Watu 303 wapimwa moyo mkoani Manyara


 Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Evelyne Furumbe akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography - ECHO) mtoto wakati wa kambi maalumu ya siku 5 ya uchunguzi na matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara (MRRH) na kimalizika hivi karibuni.

Mtaalamu wa vipimo vya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Loyce Gideon akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mkazi wa Manyara aliyefika katika kambi maalumu ya siku 5 ya uchunguzi na matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara (MRRH) na kumalizika hivi karibuni.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Geofrey Mohammed akizungumza na mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya siku 5 ya uchunguzi na matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara (MRRH) na kumalizika hivi karibuni.

Kaimu Mganga Mfawadhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara (MRRH) Dkt. Yesige Mutajwaa akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa MRRH mara baada ya kumaliza kwa kambi maalumu ya siku 5 ya uchunguzi na matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH na kumalizika hivi karibuni.

Picha Na JKCI

*****************************************************************************************************************

Jumla ya wananchi 303 wa Mkoa wa Manyara wamefaidika na huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo zilizokuwa zikitolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara (MRRH).

Huduma hizo zimetolewa katika kambi maalumu ya siku tano ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyokuwa ikifanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara (MRRH) na kumalizika hivi karibuni Mkoani Manyara.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo alisema wananchi hao wamefanyiwa vipimo vya kibingwa vya moyo ikiwemo Echocardiography (Echo) na Electrocardiogram (ECG) ambapo asilimia 46 walibainika kuwa na magonjwa mbalimbali ya moyo.

“Kati ya wananchi tuliowachunguza asilimia 46 tumewakuta na magonjwa mbalimbali ya moyo. Baadhi yao tumewapatia huduma za matibabu na ushauri huku wengine tukiwapa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya kibingwa zaidi”, alisema Dkt. Pedro.

Dkt. Pedro alisema matatizo mengi waliyoyabaini kwa watu wazima ni pamoja na tatizo la shinikizo la juu la damu ambalo ni miongoni mwa visababishi vikuu vya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara (MRRH) Dkt. Yesige Mutajwaa alisema kambi hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa imewawezesha wananchi wengi kupata huduma za kibingwa ambazo awali zilikuwa hazipatikani kwa urahisi.

“kupitia kambi hii wataalamu wa JKCI wameweza kuwabainisha watu 23 ambao wameonekana kuwa na changamoto zinazohitaji upasuaji wa moyo na matibabu ya kina zaidi”, alisema Dkt. Mutajwaa.

Dkt. Mutajwaa aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa ushirikiano waliouonesha katika kutoa huduma bingwa za moyo na kueleza kuwa hospitali hiyo imeanza kuwajengea uwezo wataalamu wake kupitia kushirikiano walionao na JKCI ambapo zaidi ya watumishi watano wamepata mafunzo ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika Taasisi hiyo.

Aidha aliiomba JKCI kuendelea kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara (MRRH) katika kutoa huduma za kibingwa, kubadilishana uzoefu na kujenga uwezo wa wataalamu ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa mkoa huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma wakati wa kambi hiyo wamewapongeza wataalamu wa JKCI kwa kutoa huduma kwa upendo bila kuchoka na kuhakikisha kuwa watu wote waliohitaji huduma hizo wamezipata.

Catherine John mkazi wa Manyara alisema huduma aliyoipata imemsaidia kujitambua, kuchukua hatua za mapema na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili tatizo la moyo alilonalo lisimdhuru zaidi.

"Kambi hii imetusaidia wananchi wengi ambao hatukuwa na uwezo wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu kuzipata hapa kwetu kwa urahisi", alisema Catherine

John Mbilinyi mkazi wa Manyara alisema ni muhimu wananchi kutumia fursa kama hizi kupima afya zao kwa sababu wanaweza kuwa na matatizo ya moyo bila ya wao kujua kama wanamatatizo hayo.  

Kambi hiyo ya siku tano ni sehemu ya juhudi za Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) za kusogeza huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo karibu na wananchi na kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufikisha huduma hizo kwa wananchi wote.

-      Mwisho - 

Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma