujadili ushirikiano wa kuanzisha huduma ya magonjwa ya moyo kati ya JKCI na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Njombe jana katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.

*************************************************************************************************************

Utalii tiba kuimarika mkoani Njombe baada ya kuanza kwa mchakato wa kuanzisha ushirikiano wa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo kati ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Njombe (NRRH) hatua inayolenga kuwahudumia wananchi wa Nyanda za Juu Kusini pamoja na wagonjwa kutoka nchi jirani.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa kikao cha kwanza cha majadiliano kuhusu ushirikiano wa kuanzishwa kwa kitengo cha moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Njombe (NRRH).

Akizungumza wakati wa kikao hicho Dkt. Kisenge alisema ushirikiano huo utasaidia kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa NRRH kupitia mafunzo na kubadilishana uzoefu na wataalamu wa JKCI.

“JKCI inataka kuwafikishia wananchi huduma za magonjwa ya moyo pale walipo ndiyo maana tunawajengea uwezo wataalamu wa afya wa NRRH ili wananchi wasisafiri umbali mrefu kuweza kupata huduma hizi”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema Njombe ni eneo la kimkakati kutokana na kuwa karibu na nchi za Malawi na Zambia hivyo kituo hicho hakitawahudumia wananchi wa Njombe pekee bali kinaweza pia kuchangia katika kukuza utalii tiba nchini.

“Ni matarajio yetu kwamba hospitali hii itakuwa moja ya kituo bora kabisa jumuishi cha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu mkoani Njombe ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Njombe, mikoa jirani na nchi zilizopo jirani”, alisema Dkt. Kisenge

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Juma Mfanga alisema ushirikiano huo ni muhimu kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma za matibabu ya moyo katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.

Akizungumzia ukubwa wa tatizo la magonjwa ya moyo mkoani Njombe Dkt. Mfanga alisema takwimu za mwaka 2025 zinaonyesha kuwa kati ya asilimia 40 hadi 48 ya wagonjwa waliotibiwa walikuwa na matatizo yanayohusiana na moyo au mishipa ya damu, hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuanzisha huduma hizo mapema ili wagonjwa wapate matibabu kabla ya kupata madhara makubwa.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe Dkt. Gilbert Kwesi alisema hospitali hiyo imekuwa ikitoa wastani wa rufaa zisizopungua mbili kwa siku kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo.

Dkt. Kwesi alisema takwimu za hospitali zinaonesha ongezeko la wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza hususan magonjwa ya moyo wanafika wakiwa tayari wamepata madhara makubwa ikiwemo kiharusi.

Ushirikiano huo kati ya JKCI na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe (NRRH) unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za magonjwa ya moyo Nyanda za Juu Kusini na kupunguza mzigo wa wagonjwa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo.


Comments