Kwa mara ya kwanza JKCI yafanya upasuaji wa myo kwa mtoto wa siku mbili
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada Aid kutoka nchini Uingereza wakimfanyia upasuaji wa kuziba tundu lililopo kwenye moyo wa mtoto wakati wa kambi maalumu ya siku sita iliyokuwa ikifanyika katika Taasisi hiyo na kumalizika jana jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza wakati wa kuhitimisha kambi maalumu ya siku sita ya upasuaji wa moyo kwa watoto iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada Aid kutoka nchini Uingereza na kumalizika jana jijini Dar es Salaam
Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akimpatia
zawadi Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Shirika la Muntada
Aid Ahmet Sasmazel wakati wa kuhitimisha kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa
watoto iliyokuwa ikifanywa na wataalamu hao na kumalizika jana jijini Dar es
Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akimpatia zawadi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Muntada Aid lililopo nchini Uingereza Nayaf Sheick wakati wa kuhitimisha kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto iliyokuwa ikifanyika katika Taasisi hiyo na kumalizika jana jijini Dar es Salaam.
Picha na JKCI
*********************************************************************** ***********************
Na Mwandishi Maalumu - Dar
es Salaam.
Kwa mara ya
kwanza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefanikiwa kumfanyia upasuaji wa
moyo mtoto wa siku mbili aliyezaliwa akiwa na tatizo la kubana kwa mshipa wa damu
unaopeleka damu kwenye mapafu (Severe pulmonary valve stenosis).
Upasuaji huo wa bila
kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Percutaneous balloon pulmonary
valvuloplasty- PBV) umefanyika akatika kambi maalumu ya siku sita iliyokuwa
ikifanywa na watalaamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka mradi wa
Little Heart wa shirika la Muntada Aid lililopo nchini Uingereza.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema ushirikiano huo wa kimatibabu
umeleta matokeo makubwa ikiwemo kufanikiwa kumfanyia upasuaji mtoto wa siku
mbili.
“Hii ni mara yetu ya
kwanza kumfanyia mtoto wa umri huu, mafanikio haya ni matokeo ya msaada wa
vifaa tiba uliofanywa na shirika hili pamoja na serikali yetu ya Tanzania kwa
kuweka mazingira wezeshi na kufanikisha upasuaji huu,” alisema Dkt. Angela.
Aidha Dkt. Angela
ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi alisema jumla ya Watoto 44 wamefanyiwa
upasuaji mdogo na mkubwa ambapo watoto 28 wamefanyiwa upasuaji kwa njia ya
tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab huku watoto 16 wakifanyiwa upasuaji
mkubwa wa moyo wa kufungua kifua.
“Kupitia kambi hiyo
wataalamu kutoka shirika la Muntada Aid wamekuja na vifaa tiba vyenye thamani
ya milioni 50 ili kwa pamoja tuweze kuwasaidia watoto wengi wenye magonjwa ya
moyo ya kuzaliwa nayo”, alisema Dkt. Angela
Katika hatua nyingine Dkt.
Angela alitoa rai kwa wanawake wajawazito kufanya uchunguzi wa mapema ili kubaini
changamoto za moyo kwa mtoto ili waweze kuwasaidia watoto na kuokoa maisha yao.
“Wazazi wa watoto wenye
magonjwa ya moyo wengi wao utufikia wakiwa wamechelewa na matokeo ya kimatibabu
yanakuwa siyo mazuri sana hivyo tunawahamasisha wafike mapema ili kupunguza
changamoto hizo kwani JKCI tunatoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo
mapema kuwalinda watoto”, alisema Dkt. Angela
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Muntada Aid Nayaf Sheikh alisema shirika hilo
limesafiri katika mataifa mbalimbali kuwasaidia watoto wanaohitaji upasuaji wa
kibingwa lakini limeona upekee wa JKCI kutokana na kuwa na miundombinu wezeshi.
“Hii ni mara yetu ya 9
kuja JKCI na mara zote ambazo tumekuwa tukija hapa tumekuwa tukipewa
ushirikiano wa watalamu ambao unatuwezesha kufanya upasuaji wa kibingwa kwa kiwango
kikubwa hivyo watanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla hawana haja tena ya
kusafiri kwenda nje ya nchi kufuata matibabu ya kibingwa”, alisema Sheikh.
-Mwisho-
.jpeg)
.jpeg)





Comments
Post a Comment