Wataalamu wa JKCI wafanya ukaguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe (NRRH), maandalizi ya kuanzisha huduma bingwa za moyo
Mganga Mfawidhi wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe (NRRH) Dkt. Gilbert Kwesi akiwa katika
picha ya pamoja na Maafisa wa Uhakiki na Udhibiti Ubora kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) na wafanyakazi wa NRRH wakati maafisa hao walipotembelea
Hospitali hiyo kwaajili ya kufanya ukaguzi wa maandalizi ya kutoa huduma bingwa
za magonjwa ya moyo Mkoani Njombe.
Mganga Mfawidhi wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe (NRRH) Dkt. Gilbert akizungumza na Maafisa
wa Uhakiki na Udhibiti Ubora kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wakati maafisa hao walipotembelea Hospitali hiyo kwaajili ya kufanya ukaguzi wa
maandalizi ya kutoa huduma bingwa za magonjwa ya moyo Mkoani Njombe.
Kaimu Mkuu wa Kitengo
cha Uhakiki na udhibigti ubora wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Adelphina Ncheye akielezea namna ukaguzi wa maandalizi ya huduma za matibabu ya
moyo utakavyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe (NRRH) wakati
maafisa wa Uhakiki na Udhibiti Ubora kutoka JKCI walipotembelea Hospitali hiyo
iliyopo Mkoani Njombe.
Na JKCI
***********************************************************************************************
Maafisa wa Uhakiki na
Udhibiti Ubora kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) watembelea
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe (NRRH) kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa
maandalizi ya kutoa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo katika Hospitali
hiyo.
Ziara hiyo ni miongoni
mwa hatua za kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
Kabla ya kuanza ukaguzi
katika Hospitali hiyo maafisa hao walitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe
Mhe. Anthony Mtaka kuelezea madhumuni ya ziara hiyo na shughuli za ukaguzi.
Akizungumza na maafisa
hao Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka alisema ujio wao umeanza
kuonyesha utekelezaji wa Serikali ya awamu ya sita wa kusogeza huduma bingwa za
uchunguzi na matibabu ya moyo karibu na wananchi.
Mhe. Mtaka alisema kuanzishwa
kwa huduma hizo kutaifanya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe kuwa kituo
kikubwa cha tiba ya magonjwa ya moyo kwa Nyanda za Juu Kusini, huku akitaja pia
kufungua fursa ya utalii tiba kwa raia wa nchi zilizopo Jumuiya ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwemo Malawi na Zambia.
Kupitia ziara hiyo
maafisa hao watafanya ukaguzi wa maeneo muhimu yanayohusiana na utoaji wa
huduma za moyo ikiwemo miundombinu, vifaa tiba, rasilimali watu, mazingira ya
kutolea huduma, na mifumo ya kuhakikisha huduma zinatolewa kwa viwango
vinavyotakiwa.
Ukaguzi huu umelenga
kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuhakikisha mazingira yanaandaliwa kwa
ajili ya utoaji wa huduma bora na salama za moyo.
Ushirikiano kati ya
JKCI na NRRH unatarajiwa kusaidia kusogeza huduma za kibingwa za magonjwa ya
moyo karibu na wananchi wa Mkoa wa Njombe na maeneo ya jirani ili kupunguza
ulazima wa wagonjwa kusafiri umbali mrefu, pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa
NRRH katika kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma katika Hospitali hiyo.




Comments
Post a Comment