Asilimia 30 ya watu wenye magonjwa yasiyoambukiza wanaotibiwa JKCI hutoka Kanda ya Kaskazini


Daktari wa macho wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI – ALMC) John Moteswa akimuonesha Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya GSM Foundation Faith Gugu kifaa maalum kinachotumika kufanya uchunguzi wa macho (Slit Lamp) alipotembelea kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza inayofanyika katika Hospitali ya JKCI-ALMC jijini Arusha.

Kaimu Mkurugenzi wa Tiba na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Dharura wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI – ALMC) Peter Mabula akimueleza Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya GSM Foundation Faith Gugu huduma zinazotolewa katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza inayofanyika katika Hospitali ya JKCI-ALMC jijini Arusha.



Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI – ALMC) Veronica Masandika akimpima mapigo ya moyo mwananchi aliyefika kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza katika kambi maalumu inayofanyika katika hospitali ya JKCI-ALMC jijini Arusha.


Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI – ALMC) Dkt. Godwin Kivuyo, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya GSM Foundation Faith Gugu, wafanyakazi wa JKCI – ALMC na GSM foundation wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza inayofanyika katika hospitali ya JKCI-ALMC jijini Arusha.



 Mtunza kumbukumbu za afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI – ALMC) Jackline Nguruka akimsajili mwananchi aliyefika kupata matibabu katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza inayofanyika katika Hospitali ya JKCI-ALMC jijini Arusha.

Picha na JKC

Inakadiriwa kuwa takribani asilimia 30 ya watu wenye magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) hutoka kanda ya kaskazini.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI – ALMC) Dkt. Godwin Kivuyo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza inayofanyika katika Hospitali ya JKCI – ALMC iliyopo mkoani Arusha.

Dkt. Kivuyo alisema kambi hiyo inalenga kuwapa wananchi fursa ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza hususani magonjwa ya moyo na macho bila gharama lakini pia kuwapa fursa ya kuwa na tabia ya kuchunguza afya zao mara kwa mara.

Dkt. Kivuyo alisema kambi hiyo imefadhiliwa na Kampuni ya GSM Foundation hatua ambayo imewezesha huduma za uchunguzi na matibabu kusogezwa karibu na wananchi wa Arusha na maeneo mengine ya Kanda ya Kaskazini.

“Kampuni ya GSM Foundation imetoa mchango mkubwa kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani, tunafurahi kuona mwitikio umekuwa mkubwa kama ambavyo tulitarajia”, alisema Dkt. Kivuyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya GSM Foundation Faith Gugu alisema taasisi hiyo imeamua kufadhili kambi hiyo baada ya kubaini kuwa asilimia 20 hadi 30 ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tawi lake kuu lililopo jijini Dar es Salaam wanatoka Kanda ya Kaskazini.

Faith alisema Kampuni ya GSM Foundation imekuwa ikishirikiana na JKCI kwa muda mrefu, ikiwemo kufadhili matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo lakini pia kutoa vifaa vya matibabu katika Hospitali ya JKCI-ALMC na na sasa imepanga kutoa mashine itakayowezesha kufanyika kwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua katika hospitali hiyo.

 “Kampuni ya GSM Foundation tumekuwa tukishirikiana na JKCI kwa muda mrefu, hata sasa tunawafadhili watoto wanaotoka katika familia duni na wanatakiwa kufanyiwa upasuaji katika Taasisi hii”, alisema Faith

Mkazi wa Levolosi mkoani Arusha Aziza Abdallah alisema amefurahishwa na huduma alizopata katika kambi hiyo huku akiwataka wahudumu wa afya kuendelea kuwahudumia wananchi licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya wagonjwa.

“Wataalamu wanaotoa huduma katika kambi hii wasikate tamaa, waendelee kuwahudumia wananchi kwani kazi yao ni ya wito, tunawapongeza sana”, alisema Aziza.

-         Mwisho - 


Comments

Popular posts from this blog

Serikali yazindua kitabu safari ya upandikizaji wa moyo Tanzania, JKCI yaweka historia mpya ya huduma za kibobezi

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma