JKCI yazindua Bodi ya kusimamia tafiti (Institutional Review Board – IRB) kuimarisha utafiti wa magonjwa ya moyo nchini
Wajumbe
wa bodi ya kusimamia tafiti (Institutional Review Board – IRB) ya Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo uliofanyika
leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.
Na
JKCI
************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) imezindua Bodi ya kusimamia tafiti (Institutional Review Board – IRB) itakayohakikisha
tafiti za JKCI zinazingatia maadili, sheria na viwango vinavyotakiwa katika
tafiti zinazohusisha binadamu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa
bodi hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya IRB Dkt. Ahmed Abdallah alisema kuanzishwa kwa
IRB ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa usimamizi wa tafiti zinazofanywa
na JKCI hivyo bodi hiyo ina jukumu la kupitia na kutoa kibali kwa tafiti zitakazofanyika.
“Tunatarajia kwamba tafiti
zitakazofanyika hapa zitaangaliwa na bodi na kupewa kibali, hatua hii itasaidia
kuongeza ufanisi wa JKCI katika kutekeleza majukumu yake ya utafiti na
kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinakuwa na msingi mzuri wa kitaalamu na
kimaadili”, alisema Dkt. Abdallah.
Kwa upande wake daktari bingwa wa
upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Evarist Nyawawa alisema kuanzishwa kwa bodi
ya IRB ni hatua muhimu kwa JKCI kutokana na nafasi ya taasisi hiyo
inavyotambulika kimataifa katika kutoa huduma bingwa za uchunguzi na matibabu
ya magonjwa ya moyo.
“Taasisi yetu ina taarifa (data)
nyingi sana na tunahitaji kufanya tafiti kubwa kuhusiana na magonjwa ya moyo
ili mwisho wa siku jamii na taifa zima wafaidike na uchunguzi unaofanyika
kutokana na magonjwa yanayotibiwa kwenye Taasisi yetu”, Alisema Dkt. Nyawawa
Dkt. Nyawawa alisema JKCI
inaendelea kukua na kupanuka, hivyo uwezo wa kufanya tafiti ni wa muhimu ili
iweze kuongeza mchango wake kitaifa na kimataifa na kuweza kuilinda jamii na
magonjwa ya moyo.
Naye Afisa Utafiti wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Hilda Tutuba alisema bodi ya IRB itasaidia
kuhakikisha tafiti zinazohusisha binadamu zinafanyika kwa kuzingatia usalama,
haki na maadili ya wanaofanyiwa utafiti.
“Tunapoongelea tafiti yoyote
ambayo inamhusisha mwanadamu ni lazima ipite katika mapitio ili kuangaliwa kama
imefuata masharti na vigezo vinavyotakiwa kuhakikisha kwamba haileti madhara
kwa yule mtu ambaye utafiti utafanywa kwake”, alisema Hilda.
Kuanzishwa kwa Bodi ya Kusimamia
Tafiti (IRB) kunatarajiwa kuimarisha uwezo wa JKCI katika kufanya tafiti
zinazolenga kuongeza maarifa kuhusu magonjwa ya moyo na kuboresha huduma za
afya huku tafiti hizo zikifanyika kwa kuzingatia misingi ya maadili na usalama
wa washiriki.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Comments
Post a Comment